Na Saleh Ally aliyekuwa Zurich
Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) zilizo jijini New York nchini Marekani, thamani yake ni dola milioni 65 (zaidi ya Sh bilioni 104).
Jengo hilo maarufu ni kati ya majengo bora na maarufu duniani, lilijengwa mwanzoni mwa miaka ya 1950. Ingawa lengo si kulinganisha, lakini jengo la makao makuu ya Shirikisho la Soka (Fifa) yaliyoko jijini Zurich nchini Switzerland, linautofauti na nataka kuonyesha nguvu ya soka katika ulimwengu huu.
Jengo la Umoja wa Mataifa (UN) unaweza kusema ni makao makuu ya dunia, thamani yake ni pauni milioni 65, wakati jengo la Fifa thamani yake ni zaidi ya pauni milioni 200 (zaidi ya Sh bilioni 520).
Unaweza kusema kwa kuwa moja limejengwa zamani, hili la Fifa lilijengwa kuanzia mwaka 2004 tu, liko katika eneo la Zurichberg. Thamani yake ni kubwa sana ingawa linazidiwa kwa ukubwa na lile la Umoja wa Mataifa (UN).
Achana na mambo ya thamani, kwa kuwa nilipata nafasi ya kutembelea katika jengo hilo, nikaona vizuri kuelezea kutokana na mambo mengi yaliyopo.
Ukiwa katika Jiji la Zurich, wakati unafika katika Mtaa wa Fifa (Fifa Strasse), utulivu ni wa hali ya juu sana kulinganisha na maeneo mengi na ajabu zaidi katika jengo hilo maarufu na lenye thamani kubwa, hakuna askari hata mmoja anayeonekana analinda.
Mfano ukienda TFF wakati mwingine kuna mlinzi anayefungua mageti na anahoji unafuata kitu kipi, pale geti liko wazi na unaingia, umbali wa mita takribani 500 ndiyo unaanza kufika katika jengo hilo na hautakutana na askari atakayekuuliza.
Unaweza kudhani hakuna ulinzi, lakini ukweli ni kwamba ndani yake kuna zaidi ya kamera 70 za siri ambazo kuna watu walio katika chumba maalum wanaziendesha na kufuatilia kila kitu, kama ikitokea ukakosea, mara moja kundi la walinzi linaibuka.
Zaidi ya walinzi 15 wanakuwa tayari kwa tukio lolote, lakini nao wanakuwa katika chumba maalum ambacho kipo chini ya ardhi. Inawezekana wakawa wachache ukilinganisha na ikulu, lakini lilivyojengwa huenda ni zaidi ya ikulu.
Sehemu ya mapokezi ya Fifa ni kubwa takribani nusu uwanja wa soka, eneo kubwa liko wazi na zaidi sehemu ya mapokezi, sehemu ya makochi kwa ajili ya wageni pia kuna mipira iliyotumika katika Kombe la Dunia tokea mwaka 1974, halafu makombe mbalimbali ambayo yako chini ya shirikisho hilo likiwemo lile la dunia.
Mapokezi:
Watu wachache na mara nyingi wafanyakazi wanapita kuingia kwenye lifti. Nje ya jengo hilo kuna gym kwa ajili ya wafanyakazi na juu yake umejengwa uwanja maridadi wa soka, wafanyakazi wamekuwa wakiendelea na mazoezi.
Ukirudi pale upande wa mapokezi katika jengo hilo ghali zaidi katika ofisi za soka duniani, kwenda juu kuna ghorofa mbili tu lakini kivutio zaidi ni urefu wake kwenda mbele. Yaani tokea pale mapokezi, unaweza kutembea urefu wa viwanja viwili vya soka kufikia kona nyingine.
Kivutio ni makochi machache na yenye mpangilio mzuri, ukiachana na makombe kuna taa maalum ambazo zinatumia maji na mwanga wake unaongezeka kutokana na ukubwa wa kiza.
Paa:
Paa na jumba hilo, asilimia 25 limeezekwa kwa vioo na lina jumla ya tani 500 ya vioo na tani 250 ya vyuma.
Ghorofa:
Kivutio zaidi katika jengo hilo, kwamba unapokuwa pale mapokezi ni ghorofa mbili tu kwenda juu. Lakini kwenda chini kuna ghorofa nyingine tano, hivyo kufanya liwe na jumla ya ghorofa saba.
Asilimia 75 ya ofisi muhimu ya jengo hilo ziko ardhini na chache ndiyo ziko katika eneo la juu.
Nilihoji kwa nini iwe hivyo, inaonekana ulikuwa ni mpango wa mbunifu wa jengo hilo raia wa Swiss mwenye asili ya Ujerumani ambaye ndiye mbunifu wa jengo hilo.
Alifanya hivyo kwa kuleta mabadiliko katika ujenzi wa majumba, lakini linaaminika ni salama zaidi na ghali zaidi kutokana na ujenzi wake mkubwa kufanyika chini ya ardhi.
Blatter:
Ulinzi wa Sepp Blatter ambaye ni rais wa Fifa unalingana na marais wengi maarufu hasa anapokuwa katika eneo hilo, kwanza ni nadra sana kujua wakati anaingia au kutoka ofisini hapo.
Mmoja wa watu wa mapokezi anasema wakati mwingine humuona Blatter kila baada ya miezi sita au mwaka.
Hii inatokana na kiongozi huyo mkubwa zaidi wa soka duniani kutumia geti la magari linalopita chini ya ardhi. Maegesho ya magari yote yako chini ya ardhi.
Lakini Blatter anakuwa na sehemu yake maalum mara baada ya kuingia chini, ingawa wamekuwa wakifanya siri kubwa kuhusiana naye kuwekewa ulinzi mkali lakini sehemu anayoegesha gari ni vigumu risasi au mabomu ya saizi ya kati kupenya.
Ukumbi:
Ndani ya jengo hilo kuna ukumbi mkubwa wa mikutano ambao unaweza kuchukua zaidi ya watu 2001 na huu uko katika ghorofa ya kwanza upande wa juu. Lakini ndani yaani chini ya ardhi kuna ukumbi mwingine ambao unaweza kuchukua hadi watu 30.
Ukumbi huu wa chini ya ardhi zaidi umekuwa ukitumiwa na Blatter au maofisa wengine wa juu wa Fifa kwa ajili ya kufanya mikutano maalum ya ndani au ile inayohusisha watu kutoka nje.
Viwanja:
Nje ya jengo la Fifa kuna zaidi ya viwanja sita vya soka katika ukubwa tofauti. Vingi vinatumiwa na wafanyakazi lakini hiyo ni sehemu ya nembo kuonyesha eneo hilo ni sehemu ya soka.
Bustani:
Bustani kubwa imelizunguka jengo hilo, lakini imetengwa kwa kufuata mashirikisho makubwa yaliyo chini yake ambayo ni Caf, (Afrika) Uefa (Ulaya), Conmebol (Amerika Kusini), OFC (Ocenia), AFC (Asia) na Concacaf (Amerika Kaskazini).
Pamoja na bustani hiyo kuna sehemu maalum ambayo ina bendera pamoja na majina ya wanachama wote wa Fifa ikiwemo Tanzania.
Lugha rasmi za shirikisho hilo ni nne ambazo ni Kingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kihipaniola.








0 COMMENTS:
Post a Comment