Sakata la
ujio wa mtu anayedaiwa kuwa katibu mpya wa Yanga, Patrick Naggi limechukua sura
mpya, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuitisha kikao cha dharura, lakini yeye
mwenyewe akaeleza kila kitu juu ya ujio wake.
Naggi alifika
katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Jumanne
wiki hii ambapo alikutana na maswali mengi. Kesho yake Baraza la Wazee wa Yanga
likatoa tamko rasmi la kutomtambua bosi huyo ambaye aliwahi kuwa kiongozi mzito
ndani ya Shirikisho la Soka nchini Kenya (KFF), akiwa kama mkurugenzi wa
ufundi.
Wakati Kamati
ya Utendaji ya Yanga ikikutana jana jioni tayari kwa kumtambulisha Naggi, bosi
huyo ameliambia Championi Ijumaa jana kuwa, alishangazwa na hali aliyokutana
nayo mara baada ya kuwasili katika jengo la klabu hiyo, ambapo alifika hapo
kuangalia mazingira ya klabu hiyo.
Naggi amesema
bado hajasaini mkataba wowote na uongozi wa Yanga katika kuanza kazi rasmi,
ambapo ametamka kwamba hana tatizo na yeyote ndani ya Yanga huku akiahidi
kuleta mabadiliko makubwa endapo atamalizana na kukubaliana juu ya kufanya kazi
hiyo.
“Hakukuwa na
tatizo kubwa, ingawa nilishangazwa na vile nilivyokuwa nikihojiwa, ngoja
nikwambie, sikwenda pale kuanza kazi rasmi ila nilikwenda kuangalia mazingira
na ofisi za timu, siwezi kufanya hivyo kwa kuwa bado sijakabidhiwa ofisi
rasmi,” alisema Naggi huku akiongeza kwa kusema:
“Sitaki kukwambia
nani alinipeleka pale kwa kuwa itakuwa kama nataka kuyarefusha haya, nikwambie
tu sina tatizo na mtu yeyote wa Yanga, nimekuja tayari kwa kazi, kama
tutakubaliana na viongozi nitaleta mabadiliko makubwa ndani ya Yanga.”
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment