Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepitia usajili wa
wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa
kuchezea timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya
Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine
Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa
kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh.
milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za
mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha
hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa
kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Vilevile Kamati imepitia pingamizi
zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya
wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi Alhamisi
(Agosti 22 mwaka huu).
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni,
Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa
(Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe
zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo
hazikuafikiana.
Hiyo kamati ni ya kipuuzi uwezi kumuizinisha mchezaji akacheze club nyengine wakati mnajua bado ana mkataba na club alotoka. Huu ni upuuzi
ReplyDelete