Beki wa kimataifa wa Yanga raia wa
Rwanda, Mbuyu Twite, amestaafu rasmi kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo akieleza
kuwa ni kutokana na kuzidiwa na kazi za Yanga huku taarifa nyingine zikisema ni
kutokana na kufanyiwa vitendo vya kibaguzi.
Kikizungumza na Championi Ijumaa, chanzo
kutoka ndani ya klabu hiyo ambacho hakikutaka kuandikwa jina lake, kilisema
Twite aliamua kujitoa kutokana na kufanyiwa vitendo vya kibaguzi kufuatia kuwa
na uraia wa nchi mbili za Rwanda na DR Congo.
Kilisema hivi karibuni beki huyo
aliitwa timu ya taifa kwa ajili ya kucheza mchezo wa kirafiki lakini alikataa
na sasa hivi ameitwa tena kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia pia
amegoma.
“Twite amejitoa kwa sababu anahisi
anafanyiwa ubaguzi kwa kuwa yeye ana uraia wa nchi mbili, ndiyo maana hata
alipoitwa kwenye mechi ya kirafiki alikataa.
“Pia juzikati ameitwa kwenye mchezo wa
kuwania kufuzu Kombe la Dunia, pia amegomea na kumuacha mwenzake Niyonzima
(Haruna) akiondoka peke yake,” kilisema chanzo hicho.
Championi lilimtafuta beki huyo ambapo
alikiri kutojiunga na kikosi hicho cha Rwanda na kudai kuwa ameamua kustaafu
kuichezea timu hiyo kutokana na kuwa na kazi nyingi katika klabu yake.
Alisema anatarajia kuiandaa barua na
kuipeleka katika Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) kuwaeleza kuhusiana na
sakata hilo.
“Mimi nimeamua kustaafu kuichezea
Rwanda kwa kuwa nina kazi nyingi sana hapa Yanga, hakuna shinikizo lolote katika
hili na nitaandaa barua ili niwapelekee taarifa juu ya suala hili,” alisema
Twite aliyejiunga Yanga akitokea APR ya Rwanda, msimu uliopita.
0 COMMENTS:
Post a Comment