Na Saleh
Ally
Mshambuliaji nyota wa Simba, Amissi Tambwe amesema ameanza kuingia hofu kutokana na mabeki
kumpania lakini mbaya zaidi ni kumshambulia kwa kumpiga ngumi kila wanapopata
nafasi ya kufanya hivyo.
Tambwe raia
wa Burundi, ameliambia Championi Jumatatu kwamba amekuwa akishambuliwa kila
mara na mabeki wa timu mbalimbali kwa kupigwa ngumi za kichwani, tumboni na
mabeki wa Ruvu JKT walitia fora zaidi.
“Karibu
kila mechi nilicheza nimekuwa nikikumbana na hali hiyo, lazima nipigwe ngumi
mbili au tatu, matusi ndiyo usiseme, tena masimango ya ajabu. Wale wanajeshi
(Ruvu Shooting) wa jana (juzi), walinipiga ngumi nyingi zaidi, zinazidi tatu na
mmoja alinipa ngumi ya jicho, nikapata maumivu makali sana.
“Baada ya
mechi nililazimika kwenda kwa daktari naye akanifanyia uchunguzi na kusema
sikuumia sana, ila kulikuwa na uvimbe kidogo ambao leo umezidi kupungua,”
alisema mshambuliaji huyo aliyepiga mabao nane katika mechi sita.
Tambwe
alipoulizwa kama anahitaji ulinzi, alisema: “Ulinzi maalum si sahihi, lakini
sheria zifuatwe na waamuzi wanaweza kuliona hilo kwa kuwa wako zaidi ya mmoja
uwanjani. Soka si mchezo wa kuumizana kwa makusudi.
“Kila mtu
atumie mbinu kumpita au kumzuia mwenzake lakini kimichezo, kupigana ngumi na
wakati mwingine mateke kwa makusudi si kitu chema.
“Angalia,
mara kadhaa wachezaji wanawatukana kabisa waamuzi, lakini wanawaacha, huenda
wanahofia. Nafikiri hata wachezaji tunapaswa kuangalia Fair Play, si sahihi
kutoa lugha chafu kwa waamuzi.
“Kama akija
mwamuzi kutoka nje akapata nafasi ya kuchezesha ligi, basi ninaamini kutakuwa
na kadi nyingi sana kwa kuwa wachezaji wengi hawaheshimu waamuzi na wanacheza
kwa uadui, soka ni kazi, soka ni furaha.”
Tambwe
amekuwa gumzo kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao, wakati ligi ina mechi
saba kwa kila timu, yeye ameishapachika mabao nane kimiani.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment