November 27, 2013




Na Saleh Ally
Wakongwe wa soka nchini, Yanga na Simba, ndiyo timu gumzo kuliko nyingine zote nchini na zinaingia katika kila linalozungumziwa kwenye mchezo huo nchini.
 
Yanga na Simba ndizo zinachangia kwa kiasi kikubwa mchezo wa soka nchini, lakini ndizo zinazohusika katika lawama ya kuporomoka kwa mchezo huo.
Kama utasikia suala la kuharibika kwa mambo katika mchezo wa soka, basi Simba na Yanga hawawezi kukosekana na yote hayo yanatokana na mambo mawili makubwa.

Kwanza ni wivu wa kawaida ya timu hizo kutaka kuwa juu siku zote hata kama hazijitumi, ndiyo maana Yanga au Simba itaona bora ubingwa uchukuliwe na mmoja wao kuliko timu nyingine.

Pili ni mapenzi binafsi, maana hata viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wale wa serikali, wapo katika makundi mawili kama mashabiki wa kawaida.

Simba na Yanga haziwezi kukwepa hilo, lakini ukirudi katika suala la maendeleo, si sahihi kuziacha na lawama ziwe kama mafuriko kwao, badala yake wakati mwingine zinastahili pongezi.
Maendeleo:
Maendeleo ya karibu asilimia 90 yamepatikana kupitia timu hizo, utaona zikiwa uwanjani zinasukuma ‘gozi la ng’ombe’ lakini ukweli zenyewe ndiyo wafalme wa mengi mazuri yanayopatikana.

Mfano, mapato kila zinapocheza yanapatikana kwa wingi zaidi kuliko inapocheza timu nyingine yoyote.
Yanga na Simba, kila moja imecheza mechi 13 za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, hakuna hata timu moja imefikia nusu ya kila kilichofanyika kwao kwa maana ya faida.

Kama utazungumzia mapato, idadi ya watu zilizoingiza uwanjani, utaona hakuna hata timu iliyofanikiwa kunusa nusu ya zilivyofanikiwa, hii ni sehemu ya kuonyesha ubora wao, hata kama kuna sehemu zinaharibu.

Mapato:
Yanga ndiyo imeongoza kwa mashabiki na kiwango cha mapato, Sh milioni 334.2 katika mechi zote 13, Simba Sh milioni 304 na Mbeya City ikashika nafasi ya tatu na Sh milioni 83.8.

Mapato hayo ni baada ya makato yote, lakini kabla ya makato makubwa, Yanga na Simba, kila moja imeingiza zaidi ya Sh bilioni moja katika mechi hizo 13. 

Angalia Mbeya City iliyoshika nafasi ya tatu kwa mapato, imeshindwa kuingiza hata nusu ya fedha ambazo wameingiza Yanga na Simba (kila moja). Huu ni mfano mzuri kwamba timu hizo zinachukua mapenzi ya wapenda soka wengi.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ndiyo umeongoza kwa kuingiza mapato makubwa zaidi, Sh bilioni 1.8 si mchezo na hii ni kwa kuwa unatumiwa na timu hizo kongwe.

Uwanja wa Sokoine, Mbeya unaotumiwa na timu za Prisons na Mbeya City umeibuka na kushika nafasi ya pili kwa kuingiza Sh milioni 260.5. Hii ni robo tu ya mapato ya Taifa.

Mbeya wamejitahidi na hayo ni mabadiliko ya kuwepo Mbeya City, lakini hakuna ubishi tena kuwa Yanga na Simba ndizo zinazoendesha mapato ya soka nchini.

Mashabiki:
Katika mechi ambazo Yanga au Simba wamekuwa wenyeji au wanacheza, ndizo mashabiki walizojitokeza kwa wingi kuliko timu nyingine na huu ni uthibitisho wa mvuto wao kwa mashabiki.
Yanga imeonyesha kuwa na mvuto zaidi kwa kufuatwa na mashabiki 107,890, Simba inafuatia kwa mashabiki 97,364, Mbeya City  43,439 na Azam FC 30,236.

Hapa bado heshima kwa timu hizo kwamba ndizo zenye mvuto zaidi kwa mashabiki nchini, pia takwimu hizo zinamaliza ubishi kuwa Yanga ndiyo yenye mvuto zaidi kwa maana ya mashabiki.

 Yanga na Simba ndiyo chachu ya mafanikio ya soka nchini, huenda zinageuka kuwa sumu kutokana na mfumo wa wanaoziendesha na hasa viongozi. Lakini zikitumika vizuri, basi zinaweza kuwa changamoto ya maendeleo maradufu.

 Angalia namna zilivyotesa kwenye mapato na wingi wa mashabiki huku kukiwa hakuna timu iliyosogea na kunusa hata nusu yao.


MAPATO KWA TIMU
Yanga imekusanya Sh 334.2m
Simba imekusanya Sh 304m
Mbeya City imekusanya Sh 83.8m
Azam FC Sh 67.1m
Coastal Union Sh 65.7m
Mtibwa Sugar Sh 49.9m
Ruvu Shooting Sh 46.1m
Tanzania Prisons Sh 38.1m
JKT Ruvu Sh 36.1m
Ashanti United Sh 35.7m
Rhino Rangers 31.1m
Mgambo JKT Sh 25.8m
Oljoro JKT Sh 20.8m
Kagera Sugar Sh 18.5m

IDADI YA MASHABIKI:
Yanga-107,890
Simba- 97,364
Mbeya City- 43,439
Azam FC-30,236
Coastal-27,880
Mtibwa-Sugar 20,794
Rhino Rangers -20,263
Prisons-19,923
Ruvu Shooting -19,000
JKT Ruvu-16,095
Ashanti-16,093
Mgambo-11,726
JKT Oljoro-10,430

FEDHA AMBAZO VIWANJA ZIMEINGIZA…
Uwanja wa Taifa (Dar) Sh bilioni 1.8
Sokoine (Mbeya) Sh milioni 260.5
Mkwakwani (Tanga) Sh milioni 105.3
Ali Hassan Mwinyi (Tabora) Sh milioni 100.2
Sheikh Amri Abeid (Arusha) 57.4
Azam Complex (Dar) Sh milioni 32.1
Kaitaba (Bukoba) Sh milioni 26.1
Manungu (Turiani) Sh milioni 9.4
Mabatini (Mlandizi) Sh milioni 3.9





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic