| MKE WA MZEE SMALL, MAARUFU KAMA MAMA SAID |
IJUMAA, Mzee Small alizungumzia namna
alivyozushiwa kifo na kufurahishwa kwake na Watanzania walivyoonyesha kumjali
baada ya kusikia taarifa hizo.
Lakini akasisitiza bado anaumwa, upande
mmoja wa mwili wake umepooza na analazimika kutembea kwa kujivuta huku akitumia
fimbo. Je, maisha yake yakoje? Endelea.
MZEE Small anasema maisha kwake ni
magumu sana kwa kuwa wakati fulani alikuwa akiendesha maisha yake kwa kuuza
maji kupitia visima vyake.
Sasa mambo yamekuwa magumu na hasa
kutokana na gharama kubwa za matibabu ambazo amekuwa akitoa.
“Kama ulivyoona leo, ninakwenda kufanya
mazoezi mara mbili kwa siku na kila ninapokwenda lazima bodaboda ije kunichukua
na kunirudisha.
“Si kitu kidogo kwangu kwa kuwa sina
sehemu inayoweza kuniingizia kipato kwa uhakika ili niweze kujihudumia katika
kiwango kizuri na kwa asilimia mia.
“Ila ninasisitiza, sitaki kutangaza
kwamba ninaomba msaada. Ninajua wako wenye mapenzi na mimi na wakijisikia
kufanya hivyo basi nitafurahi.
“Naogopa kusema nisaidieni maana watu
wana majukumu na matatizo yao, lakini kwa anayeona anaweza kufanya hivyo,
nitajisikia faraja.
“Wakati mwingine hata mtu kama akitokea
kunitembelea kama mlivyofanya nyie nafurahi.nasikia faraja sana,” anasema Mzee
Small.
Hata hivyo, Mzee Small anasisitiza
pamoja na shida zote anazopata, mkewe ni kama dereva wa kila kitu naye
anamchukulia tena kama ndugu na si mkewe tu pekee.
Pamoja na hivyo, Mzee Small ambaye ni
gwiji wa uigizaji nchini anaonyesha kuingia hofu na mkewe, kwamba anaweza
kuchukuliwa na mtu fulani, halafu bila ya kusita anapiga mkwara mzito, tena
hadharani.
“Mimi katika hili nitakuwa mkweli tu
bila ya woga, kama nitasikia kuna mtu anataka kufanya ujanja na kumchukua mke
wangu, sitachelewa, nakuambia namroga aokote makopo.
“Huyu mke wangu amekuwa akifanya kila
kitu kwa ajili ya kuhakikisha napona. Sasa mimi namuona si mke tu, huyu ni kama
ndugu yangu.
“Unajua anapambana, anafanya kila juhudi
kuona nina nafuu na mambo yangu yanarejea katika hali nzuri. Sasa kama anatokea
mtu anataka kumchukua unadhani nitafanya nini, maana nguvu za kupambana naye
sina.
“Kilichobaki ni kumroga tu, hata
ikiwezekana aokote makopo kama nitaweza kweli kufanya hivyo,” anasema Mzee
Small, kawaida yake vituko haviishi (anaangua kicheko).
Pamoja na mkwara huo kuhusiana na mkewe,
Mzee Small anasema amekuwa akishangazwa na baadhi ya ndugu zake kumtupia lawama
mkewe.
“Wakati mwingine kuna baadhi ya ndugu
zangu wamekuwa hawaelewi, wanamtumia mke wangu lawama nyingi sana, wanahisi ananipotosha,” anasema.
“Si sahihi, maana hata baada ya
kuzushiwa kifo, kuna ndugu walisema mke wangu ndiyo kasababisha, eti amekuwa
akinipeleka sana kwenye vyombo vya habari, nasema si kweli.
“Wakati watu wanaanza kupiga simu, wote
tulikuwa chumbani tumelala, hakuna aliyejua kati yetu. Nakumbuka mlikuwa wa
kwanza kutaka kujua, mara tu baada ya kuzungumza nanyi, basi hatukulala tena,
maana simu ziliendelea kutoka kwa watu mbalimbali ambao walitaka kupata
uhakika.”
Kuhusiana na suala la matibabu, pamoja
na mazoezi, Mzee Small amekuwa akihangaika kila aina ya tiba ilimradi apate
kupona tu.
“Kuna kipindi nilipata mganga wa
kienyeji kutokea Kigoma, alitaka nimuandalie sehemu ya kulala ili aje hapa
anitibu. Nilifanya hivyo, lakini alipofika Dar, ilikuwa ni vituko na havina
mfano wake, hadi nikakasirika.”
MZEE SMALL anasema mganga wa kienyeji
aliyehamia kwake alizua vituko ambavyo havikuwa na mfano. Ni vituko vipi,
mwisho wake ilikuwaje na alichukua uamuzi gani? ENDELEA KUFUATILIA KESHOKUTWA
JUMATANO.







0 COMMENTS:
Post a Comment