Jaji Steven Ihema na wakili mwandamizi,
Bi Jesse Mguto wataongoza kamati muhimu za za maadili za Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) zilizoundwa baada ya kufanya mabadiliko kwenye katiba ya shirikisho hilo
mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa TFF Leodegar C. Tenga alitangaza jana.
Shirikisho hilo pia limemteua Jaji
Bernard Luanda kuongoza Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wakati Profesa Mgongo Fimbo
ataendelea kuongoza Kamati ya Rufaa za Nidhamu na Kamanda Mstaafu, Alfred
Tibaigana akiendelea kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu.
Rais Tenga alisema hayo wakati
alipoongea na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa
Taifa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho
kikatiba kina jukumu la kuunda Kamati Ndogo za TFF na vyombo vya maamuzi.
“Tulitaka tuwe na watu solid (imara) na
makini ambao watatuhakikishia tunakwenda vyema,” alisema Tenga akizungumzia
uteuzi huo ambao unahitimisha mchakato wa mageuzi kwenye Shirikisho baada ya
Uchaguzi Mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika mwezi Februari kusimamishwa kutokana
na baadhi ya wagombea kupinga kuenguliwa na baadaye kwenda Fifa.
Katika kumaliza tatizo hilo, Fifa ilituma ujumbe wake kusikiliza walalamikaji na watu wengine na baadaye kuagiza
kuundwa kwa Kamati za Maadili na kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa TFF kwa
ajili ya kuingiza vyombo hivyo kwenye katiba kabla ya kuelekea kwenye Uchaguzi
Mkuu wa TFF.
“Tumezingatia pia maoni ya wajumbe wa
Mkutano Mkuu ambao walitaka kamati ziwe na majaji... lakini si rahisi kupata seating
judges (majaji walio kazini) ndio maana tunawashukuru wale waliotuambia kuwa
wako tayari kutusaidia.
“Tumetafuta majaji na mawakili
waandamizi ambao tunaamini watatuhakikishia haki inatendeka na inaonekana
inatendeka,” alisema Tenga na kuongeza kuwa pia walizingatia maombi ya wajumbe
wengine watatu ambao walitaka kupumzika, akiwataja kuwa ni Deo Lyatto,
Sylvester Faya na Idd Mtiginjollah.
Alisema kutokana na mfumo huo mpya,
mambo yote yanayohusu masuala ya ndani ya uwanja sasa yatashughulikiwa na Kamati
ya Nidhamu, wakati yale ya nje ya uwanja, ambayo yanawahusu viongozi na
wanafamilia ya mpira wa miguu kwa ujumla, yatashughulikiwa na Kamati za
Maadili.
Tenga alisema mabadiliko hayo pia
yamegusa kamati nyingine mbili, yaani Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Uchaguzi
ambayo sasa itaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamidu
Mbwezeleni
Jaji Ihema ataongoza Kamati ya Rufaa za
Maadili akisaidiwa na mwanasheria mwingine mwandamizi, Victoria Makani, huku Bi.
Mguto, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza vyombo vya vya maamuzi
ataongoza Kamati ya Maadili akisaidiwa na makamu wake Francis Kabwe, ambaye
Msajili wa Mahakama Kuu.
Katika uteuzi huo, baadhi ya wajumbe
wamehamishwa kutoka kamati moja hadi nyingine. Mhe. Murtaza Mangungu, ambaye
awali alikuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi, sasa ataingia kwenye Kamati ya Rufaa
za Maadili; Kamanda Mohamed Mpinga na Prof Madundo Mtambo wamehamishwa kutoka
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi kwenda Kamati ya Maadili.
Wajumbe wapya kwenye Kamati hizo ni
pamoja na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Mshindo Msolla na
Kamanda Mstaafu Jamal Rwambow wanaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; mwanasheria
maarufu Evodi Mmanda anaingia kwenye Kamati ya Maadili; mwanasheria mwandamizi
Mustapha Kambona ambaye anaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; Mhe. Mohamed Misanga
ambaye anaingia kwenye Kamati ya Maadili na Kanali Iddi Kipingu, ambaye
anasifika kwa kuendesha soka la vijana, anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za
Nidhamu.
Pia Mwanasheria Anne Steven Marealle
anakuwa mjumbe kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi; Yohane Masale (Rufaa za
Uchaguzi), Allen Kasamala (Rufaa za Uchaguzi); Francis Kiwanga ambaye pia aningia kwenye
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi na mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau ambaye anaingia
kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili.
Kamati ya Utendaji pia imefanya
mabadiliko kwenye Kamati ya Waamuzi ambako mwenyekiti Said Nassoro na katibu
Charles Ndagala wa Chama cha Waamuzi wanaingia kwenye kamati hiyo kushika
nafasi ya Joan Minja na Riziki Majala.
Wajumbe wa Kamati hizo ni kama
ifuatavyo:
Kamati ya Rufaa za Maadili ni Jaji
Steven Ihema (mwenyekiti), Victoria Makani (m/mwenyekiti), Mhe. Mohamed
Misanga, Henry Tandau na Mhe. Murtaza Mangungu.
Kamati ya Maadili: Bi Jesse Mguto
(mwenyekiti), Francis Kabwe (m/mwenyekiti), ACP Mohamed Mpinga, Prof. Madundo
Mtambo, na Evod mmanda.
Kamati ya Rufaa za Nidhamu: Prof. Mgongo
Fimbo, Ong’wanuhama Kibuta (m/mwenyekiti), Kanali Mstaafu Idd Kipingu, Dk.
Mshindo Msolla, ACP Jamal Rwambow.
Kamati ya Nidhamu: Kamanda Mstaafu
Alfred Tibaigana (mwenyekiti), Mustafa Kambona (m/mwenyekiti), Azzan Zungu,
Yussu Nzowa na Mohamed Msomali.
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi: Jaji
Bernard Luanda (mwenyekiti), Francis Kiwanga (m/mwenyekiti), A. Steven Semu,
Yohane Masalla na Allen Kasamala.
Kamati ya Uchaguzi: Hamidu Mbwezeleni
(mwenyekiti), Moses Kaluwa (m/mwenyekiti), Mustafa Siani, Hassan Dyamwale na
Kitwana Manara.
Kamati ya Waamuzi: Kapteni Mstaafu
Stanley Lugenge (mwenyekiti), Omar Kasinde (m/mwenyekiti), Said Nassoro,
Charles Ndagala na Mohamed Nyama.








0 COMMENTS:
Post a Comment