BOBBY AKIWA MAZOEZINI, JANA JIJINI NAIROBI |
Na Saleh Ally, Nairobi
Bado inaonekana uongozi na hata
mashabiki wa Simba hawana furaha sana na mwenendo wa kikosi chao, ingawa wako
wanaamini mambo yanaweza kwenda sawa.
Mashabiki na wanachama wa Simba, huenda
wangefurahi kupata mkombozi wa kuwatoa hapo walipo, wengi wanaamini kocha
mwingine na hasa mahiri na ikiwezekana kutoka nje ya Tanzania anaweza kuwa
msaada mkubwa.
...SALEH ALLY NA BOBBY NYUMBANI KWAKE KATIKA ENEO LA HURLIGHAM JIJINI NAIROBI |
Uongozi wa Simba, bado haujafungua mdomo
wake rasmi kusema kwamba Kocha Abdallah kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri
Kiwhelo ‘Julio’ ambaye hahofii kutimuliwa, kwamba safari imewakuta.
Mechi ya juzi dhidi ya Ashanti United
ilikuwa inasubiriwa kama jibu sahihi la nini cha kufanya lakini kabla kukaibuka
taarifa za ujio wa kocha mpya, huyu ni Robert ‘Bobby’ Williamson, raia wa
Scotland.
Taarifa hizo kutoka katika gazeti ambalo
hutoka Jumamosi, liking’ara na picha kubwa kabisa mbele, lilieleza kuwa Mskochi
huyo ndiye kocha mpya wa Simba, ikiwa ni habari kubwa na tayari ikazua hofu kwa
makocha wa Simba na furaha kwa baadhi ya mashabiki, kwamba mkombozi
amepatikana.
Uchunguzi wa Salehjembe ulianza
kuonyesha hofu katika jambo hilo, kwani viongozi karibu wote wa Simba, walisema
wazi hawakuwa wamefanya mazungumzo na Williamson kuhusiana na suala la yeye
kujiunga Simba.
Vipi kuwe na taarifa kama hiyo bila hata
kuwa na uhakika, kwa kuwa Nairobi si mbali hasa kama wasomaji wanataka uhakika
wa jambo, Championi lilifunga safari hadi katika mji huo mkubwa zaidi nchini
Kenya kwa ajili ya kuzungumza naye, ana kwa ana ili kupata uhakika zaidi.
Williamson ambaye ni mshambuliaji wa
zamani wa Rangers ya Scotland ambaye Alex Ferguson pia aliwahi kuichezwa kama
mshambuliaji, anaonyesha kushangazwa na jambo hilo, huku akisisitiza hapendi
kuzushiwa mambo, badala yake hufurahia uhakika wa mambo.
Kocha huyo ambaye pia amewahi kuinoa Wes
Brom Albion ya England kati ya mwaka 1986-88, anasema amekuwa akifanya mambo
yake kwa kufuata utaratibu kwa kila kitu na sasa anaheshimu sana mkataba wake.
Kwani siku chache, Williamson ameiongoza
Gor Mahia anayoinoa sasa kutwaa ubingwa wa Kenya baada ya kuukosa kwa zaidi ya
miaka kumi.
Sifa yake kubwa katika ukanda wa Afrika
Mashariki ilianza kupanda baada ya kubadilisha soka la Uganda na kuibebesha
Kombe la Chalenji kwa miaka minne ambayo ni 2008, 2009, 2011, 2012.
Mahojiano kati ya Williamson na gazeti
hili, yalifanyika jijini hapa nyumbani kwake katika eneo la Hurringum, moja ya
maeneo yanayokaliwa na ‘wenye nazo’.
Salehjembe: Vipi Bobby, taarifa za wewe
kuwa ni kocha mpya Simba zimeshika kasi nchini Tanzania, labda lini unatarajia
kutua na umeishakubaliana nao kuhusiana na maslahi?
Bobby: Kuna mtu pia kanieleza kuhusu
hilo kutoka Tanzania, lakini nakuhakikishia sijawahi kuzungumza na kiongozi au
mtu yoyote wa Simba.
Salehjembe: Taarifa zinasema mmeanza
mazungumzo, au ni siri kubwa?
Bobby: Sidhani kama kuna siri katika
jambo kama hilo, kama Simba wangekuja, basi ningewaeleza wanonane na Gor
(Mahia) kwanza. Ninaheshimu mkataba wangu na nisingependa kuchanganya mambo.
Salehjembe: Mara nyingi watu wa mpira
mmekuwa mkificha mambo, utakataa leo, kesho tunasikia uko Simba.
Bobby: Kama watakuja Simba, basi labda
nisubiri, ikiwa hivyo nitakueleza mara moja. Lakini nakuhakikishia, sina
mazungumzo yote na Simba, ndiyo maana nasema sipendi mambo ya kuzushiwa.
Salehjembe: Kuzushiwa kivipi?
Bobby: Nimeelezwa kuwa imeripotiwa mimi
ni kocha mpya Simba, ni kitu ambacho sikijui kabisa. Wewe pia umeuliza kitu
hicho hicho. Mimi ni mtu mwenye ushirikiano, naweza kupatikana na ningezungumza
kama ninavyofanya hapa. Sipendi kabisa mambo ya kubahatisha, mimi ni kocha wa
Gor.
Salehjembe: Labda mkataba wako unaisha
lini na ikitokea timu ikakuhitaji, mfano Simba au nyingine yoyote, uko tayari
kuondoka?
Bobby: Mkataba unaisha mwakani, sina
shida katika suala la kuondoka, mimi ni kocha lakini ningependa utaratibu
ufuatwe na ndiyo maana nasisitiza uongozi wa Gor kupitia kwa mwenyekiti vizuri
ukahusishwa.
Salehjembe: Tukiachana na hilo ambalo
angalau sasa tuna uhakika, vipi kuhusiana na kipa Ivo Mapunda ambaye ni kati ya
vijana wako.
Bobby: Mapunda ni kati ya makipa bora
kabisa katika kikosi changu, anafanya kazi yake vizuri. Ni kipa wa pili lakini
amefanya kazi nzuri sana kila alipopewa nafasi.
Salehjembe: Unampa nafasi gani kutokana
na makipa uliowahi kuwafundisha kuanzia Uganda?
Bobby: Nafasi ya juu, kwa maana ya
kiwango na nidhamu. Lakini anajituma na ukuliza mashabiki watakuambia, anaipenda
kazi yake na wanampenda sana.
Salehjembe: Ulikuwa kocha wa
mshambuliaji Emmanuel Okwi, lakini mambo yake yamekuwa hayaendi vizuri pamoja
na wengi kuamini anaweza kucheza Ulaya. Unafikiri nini tatizo?
Bobby: Okwi ni kati ya wachezaji bora
kabisa katika ukanda huu, inawezekana pia namna ya kumuongoza au kujiunga na
timu ambayo hawakuendana. Lakini bado ana nafasi ingawa anatakiwa kufanya mambo
yake kwa mahesabu makubwa maana muda pia usonga mbele, kwa maana ya umri.
Salehjembe: Bobby, nashukuru sana kwa ushirikiano
wako?
Bobby: Karibu tena, umesema wewe ni
mwandishi chipukizi wa Salehjembe, vipi naona kama umri umeenda.
Salehjembe: (kicheko), kwaheri.
0 COMMENTS:
Post a Comment