Na Saleh
Ally
UNAWEZA
kuona kama ni miujiza lakini hali halisi inaonyesha kuwa, mambo mengi
yanayotokea ndani ya Simba yanaashiria timu hiyo imekuwa haina uhakika wa mambo
inayoyafanya kwa kipindi chote cha misimu miwili.
Baada ya
kwisha kwa msimu uliopita, Simba ndiyo ilikuwa timu iliyofanya usajili wa
wachezaji wengi chipukizi, ilisajili wachezaji zaidi ya kumi ikiwa ni pamoja na
kuwapa mikataba wachezaji wake chipukizi waliokuwa wakiitumikia bila mikataba.
Lakini hilo
halikuwa kubwa sana zaidi ya namna timu hiyo inavyotimua makocha na sasa
imeweka rekodi mpya ya kufanya kazi na makocha wanne katika kipindi cha misimu
miwili.
Simba
imemtangaza kocha mpya, Zdravko
Logarusic, raia wa Croatia, ambaye sasa anachukua nafasi ya Abdallah Kibadeni
aliyeifundisha Simba kwa nusu msimu tu.
Kabla ya Kibadeni, Simba
ilifundishwa na Patrick Liewig, raia wa Ufaransa, ambaye alichukua nafasi ya
Milovan Cirkovic.
Sasa Simba imemtangaza
kocha mpya, Zdravko Logarusic, raia wa Croatia, ambaye anakamilisha idadi ya
makocha wanne katika kipindi cha misimu miwili.
MILOVAN AKISAINI SIMBA MBELE YA RAGE (KULIA) |
Maana yake kila kocha
amefundisha nusu msimu, kwa Logarusic ambaye alikuwa akiinoa Gor Mahia ya
Kenya, kikubwa ni kumuombea aumalize msimu.
Rekodi nyingine ya Simba
ni kwamba, katika misimu miwili, imefundishwa na makocha kutoka katika nchi nne
tofauti.
Milovan kutokea Serbia,
Liewig wa Ufaransa, Kibadeni ambaye ni mzalendo na Logarusic anayekuja ambaye
anatokea Croatia.
Hakuna kocha ambaye
angedumu milele katika kikosi cha Simba, lakini inaonekana hata uongozi wa klabu,
hasa ule wa juu, ulikuwa tatizo kubwa.
Mfano, angalia kila
ulipofika wakati wa kocha kuondoka, sababu zilionyesha kuwa na walakini. Hakuna
ubishi, misimu miwili timu kufundishwa na makocha wanne tofauti inachanganya na
inaonyesha kuna tatizo.
Milovan:
Msimu mmoja kabla alikuwa
ameipa Simba ubingwa na kuiongoza kutoa kipigo cha aibu kwa Yanga cha mabao
5-0.
Lakini uongozi wa Simba
ukamuondoa na kusema alikuwa mvivu, anashirikiana na wachezaji na timu yake
ilikuwa nafasi ya pili katika msimamo. Ikashindwa kumlipa fedha yake hadi Rahma
Al Kharusi ‘Malkia wa Nyuki’ alipojitokeza na kumlipa.
Liewig:
Mfaransa huyu alichukua
nafasi ya Milovan, akafunga safari na Simba hadi Oman kwa kambi ya wiki mbili,
aliporejea sera yake ikawa vijana zaidi na Simba ikaambulia kushika nafasi ya
tatu nyuma ya Azam FC na mabingwa Yanga.
Uongozi wa Simba ukasema
ataendelea kubaki, kosa ni alipofunga safari kwenda mapumzikoni kwao Ufaransa,
akatumiwa salamu na barua ya kufutwa kazi.
Kwa kuwa alikuwa anadai
alirejea, akalipwa nusu hadi ameondoka nchini baada ya kurudi mara ya pili,
Liewig bado anadai dola 8,500 hadi leo.
Kibadeni:
Aliiongoza Kagera Sugar
kushika nafasi ya nne nyuma ya Simba, ikaonekana anaweza na kupewa nafasi ya
Liewig.
Naye ameifundisha Simba
kwa nusu msimu tu, alianza mwanzoni mwa msimu huu, mwisho wa mzunguko wa
kwanza, kikosi chake kimeshika nafasi ya nne nyumba ya Mbeya City, Azam FC na
vinara, Yanga.
Logarusic:
Sasa ni zamu ya Logarusic,
Kocha Bora Kenya msimu wa 2011/12, akiwa na Gor Mahia ya Kenya. Aliiwezesha
kushika nafasi ya pili mara mbili, msimu huu alifundisha nusu msimu kabla ya
nafasi yake kuchukuliwa na Bobby Williamson ambaye awali ilielezwa ndiye kocha
mpya Simba kabla Championi halijakosoa na kuweka mambo sawa kwamba kocha huyo
hakuwa na mpango wa kujiunga na Msimbazi.
Huenda kwa wachezaji
waliokuwa Simba kwa misimu yote miwili, wanapaswa kuwa makini maana
wanalazimika kutumia mifumo mingi kutoka kwa makocha wanne tofauti wenye asili
ya nchi nne, si kitu rahisi.
0 COMMENTS:
Post a Comment