WATANZANIA
tunasifiwa kwa uungwana, lakini sifa yetu nyingine inayosababisha mambo mengi
tunayofanya yakwame ni woga, kitu kibaya sana.
Ukimuuliza
mtu kwa nini ni muoga, hakika ufafanuzi unakuwa hauna nguvu za kukufanya
kuamini kwamba mtu fulani alitakiwa kuwa muoga katika muda fulani, ujinga tu.
Wiki moja
iliyopita, timu ya Zanzibar iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji nchini
Kenya ilikuwa katika tafrani kubwa baada ya wachezaji wake kuzuiwa hotelini
jijini Nairobi.
Wachezaji
hao walizuiwa kwa kuwa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati
(Cecafa), lilishindwa kulipa gharama za hoteli.
Kutokana na
hali hiyo, mmiliki wa hoteli hiyo akaamua kuwashikilia wachezaji, makocha na
viongozi wa Zanzibar Heroes hadi hapo atakapopewa fedha zake.
Awali
ilielezwa kwamba wachezaji hao walikuwa wakipewa ruhusa ya kwenda kuangalia
mechi za michuano ya Chalenji iliyokuwa ikiendelea baada ya wao kutolewa.
Lakini baadaye,
mmiliki wa hoteli akaingia hofu na kuamua kuwazuia kabisa hata kutoka nje na
sasa wakawa kama wanyama au mifugo.
Mwisho
tatizo hilo limemalizika kwa Cecafa kulipa bili ya hoteli iliyokuwa inadaiwa na
Serikali ya Zanzibar kushughulikia suala la usafiri na timu hiyo imerejea nyumbani.
Kinachonishangaza
ndiyo kile ambacho nimeanza
kukizungumzia, woga au inawezekana ni tabia ya kupuuzia tu mambo kutoka kwa
viongozi wetu kuanzia wale wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na hata Serikali ya
Zanzibar.
Kama ni
tamko, basi ni ili mradi tu mtu amesema, hakuna anayeonyesha kiasi gani
tumekasirishwa na uhuni huo wa Cecafa ambayo inaongozwa na Mtanzania, Leodeger
Tenga.
Taarifa
zinasema wakati matukio ya wachezaji na makocha wa Zanzibar Heroes kunyanyaswa
namna ile yakitokea, Tenga hakuwa nchini Kenya na alifika siku ya fainali, siku
ambayo hata Sudan waliocheza fainali na Kenya pia walizuiwa hotelini.
Hii si mara
ya kwanza kwa baraza hilo kufanya mambo ya kipuuzi kama hayo ambayo hayapaswi
kupewa nafasi kwa jamii na hasa katika masuala yanayohusisha utaifa.
Kuidhalilisha
Zanzibar Heroes ni kuidhalilisha Zanzibar, lakini ni kuonyesha dharau kwa taifa
la Tanzania pia. Sasa mbona mmekaa kimya na mnaona ni kama tukio la
kufurahisha?
Cecafa
wataacha lini mambo yao ya kubabaisha kila wakati kama hayo kama viongozi
husika mnakuwa waoga kukemea na ikiwezekana hata kuhakikisha mnasisitiza Cecafa
waombe radhi na ikiwezekana waahidi kwamba itakuwa mwanzo na mwisho?
Msimamo kwa
lengo la kusimamia haki ni jambo zuri, uimara wa viongozi pia ni vizuri
ukaonekana wakati kama huu taifa linapodhalilishwa tena na kikundi tu cha watu
fulani.
Wachezaji
wa timu ya taifa ambao ni askari wa taifa, wanawekwa rehani kama mifugo halafu linaonekana
ni jambo la kawaida! Au mlitaka azuiwe mwanasiasa mmoja ili uwe wakati mzuri wa
kupiga kelele na kujipatia ujiko?
Huu ndiyo
wakati wa kuzima ubabaishaji wa Cecafa ili waachane na kuyafanya mataifa yetu
kuanzia timu za taifa na ikiwezekana klabu zetu kuwa biashara yao kwa ajili ya
kuwaingizia vipato.
Zanzibar au
Tanzania kwa jumla ina uwezo wa kuikemea Cecafa, ikiwezekana kuipa onyo ili
kuachana na ubabaishaji kama uliotokea ambao umewadhalilisha askari hao waliokuwa
wanapigania nchi. Nawakumbusha, viongozi wao, pia ni tatizo katika maendeleo ya
nchi.
FIN.








0 COMMENTS:
Post a Comment