KIWA
unatembea katika mitaa mbalimbali ya miji ya Ufaransa, kuna mambo mengi ambayo
unaweza kujifunza kama utakuwa unataka kuchunguza.
Kwa kuwa
nimefika katika nchi zaidi ya tano za bara la Ulaya, Ufaransa inaonekana ndiyo
nchi yenye Waafrika au watu wengi zaidi wenye asili ya bara la Afrika ambao
wanaishi katika nchi hiyo.
Wako wale
ambao wazazi wao walihamia tokea kitambo, wengine wamehamia kutoka katika nchi
zao hivi karibuni lakini kwa kifupi huenda ikawa ndiyo nchi ambayo ubaguzi wa
rangi kwa Waafrika ukawa si katika kiwango cha juu kama utalinganisha na
Hispania, Italia, Ujerumani na kwingineko.
Huenda
England pia ikawa inaikaribia Ufaransa, lakini katika miji miwili ya Colmar na
Strasbourg nchini Ufaransa niliyoitembelea, hali hiyo inajionyesha wazi na
huenda hakuna mtu anayeonyesha kunishangaa sana kama mgeni pale ninapokuwa
ninakatiza mitaa kwa mwendo wa mdundo.
Hali hiyo ya
mitaani, ndiyo jibu sahihi katika Ligi Kuu ya Ufaransa maarufu kama Ligue 1
ndiyo ligi kubwa duniani ya soka ambayo wachezaji wengi wenye asili ya Afrika
wameweza kufanya vizuri na baadaye kuibuka na kuwa maarufu.
Haina maana
ni Waafrika pekee ambao wanajulikana, wako wengi wakiwemo Wafaransa wenyewe
wasio na asili ya pembeni, lakini hali halisi ni kwamba hakuna ligi nyingine
maarufu duniani ambayo wachezaji wenye asili ya Afrika wamepata umaarufu mkubwa
kama ligi hii.
Kama
ukifanya hesabu za haraka kwa sasa, katika timu kubwa tatu za Ufaransa kama
Olympique de Marseille, AS Monaco na PSG utagundua kuna zaidi ya wachezaji 35
katika vikosi vyote kuanzia za vijana hadi kikosi kikubwa.
Lakini kama
ni vikosi vikubwa, basi ni zaidi ya wachezaji 15 kwa jumla ya timu zote hizo,
kitu ambacho si rahisi kutokea katika ligi kama zile za England au Premiership,
La Liga ya Hispania na Serie A ya Italia.
Wachezaji
lukuki wenye mafanikio au majina makubwa kutoka Afrika au wenye asili ya Afrika
wamepitia Ufaransa kabla ya kwenda kwenye ligi nyingine na kupata umaarufu
mkubwa.
Achana na
wale wenye asili ya Ulaya kama Michel Platin, Éric Cantona, Didier Deschamps,
Christophe Dugarry, Fabien Barthez, Emmanuel Petit, Laurent Blanc Mikel Arteta
na wengine wengi. Lakini angalia hawa wafuatao ambao asili yao ni Afrika na
wamekuza soka lao nchini humo.
Zinedine
Zidane, Basile Boli, , Nicholas
Anelka, Marcel Desailly, Jean Djorkaeff,
Jean Tigana, Abeid Pele, Didier Drogba, Lilian Thuram, Thierry Henry, Youri
Djorkaeff, Patrice Evra, Hatem Ben Arfa na wengine kibao ambao unaweza kutumia
muda wako kidogo tu kuwakumbuka.
Wengine ni
George Weah alitokea moja kwa moja Cameroon ambako alikuwa anacheza soka baada
ya kuchukuliwa kutoka kwao Liberia. Akapaa hadi Ufaransa kwa nguvu za Arsene
Wenger, baadaye akaja kuwa mchezaji bora wa dunia.
Lakini
angalia pamoja na kupita Tanzania, Afrika Kusini na Uswis, jina la Shabani
Nonda lilipaa zaidi na kupata soko kubwa baada ya kuanza kucheza katika timu za
Ligi Kuu ya Ufaransa.
Wako wengi
wengine ambao walifanya vizuri hapa kama Mnigeria Victor Ikpeba aliyekuwa lulu
akitokea Monaco, lakini Emmanuel Adebayor kutoka Togo pia akatengeneza jina
kutoka hapa na sasa ni kati ya wachezaji maarufu kabisa kutoka Afrika.
Ligi ya
Ufaransa ni ya ushindani mkubwa kutokana na vipaji vingi, ndiyo maana timu
nyingi tajiri kutoka katika ligi za England, Italia na Hispania huona ni rahisi
zaidi kupata wachezaji hapa na kuwatumia.
Inakuwa ni
nadra mchezaji nyota wa England kuja kucheza hapa baada ya kufanya vizuri huko
au Hispania, labda kama atakuwa anakaribia kustaafu ingawa PSG na Monaco zikiwa
chini ya mabilionea wa Kiarabu zinaanza ‘kupindua kabati’ kwa kugeuza mambo
kwani sasa ziwanunua wachezaji maarufu kutoka katika ligi hizo kubwa duniani na
si kuuza pekee kama ilivyokuwa awali.
Beki wa SRC
Colmar inayoshiriki ligi daraja la pili Ufaransa, Jean Verger, anasema hajawahi
kusikia mchezaji analalamika kwa kubaguliwa kwa kuwa Ufaransa ndiyo nchi ya
Ulaya inayoongoza kwa kuwa na mchanganyiko wa jamii nyingi zaidi.
“Nimeanza
kucheza soka nikiwa na miaka tisa, sasa nina miaka thelathini na nimekuwa
najiandaa kustaafu ndiyo maana nasomea ukocha. Lakini Ufaransa ndiyo nchi yenye
watu wote duniani na wanaishi sawa.
“Ukisema
umbague mweusi kutoka Afrika, kuna wengi tu ambao si weusi ambao wanatokea
Afrika. Watu kutoka Tunisia, Morocco na Algeria. Utaona hadi kuna sehemu
zinajulikana kuwa ni maeneo kwa ajili yao tu.
“Lakini hata
imani za kidini, hapa watu wana nafasi kubwa ukilinganisha na sehemu nyingine.
Ufaransa ni nchi huru ya kila mmoja. Lakini serikali ya hapa ni wakali sana kwa
anayevunja sheria kwa kuwa wanataka watu waishi pamoja kwa amani,” anasema
Verger.








0 COMMENTS:
Post a Comment