September 6, 2013





Na Saleh Ally
Uamuzi wa uongozi wa juu wa Yanga umeingia katika mgogoro baada ya kuamua kumpa ajira Katibu Mkuu mpya, Patrick Naggi raia wa Kenya.

Wazee wa Yanga wakiongozwa na Yahaya Akilimali walianzisha tafrani na moja kwa moja wakapinga ujio wa Naggi ambaye walisema walizungumza naye baada ya kufika klabuni hapo.


Kutua kwa Naggi katika Klabu ya Yanga kumezua tafrani kubwa, Akilimali amefikia hatua ya kumuita ‘Kanjanja’ kwa madai ya kushindwa kujieleza mara baada ya kufika klabuni hapo ambapo alijitambulisha kama katibu mkuu mpya wa Yanga.


“Tukamkaribisha na kumuuliza habari za Kenya, akajibu nzuri. Tulipomuuliza tumsaidie nini, akasema yeye ni katibu mkuu mpya. Tulipomuliza aliyemleta, hapo ndiyo hakujibu kabisa.

Sasa hapa tunaingia hofu kuhusiana naye. Ndiyo maana kwa umoja tumepitisha hili kwamba hatutaki kumuona klabuni,” alisema Akilimali.


Wakati mzee huyo akisema hayo, huenda Watanzania wengi watakuwa na hamu ya kujua hasa kuhusiana na Naggi ni mtu gani hasa.

Naggi ni kati ya makocha wachache wa daraja A wanaotambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), ndiyo maana aliwahi kushika vyeo kadhaa vinavyohusiana na masuala ya ufundi kuanzia katika timu mbalimbali hadi Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Lakini Naggi amekuwa kati ya viongozi ambao wamekumbana na matatizo kibao katika kipindi kifupi tu tokea aanze kujulikana kama kiongozi wa masuala ya soka.

Kocha:
Hivi karibuni aliwahi kusema yuko tayari kuchukua kazi ya kuifundisha timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) huku akikumbushia mafanikio yake ya kuiwezesha Nzoia Sugar kubeba ubingwa mwaka 2000.
Lakini pamoja na mafanikio hayo na kuwa kocha mwenye leseni A anayetambuliwa na Caf, akaambulia patupu na hakuna timu iliyomchukua.

Kashfa ya mipira 100:
Mipira 100 ilielezwa kupotea kusikojulikana na Naggi akiwa ndiye Mkurugenzi wa Soka wa FKF akajikuta akisimamishwa kwa miezi sita ili kupisha uchunguzi.

Ilielezwa mipira hiyo 100 ilitolewa na Caf kwa ajili ya timu za taifa za Kenya, ukianzia ile kubwa hadi zile za vijana. Lakini ikapotea kusikojulikana, Naggi akawa mtuhumiwa namba moja, Rais wake, Sam Nyamwea, akamsimamisha.

Ingawa yeye alisisitiza kwamba uongozi wa juu ulikuwa na haraka kwa kuchukua uamuzi wa kumsimamisha bila ya kumueleza, lakini msimamo ukashikiliwa.

Pamoja na kujitahidi kujitetea, wakati huo aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa FKF aliyetimuliwa, Sammy Sholei, naye alimtetea Naggi kwamba shirikisho hilo lilifanya haraka bila ya kumpa nafasi hata ya kujieleza.

Kuchafuliwa Fifa:
Naggi alikuwa mkurugenzi wa ufundi wa FKF lakini Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liliamua kuisaidia Kenya na mshahara wake ulikuwa unatoka moja kwa moja Zurich, Uswiss yalipo makao makuu ya shirikisho hilo.
Baada ya kupewa taarifa kwamba Naggi alihusishwa na kashfa ya upotevu wa mipira na alikuwa amesimamishwa kazi, moja kwa moja akaingia katika kashfa kubwa.
Wengine walisema baadhi ya viongozi wa juu wa FKF walikuwa hawafurahishwi na Naggi kupata malipo yake moja kwa moja kutoka Fifa, hivyo wakaamua kumuondoa au kumtafutia kashfa makusudi.

Kisa gazeti, ashambuliwa:
Maisha ya Naggi yamepitia katika matukio mengi ya vituko, achana na kusimamishwa, kukosa timu na mengine lakini mashabiki wa soka wa Kenya waliwahi kumshambulia, kisa kusoma gazeti.

Ilikuwa ni katika mechi kati ya wenyeji Kenya na wageni wao Uganda na mwisho wa mchezo wenyeji walilala kwa mabao 1-5.
Wakati Kenya ikiwa nyuma kwa mabao mawili, huku Waganda wakiendelea kuihangaisha, Naggi alionekana asiye na hofu hata kidogo huku akisoma gazeti lake.

Mara baada ya bao hilo, mashabiki walitupa jicho katika sehemu ya watu maarufu ‘VIP’ na kumuona Naggi akiwa ‘bize’ na kusoma gazeti huku haangalii mchezo huo uliokuwa unaendelea.

Hali hiyo iliwaudhi mashabiki hao ambao walianza kupiga kelele wakimzomea kutokana na kuonyesha hakuwa akijali kuhusiana timu ilivyokuwa inacheza kwa zaidi ya dakika 15 akionekana kusoma gazeti.

Mashabiki hao walianza kuimba kwa nguvu, “Naggi aondoke, Naggi aondoke”. Hali ilizidi kuwa mbaya hadi ikafikia baadhi ya viongozi waliokuwa VIP wakatoa ushauri Naggi aondoke eneo lile.

Kweli Naggi akalazimika kurudi katika viti vya nyuma ili kupunguza hasira za mashabiki waliokuwa uwanjani pale ambao walisisitiza lazima aondolewe katika nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi wa FKF.
Inawezekana ni mtu wa “majanga” au “bahati mbaya”, matatizo kama hayo ya kulazimishwa kuondolewa kazini au kusakamwa, yamemkuta tena Naggi dakika chache tu baada ya kukanyaga klabu Yanga.
Wazee wametangaza kutomtaka tena, wamesema ndani ya saa 24 aondoke na hawataki kumuona tena.
FIN.
  


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic