Na Ezekiel Kamwaga
KLABU
ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwa umma kuhusu masuala yanayoihusu
kwa sasa.
Kuhusu
Emmanuel Okwi
KATIKA siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari
hapa nchini vimeripoti kuhusu uwepo nchini wa aliyekuwa mchezaji wa zamani wa
klabu, Emmanuel Arnold Okwi kutoka nchini Uganda.
Taarifa hizo zimeeleza mambo mbalimbali ikiwamo taarifa
kuwa Simba Sports Club ina mawasiliano na mchezaji huyo na alikuja kwa mwaliko
wa viongozi wa klabu. Baadhi ya vyombo vimekwenda mbali zaidi na kudai kuwa
uongozi wa Simba unamshawishi mchezaji huyo avunje mkataba wake na klabu
anayoichezea sasa ya Etoile du Sahel (ESS) ya Tunisia.
Klabu inapenda kuuarifu umma kwamba Simba au kiongozi
wake yeyote (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na
Sekretarieti haijahusika kwa namna yoyote ile na ujio wa mchezaji huyo hapa
nchini. Hakukuwepo na mwaliko rasmi au usio rasmi kwa viongozi wa Simba.
Taarifa zozote za kuhusisha ujio wa Okwi na uongozi wa
Simba ni za upotoshaji na zina lengo la kuharibu heshima na hadhi ambayo
uongozi huu umeijenga kitaifa na kimataifa kwenye tasnia ya soka.
Hata hivyo, kisheria, Simba haiwezi kumzuia mchezaji
huyo kusafiri kwenda nchi yoyote anayotaka kama amefuata sheria zote za
uhamiaji. Mchezaji huyo ana mkataba na timu nyingine na Simba haihusiki na
safari zake, matembezi yake au mipango yake ya kimaisha.
Uongozi wa Simba unafahamu kwamba Okwi ni mchezaji
halali wa ESS maana wenyewe ndiyo uliomuuza kwa klabu hiyo. Kwa mujibu wa
sheria za FIFA, klabu yeyote, ikiwamo Simba SC, haziruhusiwi kufanya
mawasiliano na mchezaji huyo au yeyote yule halali wa klabu nyingine bila
ruhusa ya klabu yake kama mkataba wa mchezaji husika umebakiza kipindi
kinachozidi miezi sita. Hii maana yake ni kwamba uongozi hauwezi kumshawishi
mchezaji huyo kujiunga na klabu.
Ikumbukwe kwamba hadi sasa, klabu ya Simba, inaidai
klabu ya Etoile du Sahel kiasi cha dola za Marekani 300,000 (laki tatu) ambazo
zinapaswa kuwa zimelipwa kabla ya tarehe 30 mwezi huu wa tisa mwaka 2013. Kinyume
cha hapo matokeo mengine yataamuliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya FIFA ambapo makubaliano husika yalisajiliwa.
Uongozi wa Simba ungeomba vyombo vya habari na watu
binafsi waache kutoa taarifa zozote za kuhusisha ujio wa Okwi na klabu au
kwamba kuna mipango ya kumshawishi avunje mkataba wake kwani taarifa hizo
hazina ukweli wowote.








0 COMMENTS:
Post a Comment