Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa
amesema kuwa mechi dhidi ya Ashanti United inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na
kiwango kizuri cha wapinzani wao katika mechi mbili zilizopita.
Mkwasa amesema kuwa, Ashanti imekuwa
ikionyesha kiwango kizuri tofauti na mwanzo ilivyoanza katika Ligi Kuu Bara, ndiyo
maana ana hofu juu ya mechi dhidi ya timu hiyo, kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa
Chamazi.
“Ashanti kwa sasa ni timu nzuri sana yenye
uwezo na inaonyesha soka la ushindani, lazima tujipange ili kuhakikisha
tunapata matokeo mazuri. Maandalizi yetu yanaendelea vizuri na tupo tayari kwa
ajili ya mechi hiyo,” alisema Mkwasa.
Licha ya kuanza ligi kwa kuyumba, Ashanti
imefanikiwa kuibuka na ushindi katika mechi mbili za hivi karibuni, ambapo
inashika nafasi ya 10 baada ya kujikusanyia pointi nane katika mechi tisa.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Ashanti,
Nicholaus Kiondo, amesema wamelenga
kubeba pointi zote 12 za michezo minne iliyobaki ya mzunguko wa kwanza na
wataanza kampeni hiyo watakapoivaa Ruvu Shooting.
0 COMMENTS:
Post a Comment