![]() |
| YANGA MAZOEZINI LEO KWENYE UWANJA WA LOYOLA WALIPOKUWA WANAJIANDAA KUIVAA THREE PILLARS AMBAYO IMEGUNDULIKA NI FEKI... |
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeshituka kuwa timu inayoitwa Three Pillars FC kutoka Nigeria ni timu ya magumashi.
Akizungumza leo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema wamewasiliana na Shirikisho la Soka la Nigeria (NFA) na kugundua si timu ya ligi kuu kama ilivyoelezwa.
“Katibu Mkuu wa NFA alituambia kuwa timu hiyo si ya ligi kuu na wao hawajaipa kibali cha kuja hapa Tanzania kuja kucheza.
“Sisi tunaheshimu kanuni za Fifa, hatuwezi kuiruhusu timu kuja kucheza wakati haijaruhusiwa na mwanachama wa Fifa. Hivyo hatuwezi kuruhusu na pia mwandaaji hakuwa na kibali pia cha Fifa.
“Hivyo tunatangaza kufuta mechi hiyo iliyokuwa imeandaliwa na kampuni inayoitwa na Sports Link,” alisema Osiah.
Timu hiyo imeonyesha inaundwa na wachezaji tu wasiokuwa na timu na wako chini ya wakala mmoja ambaye anataka wapate timu za kusajili.
Hivyo amekuwa akizunguka na wachezaji wake ili wapate nafasi ya kusajiliwa, maana yake baada ya mechi ya Yanga, mwenye timu hiyo ambaye ni wakala angeanza kufanya biashara ya wachezaji.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako amethibitisha kuwa mechi hiyo haitakuwepo kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar kama ilivyotakiwa.
“Kweli kwa kuwa timu hiyo ilitakiwa kuwa na kibali ambacho kinatoka katika shirikisho lao huko Nigeria, lakini hawakuwa nacho, hivyo TFF ikazuia,” alisema Mwalusako.
“Mwanzo tuliambiwa timu inatokea daraja la kwanza nchini Nigeria na walitupa barua. Sisi tukataka kuhakikisha na kupata kibali kutoka TFF ambao pia wakawasiliana na wenzao wa Nigeria.”
Lakini taarifa nyingine zimeeleza TFF ilifanya mawasiliano na Shirikisho la Nigeria (NFA) ambalo limeonekana kutoitambua timu hiyo ya kuundaunda.








0 COMMENTS:
Post a Comment