Na
Saleh Ally
Kuna mambo mengi sana yanatokea ndani ya Klabu ya Simba, ukijaribu kuyazungumza,
basi wahusika wanatafuta ‘huruma’ kwa kusema wanasakamwa huku wakitolea mifano
laini kwamba mbona wengine wameachwa!
Kitu
kizuri ni hivi; ni mara chache kuwakuta wakisema kilichozungumzwa ni uongo,
badala yake husisitiza aliyewakosoa ametumika au amesahau kuwakosoa wengine.
Wanakuwa si wanaochambua hoja husika, badala yake wanaivisha masikio iliyopo
ili kujali ambayo hayahusiki wakati husika.
Moja ya
vitu vya ajabu kabisa vinavyotokea Simba katika kipindi hiki ni ile tabia ya
benchi la ufundi kwamba mchezaji hata akishindwa kucheza vizuri katika mechi
moja tu, anaingia kwenye lawama kubwa na kushushwa katika kikosi cha kwanza.
Hii ni ajabu.
Mimi si
kocha, lakini kweli inawezekana vipi mchezaji anaposhindwa kucheza mechi moja
tu anashushwa kikosi B na hakuna msamaha hali ambayo inajenga hali ya visasi
vya wazi?
Kocha
Mkuu, Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ndiyo makocha
wazalendo ambao tuliamini wangeweza kuwa mfano, lakini mambo yamekuwa tofauti,
lawama na tofauti ndiyo yamekuwa mazungumzo yao.
Simba
haiwezi kupoteza mchezo bila ya kuwa na mchawi anayeangushiwa mzigo. Kila mechi
utasikia hujuma, mchezaji anashushwa timu B lakini ukiangalia kiuchezaji, Simba
inahaha katika mechi kadhaa kutokana na kukosa wachezaji wazoefu.
Hii
inazua hofu huenda wachezaji wakongwe wanaonekana ni kama sumu katika kikosi
cha Simba, jiulize nini hasa tatizo?
Inawezekana kuna tatizo la woga kwamba
kama kuna kitu kinakosewa wanaweza kuhoji, hivyo kusababisha waonekane ni adui.
Wachezaji
walioadhibiwa ni Henry Joseph, Abdulhalim Humud, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na
Haruna Chanongo ambaye ni chipukizi pekee.
Kila
mmoja ameshushwa timu B ambayo sasa inataka kuonekana kama ni gereza la waovu
wa timu ya kwanza, kwani anayeharibu anashushwa huko. Kawaida jukumu la timu
hiyo ni kujenga na kuwapeleka juu na si kupokea rundo la wachezaji kutoka timu
kubwa, eti kisa wamecheza chini ya kiwango kwa dakika 45 tu!
Walio
timu B wanaweza kujengewa hisia kwamba, waliko wenyewe ni ‘gereza’ la wakosaji
wa timu ya kwanza, lakini wanaoshushwa pia wanaingiwa na hofu na kuona
wanadhalilishwa huku benchi la ufundi la Simba likiwasahau kabisa kwa kuwa
adhabu yenyewe haina fomula.
Anayekosea
hupewa nafasi ya kujirekebisha, hilo halijafanyika. Lakini kabla ya kufanya
hivyo, jambo la msingi ni kuzungumza na mkosaji na kikubwa ni walimu kuangalia
maslahi ya timu kwanza na si wao binafsi.
Simaanishi
Simba ichukue kocha Mzungu, lakini nakukumbusha wakati fulani marehemu Patrick
Mutesa Mafisango alilewa na kumtukana matusi ya nguoni Kocha Milovan Cirkovic
siku chache kabla Simba haijaondoka kwenda nje ya nchi kucheza mechi muhimu ya
Ligi ya Mabingwa.
Milovan,
raia wa Serbia, akasema amemsamehe na kumuunganisha kwenye kikosi, akacheza na
kuwa msaada mkubwa. Safari ya pili, baadhi ya viongozi wa Simba walishinikiza
Haruna Moshi ‘Boban’ apewe adhabu eti alimdharau kiongozi mmoja.
Milovan
akasisitiza kiongozi aliyezozana na mchezaji hakuwa wa kuchaguliwa, hivyo
akataka kuwe na tofauti na umakini katika utoaji adhabu. Hasira za watoa misaada
hao zikachangia Milovan kuondolewa kwa madai anashirikiana na wachezaji
watukutu.
Kadhalika,
baada ya kuondoka kwa kipa Juma Kaseja, utaona mambo yanavyowabana wakongwe
wengine ambao sasa wameingizwa tayari kwenye mlango wa kutokea, kilichobaki ni
kuufungua tu.
Henry:
Kosa
lake lilikuwa ni kwenda kupumzika, lakini baada ya kuwasiliana na Julio.
Kibadeni akakasirika na kumuondoa katika kambi, leo ni zaidi ya mechi ya tatu
Simba imecheza, hajarudishwa.
Taarifa
zinaeleza atarudi kucheza mechi ‘siriaz’ kwenye mzunguko wa pili. Jiulize Simba
ilimsajili wa nini? Maana yake anaendelea kula mshahara na hatakuwa katika
mpira wa ushindani kwa muda mrefu, tatizo ni hilo.
Angalia
namna benchi la ufundi la Simba lilivyoshughulikia suala hilo, tafakari utaona
kilichopo.
Redondo:
Ramadhani
Chombo ‘Redondo’ ni kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa kisoka, tumekuwa
tukielezwa ameshushwa kutokana na matatizo yake mengi, lakini kumbuka kipindi
cha Patrick Phiri na Milovan Cirkovic alicheza tena vizuri tu.
Msimu
huu tangu umeanza eti yupo kikosi cha pili tu kwa kuwa alikosea, lakini jiulize
kwa kikosi cha Simba kilichopo sasa, kweli hahitajiki?
Ataendelea
kubaki kikosi cha pili hadi lini na mwisho wake utakuwa upi na kweli benchi la
ufundi halimhitaji? Ukweli ni kwamba anaendelea kudidimia na miaka inasonga.
Humud:
Mkongwe
mwingine, huyu alikumbana na rungu la kuteremshwa katika timu ya pili eti kwa
kuwa alicheza vibaya dhidi ya Yanga. Alipotolewa, vijana walioingia
wakafanikiwa kuongeza nguvu na Simba ikasawazisha.
Tangu
wakati huo, akabaki kikosi cha pili, hakuna maelezo zaidi lakini ukweli ni
dakika 45 tu ndizo zimemuondoa kikosini. Jiulize akirudi atacheza vizuri au
ndiyo kummaliza kabisa?
Chanongo:
Hapa
kuna hatari zaidi, Chanongo alionyesha uwezo mkubwa msimu uliopita akitokea
timu B hadi timu ya wakubwa na sasa ni tegemeo. Lakini amerudishwa kikosi cha
pili na kesi yake ndiyo ileile ya Humud.
Huyu si
mkongwe, lakini unapomrudisha kikosi B kwa kucheza chini ya kiwango ndani ya
dakika 45 katika mechi moja tu, unamfanya aendelee kuporomoka.
Angalia
umri wa Chanongo, uzoefu wake katika soka na ukubwa wa mechi ya Simba na Yanga.
Lakini hebu angalia kama kweli kuna waliotuma shutuma kwake kwamba amehujumu,
vipi hadi leo hawajatoa ushahidi? Ukimya wao unamaanisha hawana uhakika, hapa
kuna mambo mawili tu yanaweza kufanyika, wamuachie aendelee na kazi au
wawasilishe ushahidi ashughulikiwe.
Wewe ni mchawi wa Simba!! Mbona huisemi vibaya YANGA. Makala zako zimejaa majungu na lengo ni kutaka kudhoofisha SIMBA!!!!
ReplyDeletewewe ulie comment, nadhani hujitambui,..sidhani kama ww ni mpenzi au mshabiki wa samba,sidhani kama yanga inahusika hapa issue ni simba ,..kiukweli hata mie namuunga mkono mwandishi wa makala hii, jullio,kibaden na mashabiki wababaishaji kama ww ndo mnao iharibu simba kwa kuwa hamtaki kuuona ukweli mkasoma alama za nyakati.
Delete