November 8, 2013

...NIKIWA NA IVO MAPUNDA BAADA YA MAZOEZI YA GOR JANA KWENYE UWANJA WA CITY JIJINI NAIROBI, KENYA. (PICHA NA MARTIN NYAMORI)

Na Saleh Ally, Nairobi
KIPA Ivo Mapunda alionekana kupoteza umaarufu, taarifa kutoka kwa viongozi wa Yanga wakasema kiwango chake kimeporomoka, akaachwa.

Siku chache baadaye akaibukia African Lyon, katika mechi alizocheza kiwango chake kikaonyesha kuwa juu lakini kutofanya vizuri kwa timu hiyo, kukamponza aonekane hakuwa vizuri sana.

Baada ya hapo, Ivo akaamua kuachana na soka nyumbani Tanzania na kuonyesha anaamini uwezo wake na kwenda kufatuta timu nje ya Tanzania, alianzia Bandari ya Mombasa.

Pamoja na timu kutokuwa na umaarufu lakini kazi yake ilikubalika na Bandari ikawa moja ya timu gumzo huku Ivo akiwa mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri.

Kutokana na uwezo wa juu aliuonyesha, Ivo akachukuliwa na Gor Mahia, klabu kongwe iliyokuwa kwenye mikakati ya kuamka tena baada ya kuwa imepoteza mwelekeo kwa kipindi zaidi ya miaka 15.
Gor Mahia hawawezi kujuta kumchukua Ivo, kwani wiki iliyopita wametawazwa kuwa mabingwa wa Kenya, ubingwa walioukosa kwa zaidi ya miaka kumi.

Bado hilo halitoshi, Kocha Kim Poulsen naye amemuita katika kikosi cha Young Taifa Stars,  hii maana yake uwezo wake umekubalika tena nyumbani kwa mara nyingine.

Lakini tokea ametua Gor Mahia, misimu miwili iliyopita, Ivo hajawa kipa namba moja, nafasi hiyo anayo Jerim Onyango lakini Kocha Mkuu, Robert ‘Bobby’ Williamson anasema kipa huyo ndiye alisababisha Ivo apate namba.

“Kidogo unaweza kuona tofauti, lakini Onyango aliniambia Mapunda ana uwezo mkubwa sana. Hivyo ni vizuri kumpa nafasi acheze, nikamsikiliza na kweli hajawahi kutuangusha na mechi zote za makombe (ambazo si za ligi kuu) amekuwa akianza yeye na anafanya vizuri.

“Mfano, wiki ijayo tutacheza mechi ya Kombe la runinga ya SuperSport na Mapunda ndiye katufikisha hapo, ametoa penalti nyingi sana kila tulipotakiwa kuvuka kwa mikwaju,” anasema kocha huyo raia wa Scotland.

Kwa Ivo anasema maisha jijini hapa ni tofauti kabisa na ilivyo Dar es Salaam kwa kuwa heshima imekuwa juu kupita kiasi.

“Kweli, kipindi hiki ninapata sapoti kubwa sana kutoka kwa mashabiki wa Gor (Mahia). Kwangu ni dalili kwamba ninafanya kazi na nimekuwa nikiongeza juhudi kila kukicha kwa kuwa ninakubalika.

“Kila sehemu nikipita, naweza kusema ule umaarufu wa Dar es Salaam umehamia Nairobi. Najua, Dar es Salaam kuna watu wameishanisahau, lakini hapa ndiyo wameanza kunijua sasa,” anasema.

Kivutio kikubwa kwa Ivo jijini hapa ni kwamba ndiye kipa maarufu zaidi katika Ligi Kuu Kenya (KPL) anayeongiza kwa kuokoa mikwaju ya penalti.

Katika mechi kumi na ushee alizocheza ameokoa penalti nane na hii imefanya mashabiki wengi wajenge hisia kwamba uwezo wake huo huenda una nguvu ya ziada na hasa ile taulo ambayo huingia nayo uwanjani.

“Kweli taulo imekuwa maarufu sana, ikiwezekana hata kuliko mimi. Wakati unapocheza, si unajua unakuwa na taulo na unaweza kuamua kupunguza jasho kwa kujifuta.

“Ukifanya hivyo tu, watu wanaamini kwamba ni kitu cha ziada. Hivyo wamekuwa wakiizungumzia sana taulo hiyo na ni maaufu sana. Lakini ninachoweza kukuhakikishia hakuna ushirikina wala taulo ya Mapunda.

“Ninachofanya ni juhudi tu ya mazoezi, kweli ninajituma sana na ninataka kufanikiwa pia zaidi ya hapa nilipo,” anasema.

“Niko ugenini na ushindani ni mkubwa, najua ni changamoto na ndiyo maana nilikubali kuja hapa. Maana yake lazima nijitume na kufikia mafanikio maana hakuna njia ya mkato,” anasema.

“Hapa maisha pia yanaweza kuwa tofauti na nyumbani, lakini nimeamua kufanya kazi, ninajiamini lakini mambo hayawezi kuwa bora bila ya kujituma,” anasema.


Katika mitaa ya jijini la Nairobi hasa kwa wapenda soka, Ivo ni kati ya wachezaji maarufu zaidi wa kigeni wanaocheza soka katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu Kenya.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic