Na Saleh Ally, aliyekuwa Zurich, USWISS
Kila mmoja anaweza kuwa na ndoto zake,
zangu ni nyingi na sijui kama nitatimiza zote lakini kufanya mahojiano ndani ya
makao makuu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lilikuwa ni jambo kubwa
na muhimu kwangu.
Hivi karibuni, nilisafiri hadi jijini
Zurich, Uswis na lengo lilikuwa ni kufikia ndoto hiyo. Nilitamani kujua Fifa
wanafanya vipi shughuli zao hadi kufikia kufanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja
na kutoa misaada kwa wanachama wake.
![]() |
| ...AKITAZAMA MAKOMBE MBALIMBA YA DUNIA KAMA KOMBE LA DUNIA LA WANAWAKE, VIJANA, KOMBE LA MABARA, KOMBE LA DUNIA LA KLABU NA MENGINEYO YALIYO CHINI YA FIFA |
Mfano, kila mwaka hutoa zaidi ya dola
250,000 (Sh milioni 405) kwa Tanzania ambao ni wanachama. Swali ni je, Fifa
wanaingiza vipi fedha wakati hawana ligi wanayoisimamia moja kwa moja? Kumbuka
kwamba, Fifa pia ni moja ya mashirika au taasisi tajiri kabisa duniani.
Maswali yalikuwa mengi, lakini ilikuwa
shida na ngumu kupata mwaliko hadi siku ilipotimia. Waalikwa wa siku hiyo
walikuwa hawa; waamuzi kutoka Sweden, makocha kutoka Japan, wakala kutoka
Tanzania (Damas Ndumbaro) na waandishi wawili, Amber Lee (ESPN-Marekani) na
Saleh Ally (Salehjembe.com-Tanzania).
Sikutegemea kumuona Ndumbaro pale Fifa,
wakati naingia alikuwa anatoka, nililazimika kumshawishi ili niweze kumhoji na
hivyo ikabidi anisubiri wakati nikiingia katika chumba cha mahojiano na baadaye
kutembezwa katika sehemu mbalimbali za jengo hilo.
![]() |
| ...AKIWA NA WAAMUZI WA FIFA KUTOKA SWEDEN PAMOJA NA OFISA WA FIFA |
Hata hivyo, ombi langu moja la kutaka
kuzungumza na Rais Sepp Blatter liliondolewa, hivyo aliyekuwa anaisimamia ziara
yangu alitaka kujua kilichonipa ujasiri wa kutaka kumuona Blatter, nikampa
majibu, mwisho akasisitiza anaamini siku itafika itakuwa hivyo, yaani nitamuona,
lakini wakati huo alikuwa amebanwa na alikuwa nje ya ofisi.
Kweli Blatter ni mkubwa, lakini hata
Salehjembe ni blog kubwa ya michezo, hata kama kuna kasoro kwa kuwa linaongozwa na binadamu,
hivyo haki ya kumuona na kumhoji bado haipotei.
Nakubali haikuwa bahati au vinginevyo,
lakini nafurahi Salehjembe.com kuwa blog ya kwanza Tanzania kufika Zurich kumsaka
Blatter, hata kama hakupatikana, lakini mahojiano yakafanyika ndani ya mjengo huo.
Katika mahojiano ingawa maswali mengi
yalikuwa hayajibiki kutokana na msemaji niliyepewa kusema hakuwa na mamlaka ya
kujibu, alikubali kwamba kwanza Fifa haiungi mkono migogoro lakini haisaidii
vyama vya soka kupambana na serikali za nchi zao.
“Hatuungi mkono migogoro, soka
linachezwa kwenye amani. Lakini tunasisitiza mambo yaende kwenye msitari kwa
kufuata utaratibu. Lakini pia tunakataa serikali kutumia mabavu kuviingilia
vyama, Tanzania kuna matatizo lakini tunaona hayajafikia katika kiwango
kikubwa.
“Tunaamini siku itafika jibu litapatikana
na mambo yanakwenda vizuri, hivyo lazima kuwe na subira na kama kuna makundi,
basi yawe kwa ajili ya uchaguzi na baada ya hapo watu waungane,” anasema.
“Pamoja na hivyo, mimi nikaangalia zaidi
kuhusiana na Fifa, kwamba inatoa wapi fedha za kuweza kusaidia nchi lukuki,
tena mamilioni ya fedha.
“Fifa inategemea mapato yake katika haki
ya mambo kadhaa, lakini matangazo ya TV ndiyo yanaingiza fedha nyingi sana na
hasa katika michuano ya Kombe la Dunia.
“Kati ya mwaka 2007 na 2010, kulikuwa na
mafanikio na mabadiliko makubwa katika kipato chetu, tulifanikiwa kuingiza hadi
dola bilioni 4.189 (Sh trilioni 6.8) ukilinganisha na miaka minne ya nyuma
tuliyokuwa tumeingiza dola bilioni 2.634 (Sh trilioni 4.3).
“Wakati wa Kombe la Dunia la Afrika Kusini
ndiyo kulikuwa na mabadiliko makubwa zaidi ya kipato kwa Fifa. Tuliingiza dola
bilioni 2.408. Kati ya hizo dola bilioni 1.072 zilitokana na mapato ya haki za
matangazo.
“Pamoja na kwamba tunaingiza fedha
nyingi kutoka kwa wadhamini lakini Kombe la Dunia pekee liliingiza takribani
asilimia 87 ya mapato yote.
“Haya yalikuwa mapinduzi makubwa ya
kiuchumi, haraka baada ya hapo, timu yetu ya wachumi ikaongezwa nguvu, imekuwa
kubwa zaidi kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kutanua soko.
“Tunataka kuingiza fedha nyingi zaidi
kwa kuwa tuna matumizi makubwa. Hivyo tuna wataalamu wa uchumi kutoka makampuni
makubwa kabisa duniani, wengine ni maprofesa na ndiyo wanaoendelea kutufanyia
uchunguzi,” anasema.
Hapo nikaanza kugundua ‘akili’ ya haraka
ya Fifa na tofauti yake na ile ya TFF ambayo ina mtu mmoja tu wa masoko, tena
ambaye hasikiki hata chembe na haijulikani kama anafanya kazi ya kutafuta
masoko au la.
Kweli TFF inafanya kazi ya mpira, lakini
najiuliza ina juhudi zipi kuwavuta wadhamini lukuki ili kupata mafanikio zaidi,
hasa kwa kuwa kama wakijitokeza na kutoa fedha ndiyo maendeleo yenyewe? TFF
inapata misaada kutoka Fifa kwa kuwa shirikisho hilo la kimataifa limeajiri
‘wakali’ wa masuala ya uchumi ili kupata faida.
Hapa nyumbani ni tofauti, inawezekana soko
halipewi umakini mkubwa, hili si suala la leo, maana mgogoro kati ya Yanga na
Azam TV usiwe kisingizio, lakini TFF lazima ikubali, lazima kuwe na juhudi za
makusudi za kutafuta masoko.
Hakika haiwezi kuingiza mabilioni kama
ya Fifa, lakini inaweza kupata fedha zaidi na kujenga mafanikio ambayo
yataiwezesha kusaidia ipasavyo vyama vya wilaya na mikoa.
Fifa inapeleka mamilioni ya fedha katika
nchi nyingi ikiwemo Tanzania, hata TFF ikiwa na mipango, siku moja itapeleka
fedha wilayani na mikoani na mwisho mafanikio yatapatikana kwa kuwa fedha inasaidia
mabadiliko.
Hakutakuwa na maendeleo kama TFF itakuwa
ni ya Dar es Salaam tu. Angalia Fifa inajua Ulaya na Marekani ndiyo Dar es
Salaam na wanajiendeleza wenyewe. Lakini Afrika ndiyo mikoani, inapeleka misaada
na mambo yanakwenda.
Mfano katika fedha hizo inazoingiza, nyingi
pia zinatumika Afrika, Amerika Kusini na Asia na moja ya miradi yake mikubwa ni
ule wa kujenga viwanja wa Goal Project. Tayari Tanzania Bara na Zanzibar zimeshafaidika.
Sasa kuona fedha tu za Fifa zinatua
nchini kama mvua na hakuna anayejifunza kutoka katika shirikisho letu, mimi
naona si sahihi. Inawezekana nikawa nimejifunza mengi kutokana na maswali
yangu, lakini hili lilinigusa zaidi, ninaamini TFF wanaweza kujitanua zaidi.
Soka ni utajiri, hasa ikipata watu
makini wanaolenga maendeleo. Haitakuwa rahisi, lakini waliokabidhiwa dhamana
lazima wakubali kuumia na kuchoka kwa ajili ya kuleta maendeleo, nasi tuwaamini
na kuwapa nafasi.
TFF inaweza kusaidia kukua kwa soka kwa
kujali vijana na kusaidia soka vijijini, wilayani na mikoani lakini hata kama
programu zitakuwa vipi, lazima kuwe na fedha ambazo zitapatikana kwa kuwa na
watu wabunifu na makini wa kuzitafuta.











0 COMMENTS:
Post a Comment