LUNYAMILA&MMACHINGA |
Na
Saleh Ally
Katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, ni nane tu yenye timu zinazoshiriki ligi kuu, mingi
ikiwa na timu zaidi ya moja.
Dar es
Salaam ina timu nne, Mbeya, Tanga na Pwani kila mmoja una timu mbili, wakati
mikoa ya Tabora, Arusha, Morogoro na Kagera ina timu moja moja.
Ajabu,
kuna baadhi ya mikoa inayosifika kwa kutoa vipaji vya soka au iliwahi kuwa na
timu tishio katika miaka ya 1980, 1990 na 2000 mwanzoni lakini sasa haina kitu.
Hali
hiyo huenda inatokana na matatizo ya ubinafsi wa watu, kutojituma na
ikiwezekana viongozi kutokuwa wabunifu au kukosa mapenzi ya dhati na mchezo
huo. Fuatilia mikoa hii.
Mwanza:
Mwanza
ilipewa jina la Brazil ya Tanzania na hiyo ilitokana na rundo la vipaji ndani
ya mkoa huo ambao umewahi kutikisa vilivyo na Klabu ya Pamba au TP Lindanda.
Baada ya hapo stori ikawa ni Toto African.
Lakini
ajabu Wanamwanza wenyewe wakaongoza kujipiga vita, sasa wameingia katika mikoa
isiyokuwa na timu Ligi Kuu Bara, hiki ni kichekesho.
Aibu
kubwa kwa Mwanza kutokuwa na timu wakati imezalisha wachezaji kibao mahiri kama
akina Ibrahim Magongo, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Deo Mkuki, Fumo Felician,
Salum Kabunda ‘Ninja’, Khalfan Ngassa, Hussein Masha, Kelvin Yondani, Mrisho
Ngassa, Oscar Joshua na Jerry Tegete.
Inawezekana
baadhi ya wachezaji hao asili yao si Mwanza, lakini wamejifunzia soka mkoani
humo na kuanza kutamba wakiwa huko na timu za huko.
Vipi
leo hata timu moja hakuna na hata ukiangalia wakati wa Toto African, kila msimu
ilikuwa ikipigana kuepuka kushuka daraja? Hakuna ubishi ni majungu na chuki
ndivyo vimechukua nafasi kubwa ya vipaji vya soka mkoani humo.
Dodoma:
Ilikuwa
na timu mbili zenye upinzani mkubwa kama Kurugenzi na CDA. Karibu kila timu
iliyokuwa inatua mjini humo, ilijua kazi ya timu hizo.
Ingawa
Kurugenzi iliendelea kubaki daraja la kwanza kwa kipindi kirefu lakini
ilizalisha wachezaji wengi waliocheza katika timu za juu.
Kati ya
wachezaji wake nyota ni Iddi Athumani ‘Pajero’, baba mzazi wa beki wa Yanga,
Athumani Iddi ‘Chuji’ ambaye pia alichipukia mkoani hapo akicheza katika timu
ya Polisi Dodoma.
Sasa
hakuna timu ya ligi kuu, lakini karibu kila kitu kuhusiana na soka kimedorora,
Dodoma umekuwa mji wa bunge tu, dalili zinazoonyesha wananchi wake kama hawana
habari tena na mpira au wanaupenda lakini chama chao cha soka kimelala usingizi
wa pono.
Ruvuma:
Achana
na uimara wa Majimaji tu enzi hizo, lakini angalia wachezaji kibao
waliozalishwa kutoka katika mkoa huo bila ya kujali ni wenyeji wa wapi.
Wengi
watamkumbuka Steven Mapunda ‘Garincha’ lakini kulikuwa na rundo la wachezaji
kama Peter Mhina, Amri Ayoub ‘Beki Mstaarabu’, Celestine Sikinde Mbunga na kaka
yake, Emmanuel Mbunga, Isihaka Majaliwa, Mohammed Mkandinga, kiungo wa ukweli
Octavian Mrope ‘Oko’ na wengine wengi.
Ruvuma
ni kati ya mikoa michache ambayo imewahi kutoa bingwa katika Ligi Kuu ya
Muungano, kazi hiyo ilifanywa na Majimaji.
Lakini
leo haina timu Ligi Kuu Bara na hata kama Majimaji ikipanda imekuwa ikisuasua
na mambo mengi ni ya kubahatisha. Hakuna viongozi wenye uchungu? Au hakuna
kiongozi mwenye mipango kama ile ya Lawrence Gama wakati wa enzi zake? Hii ni
aibu!
Tabora:
Kwa
Tabora, sifa ya Milambo inajulikana, ni mkoa wa soka hasa. Kweli sasa kuna timu
ya ligi kuu ya Rhino, lakini hadi kwa msaada wa jeshi ndiyo timu imepatikana.
Kumbuka enzi za Milambo au timu imara ya mkoa ya Mashujaa wa Unyanyembe.
Huenda
kwa nguvu ya wananchi kama wanapenda soka, basi timu ya jeshi isingekuwa ya
pili kwao kushiriki ligi kuu. Tabora ni kati ya mikoa inayoongoza kwa vipaji
vya soka, angalia wachezaji hawa wa enzi hizo na baadhi wanaoendelea kucheza.
Quresh
Ufunguo, Ally Manyanya, Mikidadi Jumanne, Idd ‘Mnyamwezi’, Mrisho, Ally na
Haruna Moshi ‘Boban’, Ahmed Mwinyimkuu, Said Mwamba ‘Kizota’, Athumani Shabani
‘Tippo’, Abubakari Kanyoro, Seif Juma, Ramadhani Hamis ‘Mvulana’, Mohammed
Banka na wengine kibao.
Shinyanga:
Anzia
timu ya Mwadui, timu iliyokuwa inamiliki ndege na ndiyo pekee Tanzania kuwahi
kufanya hivyo. Baadaye RTC Shinyanga kabla ya kuitwa Biashara na baadaye
Shinyanga Shooting.
Shinyanga
ilikuwa na wachezaji kadhaa mahiri kama Michael Paul ‘Nylon’ ambaye baadaye
alitikisa Simba, Paul John Masanja aliyetua Yanga na kuongoza ukuta mgumu na
Mwinyimvua Komba ‘Masolwa’ aliyegoma mara kibao kujiunga na timu hizo kongwe
akisisitiza anataka kubaki kwao.
Wapo
wengine wengi kama Abdallah Magubika aliyetua Yanga baadaye, Alfred Kategile
‘Kate’ aliyekwenda Simba na Steven Nyenge ambaye pia aliwahi kuichezea Simba.
Bado
kuna Nteze John Lungu aliyetokea Kigoma kama ilivyo kwa Edibily Lunyamila,
lakini wakasoma na kukulia Shinyanga huku vipaji vyao vikianza kuonekana ndani
ya mji huo.
Nteze hakuwahi
kucheza ligi kuu akiwa Shinyanga, badala yake alisomeshwa na soka, kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha sita alilipiwa karo na timu ya Halmashauri ya Mji
iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza, baada ya kumaliza shule, akatua
Pamba. Lunyamila akaenda zake Yanga.
Angalia
sasa, ligi kuu imekuwa ndoto kwa zaidi ya miaka kumi huku viongozi wakiendelea
kuwa asilimia kubwa ni walewale na maneno kibao, vitendo hakuna.
Kigoma:
Kwa
mkoa huu ni aibu nyingine kusema hauna timu ya ligi kuu, ndiyo unaotikisa kwa
vipaji katika mchezo wa soka. Wengi wanalazimika kutoka na kwenda kucheza nje
ya mkoa kwa kuwa viongozi wa chama cha soka na wale wa klabu ni watu wa maneno
tu.
Achana
na asili, kama utasema wachezaji wa soka waliotokea Kigoma, basi inaweza kuwa
asilimia 35 ya wote wanaocheza soka nchini.
Wachache
ni hawa hapa ambao ni Said Sued ‘Scud’, Juma Kaseja, Selemani Matola, Said
Maulid ‘SMG’, Alphonce Modest, Hemed Ally ‘Matobango’, Beya Simba, Hamza
Maneno, Nassor Idd ‘Cheche’, Athumani Bilal ‘Bilo’, Dadi Fares, Mavumbi Omary,
Abeid Mziba, Makumbi Juma ‘Bongabonga’ (nimechoka kutaja).
Kwa
kifupi wapo wengi sana, lakini baada ya Reli na RTC Kigoma ikafuatia Mmbanga,
baada ya hapo ni majanga na hadithi ya mkoa wenye vipaji imebaki palepale na
ligi kuu wanaendelea kuisikia kwenye bomba au kuiangalia kwenye ‘kideo’.
Mtwara:
Moja ya
mikoa yenye vipaji vya juu sana katika soka ni Mtwara, hilo halina ubishi.
Lakini ndiyo mkoa ambao umedorora kupita kiasi kisoka.
Pamoja
na umaarufu wa kulima korosho lakini wenyeji wake wanapenda sana soka, bahati
mbaya hamasa yao inaangushwa na viongozi wao ambao haijulikani wanafanya kitu
gani.
Wachezaji
kama mshambuliaji Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyeng’ara Yanga, Simba na
Taifa Stars au mshambuliaji mwingine hatari, Idefonce Amlima, wote ni mali ya
Mtwara.
Kwa
vijana wapo wengine, mfano Nizar Khalfan ni kati ya Watanzania wachache
waliocheza ligi kubwa za soka duniani. Kacheza Kuwait lakini akapaa hadi
Marekani, mdogo wake Razak Khalfan pia ni jibu kwamba Mtwara kuna vipaji.
Ajabu,
tangu Bandari Mtwara ilipotelemka daraja mwishoni mwa miaka ya 1990 na kutamba
kidogo baadaye mwanzoni mwa miaka ya 2000, hadi sasa ‘kwishney’.
Mara:
Huenda
kuna wengi hawakukulia mjini Musoma au katika sehemu mbalimbali za Mkoa wa
Mara, lakini hakuna anayeweza kusema Mkoa wa Mara hauna vipaji vya soka.
Mshambuliaji
wa zamani wa Pamba na Simba, Bhita John Musiba, kiungo mahiri enzi hizo kama
Nico Bambaga, aliyekipiga Pamba, Simba, Yanga na Malinzi ya Zanzibar, wote
asili yao ni mkoani humo.
Wengine
ni Athumani Jumapili ‘Chama’, Ramadhani Magoye, Dhikiri Mchumila, Mussa Janja
na Leonald Juma. Wapo wengi sana ambao wametokea Mara na walikuwa wachezaji
nyota, lakini hakuna kitu kabisa na mara nyingi timu za mkoa huo zimekuwa
zikipambana na kuishia daraja la kwanza.
Hadi
sasa, Ligi Kuu Bara ni kama Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Mkoa wa Mara, hakuna
timu yenye ndoto ya kugusa katika hatua hiyo, viongozi wa soka wapo, maisha
yanaendelea.
Kilimanjaro:
Unaikumbuka
Ushirika ya Moshi? Ni moja ya timu zilizokuwa zinacheza soka la ‘Kizungu’
utafikiri zinavyocheza sasa baadhi ya timu kubwa barani Ulaya.
Simba,
Yanga na timu nyingine kubwa zilikuwa zikihaha zinapokutana na Ushirika bila
kujali ni kwao Moshi au nje ya hapo. Jamaa walikuwa wanapiga soka tu, tena la
uhakika.
Wachezaji
kama Wema Juma, Abuu Juma, Willy Martin au kipa Ofen Martin ni kati ya vizazi
vya mwanzo vya Ushirika, lakini sasa mchezo wa soka unaonekana hauna nafasi
tena mkoani humo.
Sifa ya
Kilimanjaro ni biashara, soka ni biashara pia, huenda viongozi wa soka mkoani
humo hawalijui hilo na wamesahau kazi nzuri ya Ushirika enzi hizo.
0 COMMENTS:
Post a Comment