Na Saleh
Ally
Mbeya City
ndiyo imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini baada ya mechi 13 za mzunguko wa
kwanza, utafikiri ilipanda daraja misimu mitatu iliyopita.
Kuna mambo
mengi muhimu ambayo yameonekana kupitia Mbeya City na inawezekana kabisa wadau
wa timu nyingine wakikubali watajifunza.
Pamoja na
ugeni wake, Mbeya City imeonyesha mambo kadhaa ambayo ni nadra kufanywa na timu
iliyopanda msimu kwa mara ya kwanza.
Ndani ya
mechi 13 pekee, Mbeya City imefanya mapinduzi makubwa ambayo yanaweza kuwa
funzo kwa timu nyingine.
Wananchi:
Mbeya City
imeonyesha ni timu ya wananchi kweli kwa kuwa imefanikiwa kushika nafasi ya
tatu katika timu zilizoingiza mashabiki wengi baada ya Yanga na Simba.
Katika
mechi 13 ilizocheza, Mbeya City imeingiza mashabiki 43,439 na kuzipiku timu
kibao ikiwemo Azam FC iliyoshika nafasi ya nne kwa kuingiza mashabiki 30,236.
Azam FC ni
maarufu maradufu zaidi ya Mbeya City, lakini wingi kwa wa mashabiki wa timu
hiyo, imeshika nafasi ya juu.
Unaweza kusema
watu wa Mbeya walikuwa na hamu ya kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara. Kwao si
kitu kigeni kwa kuwa walikuwa na Prisons. Hii inaonyesha kiasi gani timu
zinazoungwa mkono na mashabiki zinavyokuwa na nguvu.
Mapato:
Katika
suala la mapato, ni sawa na kusema kuwa ni kitu cha kushangaza kwa kuwa Mbeya
City pia imeshika nafasi ya tatu baada ya Yanga na Simba.
Yanga imeongoza
kwa mapato, katika mechi 13 inafuatiwa na Simba ambazo zimeingiza zaidi ya Sh
bilioni kwa kila moja.
Mbeya City
pia imejitutumua kwa kuwa katika mechi 13 ilizocheza Mbeya na kwenye viwanja
vingine, imeingiza Sh milioni 360.7. Maana yake ndiyo timu inayopendwa zaidi
sasa kwenye ligi hiyo baada ya Yanga na Simba.
Sokoine &
ugenini:
Mbeya City
inakubalika zaidi kwao Mbeya, hilo halina ubishi na takwimu zinaonyesha katika
Sh milioni 360.7, Sh milioni 201 zimepatikana kwenye Uwanja wa Sokoine ambao
ndiyo wa nyumbani.
Pia imeusaidia
uwanja huo kurudisha umaarufu wake kama enzi za Tukuyu au Mecco, maana umekuwa
wa pili kwa kuingiza fedha na mashabiki wengi baada ya Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Lakini bado
imekuwa timu iliyofanya vizuri kwa kuingiza fedha nyingi ugenini ukiacha Simba
na Yanga. Katika mechi hizo nje ya Sokoine, imeingiza Sh milioni 159.5.
Kichekesho:
Kichekesho
kiko katika makato, kwamba pamoja na Mbeya City kuonyesha mapinduzi makubwa
katika soka ikiwa ndiyo imeshiriki ligi nusu msimu tu na kuingiza Sh milioni
360.7, imejikuta ikiambulia fedha kiduchu sana.
Katika
mechi hizo 13, Mbeya City imeambulia kama Sh milioni 83.8 tu huku ikiacha zaidi
ya Sh milioni 150 zikiingia kwenye migawo mingine. Kugawa kwa timu pinzani ni
sahihi, lakini makato yamekuwa mengi sana.
Inaonekana
ni kama kichekesho kwa kuwa timu kama Mbeya City au hata nyingine zimejitahidi
kuingiza fedha nyingi, lakini nyingi zinaangukia katika mengine ambayo hata
hayana msingi.
Katika
mechi mbili dhidi ya Yanga na Simba, kabla ya makato, Mbeya City iliingiza Sh
milioni 223, hii inaonyesha mechi zake dhidi ya watani hao zinafuatiliwa na
ziliingiza zaidi ya asilimia 75 ya fedha zilizopatikana katika mapato ya timu
hiyo.
Huenda hilo
likaangaliwa na kuchukuliwa hatua ili kuendelea kuzipa nguvu timu zinazoibuka
na kuleta changamoto katika mpira wa Tanzania kama ilivyo kwa Mbeya City.
Lazima
katika suala la makato kuwe na kipaumbele kwa timu kwanza, vitu vingine
vifuatie huku vikijua kuzipa timu nguvu, hii itasaidia mapato kuendelea
kupatikana kwa muda mrefu zaidi kuliko kuzikata kupindukia.
0 COMMENTS:
Post a Comment