September 27, 2013



 
TWITE (KULIA) AKIWA MAZOEZINI YANGA NA JUMA ABDUL NA SAID BAHANUZI
Beki wa Yanga raia wa Rwanda, Mbuyu Twite amezidi kuandamwa na mikosi msimu huu, baada ya sasa kubainika wakati wowote anaweza kufukuzwa katika nyumba aliyopanga kutokana na kushindwa kulipa kodi.


Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na beki huyo mwenye asili ya DR Congo, ni kuwa yupo katika wakati mgumu kwa kuwa kodi ambayo alilipiwa na uongozi wa Yanga imeshamalizika na anatakiwa kulipa tena.

Chanzo cha habari kimeeleza kuwa nyumba hiyo iliyopo maeneo ya Kinondoni jijini Dar, Mbuyu analipiwa kodi na uongozi wa klabu hiyo kwa mujibu wa mkataba wake, ambapo kwa mwezi anatakiwa kuilipia Sh 600,000, kodi ambayo inatakiwa kulipwa kwa mwaka mzima.

“Mbuyu ni kama amechanganyikiwa, kama unakumbuka hivi karibuni aliibiwa mara mbili, lakini sasa hili la kodi limekuja tena, kibaya zaidi ni tishio la wenye nyumba kutaka kumtimua kama ataendelea kusumbua kwa malipo, sijajua nini kitaendelea hapa ni jambo la kusubiri,” kilisema chanzo.

Wakati huohuo, taarifa za uhakika zinaeleza kuwa mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu naye pia yupo kwenye hali kama hiyo kwa kuwa kodi ya nyumba anayoishi Mikocheni jijini, imemalizika na bado haijalipwa.

 Mbuyu alipotafutwa alionekana kushtushwa na taarifa hizo na kusema: “Umeambiwa na nani habari hizo? Tanzania hakuna siri, kweli nadaiwa kodi ya nyumba naomba ujue hivyo tu na tayari nimeshazungumza na viongozi wa klabu kulitatua hilo.”

Alipotafutwa Kavumbagu, hakupatikana mpaka tunaingia mitamboni lakini mmoja wa viongozi alithibitisha hilo na kusema uongozi unalifanyia kazi ndani ya siku chache litakuwa limekamilika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic