Na Saleh Ally
JUZI Jumatatu nilikuwa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es
Salaam nikihangaika na maisha, nilichokiona kilizidi kunishangaza baada ya kuwa
nimeshangaa kwa zaidi ya wiki sasa.
Ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama ambaye ziara yake imeanza hiyo
juzi na kama utakuwa mfuatiliaji utaona mabadiliko katika mambo mengi sana,
hadi alipoondoka nchini siku chache zilizopita.
Mara tu baada ya kukaribia kwa siku ya kuwasili kwa Obama, wiki moja
zaidi nyuma, maandalizi yalipamba moto.
Nilifikiri yangekuwa mambo ya kawaida, lakini barabara hasa zile
tulizoelezwa angepita yeye na msafara wake ambao huenda ni mkubwa kuliko wa
rais yeyote aliyewahi kutembelea nchini, zikaanza kufanyiwa usafi.
Usafishaji wa barabara hizo ni wa aina yake, kuna sehemu zilipigwa
deki, mashimo yakazibwa na mabango yaliyo kwenye taa za barabara pia
yakaondolewa na picha za Obama zikawekwa.
Usafi uliofanyika kwa ajili ya ujio wa Obama, ukarabati wa barabara
mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam umeleta sura mpya, lakini hapo nikawa
najiuliza, kama leo serikali imeweza kupata fedha za kufanya hivyo, kwa nini
isingefanya kabla halafu wakati anatua nchini ingeendelea na mambo mengine?
Ninaamini Rais Jakaya Kikwete alipotembelea Marekani, wala
hawakushughulika na usafi wa barabara kwa kuwa ni maisha ya kila siku. Usafi hadi
aje mgeni sidhani kama ni jambo sahihi. Kutokana na nilichokiona, wazo langu
likaangukia katika mchezo wa soka kwa kuwa huku ni mdau. Kwamba ingekuwa ni
jambo la busara kwa kuwa Obama alikuwa hapa nchini, basi angepata nafasi ya
kutembelea katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Najua utaniambia ni vigumu, lakini naona Obama angekubali kama
angepewa nafasi hiyo kwa kuwa asili yake ni Kenya hapa Afrika Mashariki na nchi
yake ya Marekani inapambana kukuza mchezo wa soka.
Hakuna ubishi Obama anajua mambo mengi kuhusiana na michezo, ushahidi
ni juzi alipomzungumzia Mtanzania, Hasheem Thabeet ambaye anakipiga katika timu
ya Thunder inayoshiriki Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA).
Bila kujali angesema hapana au la, lakini ninaamini kwa mabadiliko
yaliyopatikana katika maisha ya kawaida ya Mtanzania wa Dar es Salaam, basi
soka ya Tanzania ingepiga hatua kwa asilimia kubwa ambayo bila Obama kutembelea
basi itapatikana baada ya miaka mingine 15 ijayo.
Angalia serikali yenyewe imeonyesha kiasi gani inamuogopa Obama au
inataka awe na furaha hata kupita wananchi wake. Ikaamua kufanya kila aina ya
marekebisho, sasa TFF unafikiri italala kama Obama akitembelea pale Karume?
Hakika jibu litakuwa hapana, maana ukarabati utaanza mapema na
inawezekana ujenzi wa viwanja vingine vya mazoezi vikiwemo vile vidogo
vinavyotakiwa kujengwa kwa mujibu wa ramani, ungemaliziwa haraka.
Lakini kwa kuwa lazima Obama angetaka kuelezewa kuhusiana na Ligi Kuu
Tanzania Bara, basi ni dhahiri kwamba angeonyeshwa hata viwanja vinavyotumiwa.
TFF wangeona aibu kuonyesha viwanja vya mikoani wakati ni lazima wamuonyeshe
mgeni huyo.
Ambacho wangekifanya, ninaamini wangetumia ‘akili’ hii, kwamba
wazungumze na uongozi wa viwanja hivyo na kutoa masharti ya kuvikarabati katika
‘standard’ wanayotaka wao TFF, ukarabati huo ungekuwa ni msaada kwa kukuza
viwango vya wachezaji.
Hakuna asiyejua namna asilimia 90 ya viwanja vya mikoani vilivyo na
matatizo sawa, vikiwa na uchafu ambao ni hatari kwa afya ya wachezaji na hata
‘afya’ ya soka ya Tanzania kwa kuwa ni vigumu kukuza viwango.
Lakini siku zote TFF imekaa kimya na kusema yenyewe haimiliki viwanja,
kitu ambacho ni sahihi. Lakini inaonyesha kiasi gani watu wa shirikisho hilo
wasivyoangalia mbele kwa kutaka kufanya mambo kama Ulaya.
Wanajua Shirikisho la Soka England (FA) kweli haliwezi kuhusika na
masuala ya viwanja kwa kuwa kila timu hadi za daraja la nne inamiliki viwanja
vyenye hadhi ya kuchezewa soka. Hapa Tanzania sivyo na wanalijua hilo.
Uthibitisho mzuri wa kuwa viwanja vinapaswa kukaguliwa na shirikisho
hilo hasa watu wake wa ufundi na kupitishwa kabla ya kuanza kwa ligi, ni namna
Cecafa au Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ambavyo hukagua viwanja na kuvikubali
au kuvikataa kutokana na viwango wanavyotaka wao.
TFF inajiepusha kwamba suala la uwanja si la kwake, kikubwa inajua
kama ni ligi itaendelea, maslahi kupitia wadhamini wa ligi hiyo na viingilio
lazima vitapatikana, ndiyo maana inakuwa haijali suala la afya za wachezaji na
kiwango cha ligi husika.
Ingekuwa viwanja vingi havina majukwaa, ninaamini hilo lingewakuna TFF
na wangeshughulikia haraka sana kwa kuwa wanajua wakikosa mapato ni tatizo
kwao. Afya za wachezaji, kupanda kwa kiwango cha ligi hiyo ‘si mali’ yao.
Unaweza kusema TFF inaangalia zaidi mashabiki wanaoingia, lakini bado
haijali afya zao kwani haijawahi hata siku moja kukemea usafi wa viwanja
vinavyochezewa Ligi Kuu Bara. Hiki ni kitu kingine kibaya na sehemu ya
kuonyesha kiasi gani TFF haijalivalia njuga suala hilo.
Mfano na ‘kaushauri’ kadogo tu. TFF ikiamua kuiambia Prisons, lazima
icheze katika uwanja wenye viwango fulani, mfano vyoo visafi, sehemu ya
kuchezea uwanja ya uhakika, unafikiri klabu hiyo itashindwa kukutana na
wamiliki wa Uwanja wa Sokoine na kulifanyia kazi suala hilo? Hata kama itakuwa
ni harambee ya wana Mbeya itapigwa, kwa kuwa wanajua wanaweza kukosa kuiona
ligi kuu.
Hilo ninaamini linawezekana, lakini kuna njia nyingi ambazo zinaweza
kutumika kwa ajili ya kubadilisha mambo hasa kama TFF ikionyesha imepania
kufanya hivyo na kuachana na kuona mambo ni rahisi tu.
Hali halisi inaonyesha TFF ni watu wa kusukumwa au waoga kutokana na
ugeni kama tulivyoona kwa serikali yetu. Hivyo ni vema Obama angepitia pale
Karume kabla ya kuondoka ili awe ametusaidia na wadau wa soka kupata mabadiliko
pia. Kwa heri…
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment