Watanzania Crescentius Magori na
Lina Kessy wameteuliwa kuwa wajumbe kwenye kamati ndogondogo (standing
committees) mpya za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) zilizotangazwa
juzi na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Hicham El Amrani.
Magori na Lina ambao ni wajumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF watakuwa kwenye kamati hizo kwa kipindi cha miaka
miwili (2013-2015). Magori ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya
Mashindano ya Mpira wa Miguu wa Ufukweni (Beach Soccer) wakati Lina ameingia
kwenye Kamati ya Maandalizi ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake.
TFF tunawapongeza kwa uteuzi huo
ambao umetokana na uwezo ambapo ni imani yetu kuwa wataiwakilisha vizuri
Tanzania na uzoefu watakaopata kupitia kamati hizo utakuwa msaada mkubwa kwa
ustawi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
Naye Makamu wa Rais wa TFF, Athuman
Nyamlani ameteuliwa tena kuwemo kwenye Bodi ya Rufani ya Caf yenye wajumbe 12
kwa kipindi kingine cha miaka miwili. Nyamlani alikuwepo kwenye bodi iliyopita,
na itaendelea kuwa chini ya uenyekiti wa Prosper Abega kutoka Cameroon.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye pia
ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Caf yuko kwenye kamati tano za Shirikisho
hilo. Kamati hizo ni Kamati ya Fedha ambayo ni Makamu Mwenyekiti na Kamati ya
Maandalizi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).
Kamati nyingine ni Kamati ya Masoko
na Televisheni ambayo ni Mwenyekiti, Kamati ya Ufundi na Maendeleo, na Kamati
ya Ushauri na Vyama Wanachama wa Caf.








0 COMMENTS:
Post a Comment