Naanza na kukumbushia ile ishu ya mashabiki wa Yanga kung’oa viti katika mechi dhidi
ya Coastal Union ikiwa ni baada ya mwamuzi Martin Saanya kutoa penalti na
nahodha Jerry Santo akaukwamisha mpira wavuni.
Bao la
Santo, raia wa Kenya, lilisababisha matokeo yawe 1-1, wakati mashabiki wa Yanga
na asilimia 95 ya waliokuwa uwanjani, walikuwa wanaamini matokeo ni ushindi wa
bao moja kwa mabingwa, Yanga.
Vurugu
zikazuka, viti vikang’olewa na Jeshi la Polisi Tanzania likalazimika kutumia
nguvu za ziada kuhakikisha hali ya usalama inarejea uwanjani hapo, hali hiyo
imejirudia tena Simba ilipocheza na Kagera Sugar.
Mechi
imemalizika kwa sare ya bao 1-1, Kagera wakisawazisha katika dakika za
nyongeza, mfungaji wa bao akiwa ni Salum Kanoni. Bao lilitokana na mshambuliaji
wa Kagera kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Baada
ya hapo, mashabiki wa Simba wakakurupuka na kuanza kufanya vurugu kubwa
iliyosababisha baadhi yao kuumia na kukimbizwa katika hospitali ya Temeke kwa
ajili ya kupata matibabu.
Achana
na hivyo, hiki ndicho kinachoshangaza zaidi na ninaweza angalau kulifananisha
tukio hilo na lile la mashabiki wa Yanga katika mechi dhidi ya Coastal, viti
vikang’olewa na safari hii vingi kwa kuwa tumeelezwa ni zaidi ya 50.
Hiki ni
kitu kibaya zaidi ambacho kinapaswa kukemewa bila ya woga na waliofanya
wanapaswa kutafakari mambo mengi sana ya msingi ili angalau wajutie upuuzi
walioufanya.
Uwanja
wanaouharibu ndiyo pekee bora katika viwanja nchini, lakini inakuwaje wachukue
uamuzi wa kipuuzi kama huo kwa kuwa eti mwamuzi ameharibu na kuwavuruga wao?
Viti na mwamuzi vinahusiana vipi?
Viti
havihusiki na mpira unaochezwa, havihusiani kabisa na kipenga kinachopulizwa na
mwamuzi. Sasa kwa nini mwenye hasira akimbilie kung’oa viti huku akijua wazi
uharibifu wake ni hasara kwa taifa letu na si mwamuzi au TFF kama ambao ndiyo
wamemuudhi?
Labda
mnakuwa wasahaulifu na wakati mwingine hamhitaji kujikumbusha masuala ya msingi
kabla ya kuchukua uamuzi kama ambao mmekuwa mkifanya kwa kuwa mnatumia nafasi
ya wingi wa watu ili kujificha na kuepuka kukamatwa.
Lakini
ukweli ninawakumbusha kuwa, pamoja na ukongwe wa klabu zenu ambazo zimeanzishwa
katika miaka ya 1930, hadi sasa hakuna iliyothubutu kuweka hata nusu ya kiti
cha plastiki ikasema ni maandalizi ya kujenga uwanja.
Tunajua
Yanga na Simba wote wameshatuonyesha ramani ya viwanja vyao na hakuna hata
kimoja ambacho kimeanza kujengwa, badala yake ni kwamba, ujenzi huo unaonekana
kubaki kwenye makaratasi.
Kama
klabu zenu ambazo mnaamini ni kubwa na lazima zishinde kila mechi hazina hata
harufu ya kumiliki viwanja, vipi mfikie kubomoa viwanja ambavyo vimejengwa kwa
nguvu ya wananchi wote wa Tanzania?
Tanzania
imepata msaada kuujenga uwanja wake, lakini nusu fedha zimetolewa na serikali,
inakuwaje mfanye uharibifu kwa sababu ambayo haihusiani na uwanja? Au ndiyo
tabia za kipuuzi za kuiga mambo ya Ulaya, eti kwa kuwa mashabiki wakikasirika
wanavunja viti, basi Wabongo nao lazima muige! Huo ni utumwa wa mawazo.
Tunakwenda
mbele kwa kutaka kupambana ili kufanya tuende na dunia ya sasa katika suala la
maendeleo. Lakini mnaturudisha nyuma au mnataka tuwe na viwanja ambavyo watu
wakiingia kushuhudia mechi wanakaa kwenye mikeka?
Badilikeni,
hasira za dakika mbili hazina sababu ya kusababisha uharibifu na kingine mjenge
tabia ya kuziachia mamlaka husika kushughulikia matatizo yanayotokea, ndiyo
maana kuna waamuzi wanafungiwa na kadhalika.
Tunahitaji
kwenda mbele, ukarabati wa Uwanja wa Taifa kila kukicha hautatusaidia kwenda
mbele. Badala yake tunatakiwa kuwa watu tunaofikiri wakati mwingine kabla ya
kutenda, vizuri kutafakari faida na hasara. Jiulize kama kuna usahihi wa kuvuka
barabara ukiwa umefumba macho!
0 COMMENTS:
Post a Comment