Na Saleh
Ally, Strasbourg
SAFARI ya
kwanza nilishindwa kufika katika mji wa Strasbourg nchini Ufaransa, nilibanwa
na kumaliza shughuli zangu katika miji kadhaa ya Ujerumani. Lakini safari hii
niliona ingekuwa muhimu kufanya hivyo kwa ajili ya kujifunza lakini
kuwafikishia wasomaji wanachohitaji.
Niliamua
kusafiri nikitokea mji wa Freiburg nchini Ujerumani na baada ya saa moja na
nusu tu nilikuwa nimeishavuka na kuingia nchini Ufaransa katika mji wa Colmar,
hapo nilipata chakula cha usiku na kuendelea na safari yangu na nilitaka kufika
Strasbourg.
Kwa
wanasiasa, huenda wangedhani niliamua kuingia kwenye rekodi ya watu waliowahi
kufika katika jengo maarufu zaidi la Bunge la Ulaya ambalo liko katika mji huu
wa nane kwa ukubwa nchini Ufaransa na uko Mashariki mwa nchi hii, si mbali
kutoka Ujerumani.
Kama
mwanamichezo nimevutiwa kufika Strasbourg kwa kuwa ndiyo mji aliozaliwa Kocha
Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger, ambaye pamoja na baadhi ya mashabiki wengi
kumbeza, lakini ni maarufu huenda kuliko mwanamichezo yeyote wa Ufaransa katika
eneo lote la nchi hiyo linalopakana na Ujerumani.
Bunge la
Ulaya ni maarufu zaidi, lakini inaonekana baada ya hapo, wengi wanamzungumzia
Wenger, kwani hata wafanyakazi wa bunge hilo, mara kadhaa walikumbushia kwamba
mji huo anatokea Wenger ambaye kwa sasa ndiye kocha maarufu zaidi kutoka
Ufaransa.
Ukiachana na
kwamba ndiye kocha mwenye mafanikio zaidi kuliko wote waliowahi kuifundisha
Arsenal kwa maana ya kutoa vikombe 11 ambavyo ni vingi zaidi, lakini Wenger ni
kocha msomi ambaye nje ya soka, amekuwa na mambo mengi ya ziada kama vile elimu
ya uchumi.
Kitaaluma,
alihitimu ‘masters’ ya uchumi katika Chuo cha Stanford, California, nchini
Marekani na ana uwezo wa kuzungumza lugha kadhaa zikiwemo Kifaransa,
Kijerumani, Kiingereza na Kijapani.
Mji wa
Strasbourg una Wafaransa wengi wanaozungumza Kijerumani na ndiyo mji unaoongoza
kwa kutoa wachapakazi kwa kuwa utamaduni wao umechanganyika na ule wa
Kijerumani. Kawaida Wafaransa wengi wanajulikana kwa kupeleka mambo yao
taratibu kwa madaha, kwa kifupi wana sifa ya uvivu na maneno mengi, lakini
wanaoishi katika mji huu ni majembe.
Asilimia
kubwa ya watu wanaoishi katika mji huu wanajivunia Wenger, mfano katika hoteli
mbalimbali, sehemu za usafiri wa jamii, lakini hata kwenye viwanja vidogo vya
soka, wanaona ni jambo zuri kusema ndiko Wenger alikozaliwa Oktoba 22, 1949.
Ingawa baada
ya kukua, Wenger alihamia katika mji mdogo wa Duttlenheim na kuanza kucheza
katika timu ya FC Duttlenheim iliyokuwa inafundishwa na baba yake, baadaye
alirejea tena katika mji huu na kujiunga na kikosi cha Mutzig na baadaye
Mulhouse.
Kuonyesha
hapa ndipo ‘home’, Wenger alirejea na kujiunga na ASPV Strasbourg ambayo
aliichezea kuanzia mwaka 1975-78 na kuhamia kwa wapinzani wao wa RC Strasbourg
alikocheza mechi 11 tu na baada ya hapo akastaafu soka na kuingia katika ukocha
baada ya kuwa amehitimu diploma ya ukocha.
Mashabiki
wengi wa soka katika mji huu wanamuita Wenger kwa jina la Le Professeur, yaani
Profesa na asili ya watu wengi wa hapa ni wasomi, wanapenda ‘kubukua’ na mara
nyingi ni watu wa vazi la suti na wanajulikana kwa maringo ingawa bado sifa ya
uchapakazi inawalinda.
Alikozaliwa
Wenger leo si kijiji tena, badala yake kuna majengo mazuri tofauti na
ilivyokuwa mwanzo lakini bado asilimia kubwa ya familia yake ni watumishi wa
kanisa kwa kuwa hata yeye akiwa mdogo amewahi kuwa kati ya watumishi wa kanisa.
Kwa timu
zinazoshiriki Ligi Kuu England, mashabiki wengi wa mji huu wanaiunga zaidi
mkono Arsenal kwa sababu mbili kuu, kwanza kabisa ni kwa sababu ya Wenger na
anapewa heshima kama mtu aliyefanya kazi ya ziada kutoka katika familia ya
kimasikini, baadaye kuwa msomi na anayeutangaza mji huu kimataifa.
Pili,
wachezaji wengi kutoka Ufaransa kama Patrick Vieira, Thierry Henry, Robert
Pires, Emmanuel Petit, Silvan Wiltord na wengine wameitangaza sana Ufaransa
kisoka na kikubwa wengi wao walikuwa katika kikosi cha Ufaransa kilichotwaa
ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1998, hivyo Arsenal hapa ni kama nyumbani.
Katika hali
ya kawaida unaweza kudhani umaarufu wa Wenger ni kitu kidogo sana, lakini hali
halisi inaonyesha kocha huyo ana umaarufu mkubwa sana kwa kuwa mji wa
Strasbourg ni kati ya miji mikongwe kabisa duniani na una bandari maarufu na ya
pili kwa ukubwa katika zile zilizo katika mto maarufu Ulaya uitwao Rhines.
Miaka kadhaa
iliyopita Strasbourg ulitangazwa kuwa moja ya urithi wa dunia katika miji bora,
ingawa ni wa tisa kwa ukubwa nchini Ufaransa lakini ulishika nafasi ya tatu kwa
ubora wa mpangilio katika nchi hii na wa 18 duniani.
Strasbourg
ni mji wenye mambo mengi sana ya kumbukumbu na una mpagilio wa majumba mengi
sana ya kizamani ambayo yanabaki kuwa kama kumbukumbu ikiwemo moja ya sehemu
ambayo Wajerumani waliporwa na Wafaransa baada ya vita ya pili ya dunia.
Mmoja wa
wahudumu katika hoteli niliyofikia aliniambia, kuna idadi kubwa kubwa ya vijana
wamekuwa na ndoto ya kuwa makocha bora badala ya wachezaji bora kwa sababu ya
kocha huyo. Lakini hata walioshindwa kufanya vizuri katika soka la kulipwa,
husema wanaweza kuwa makocha wazuri kwa kuwa hata Wenger hakuwahi kunga’ra
wakati akicheza.
Pamoja na
mambo mengi ya kila aina katika mji huo, Wenger anaendelea kubaki namba mbili
katika wanaozungumzwa au maarufu zaidi baada ya bunge la Ulaya ambalo kila wiki
au mwezi, linawakutanisha watu maarufu wa Ulaya au duniani kote.








0 COMMENTS:
Post a Comment