| KAZIMOTO (KUSHOTO) AKIWA MAZOEZINI SIMBA.. |
Siku moja baada ya kutoweka katika
kambi ya timu ya taifa, imebainika kiungo nyota wa Simba, Mwinyi Kazimoto
ametimkia nchini Qatar.
Awali kulikuwa na tetesi huenda
Kazimoto amekimbilia nchini humo lakini rafiki yake wa karibu ambaye pia ni
mchezaji amethibitisha.
“Kweli amesema anakwenda Qatar, mipango
imeishakamilika nay eye amekwenda kujaribu bahati,” alisema na alipoulizwa kwa
nini hakuaga.
“Aliogopa, si unaona (Shomari) Kapombe
leo yuko hapa, alipata nafasi ya kwenda Uholanzi lakini TFF ikamzuia na sasa
yupo tu.
“Mwinyi akaona mambo kama ya Kapombe
yanaweza kumkuta, kaamua aondoke na kwenda kujaribu bahati,” alisema rafiki
yake huyo.
Taarifa zinaeleza Kazimoto ameondoka
usiku wa leo, saa tatu usiku na ndege ya Qatar Airways kwenda nchini humo
kujiunga na timu ambayo bado haijajulikana.
“Hiyo timu imemuambia aende na yenye
itajua namna ya kumalizana na Simba,” kilisisitiza chanzo.
Lakini mchana wa leo, TFF imesisitiza
lazima itatoa adhabu kwa Kazimoto ambayo itakuwa ni kufungiwa kutokana na utovu
wa nidhamu wa kutoroka katika kambi ya timu ya taifa.
Kazimoto alitoroka wakati Stars inaondoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kuweka kambi kujiandaa kuivaa Uganda katika mechi ya marudiano kuwania kucheza fainali za Chan.
Hali hiyo ilisababisha Kocha Kim Poulsen amrejeshe kiungo kinda Mudathiri Yahaya ambaye alimuacha katika kikosi kilichokwenda Mwanza kwenda kuweka kambi.
Kama atafungiwa kucheza, huenda ikamtia
ugumu Kazimoto kucheza katika timu aliyokwenda Qatar hata kama Simba watakuwa
wamekubali.







0 COMMENTS:
Post a Comment