Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuph Manji ametangaza rasmi kutowania
tena nafasi ya uenyekiti kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakaotangazwa
baadae mwakani.
Manji ametoa ametoa tamko kuhusiana na suala hilo alipozungumza na
waandishi kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani, Kariakoo jijini
Dar es Salaam.
Manji amesema ameamua kuwapisha wengine wenye uwezo wa kuiongoza timu hiyo nao
kuchukua jahazi.
“Sitagombea tena uenyekiti kwenye uchaguzi ujao, nimetangaza ili
kuwapisha watu wengine ambao wana uwezo waingie na kuendeleza kutoka
nilipoishia,” alisema.
Manji ataendelea kuwa kiongozi wa Yanga kwa miezi ijayo saba hadi hapo
utakapoitishwa uchaguzi huo, hapo mwakani.
Manji amesisitiza, baada ya muda huo kwisha naye kutogombea, basi
angependa kuendelea kubaki kama mwanachama na shabiki wa kawaida.
Taarifa za uamuzi huo wa Manji huenda zikawashtua wanachama wa Yanga
ambao walionyesha kufurahishwa na mabadiliko aliyoyafanya.
Manji aliamua kugombea siku chache baada ya Yanga kupoteza mechi yao
ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba kwa kufungwa mabao 5-0.
Alisema aliamua kuingia kugombea ili apate nafasi ya kuongoza kutokana
na kuona kwamba mambo yalikuwa yamevurugika, wanachama hawakuwa wakiuamini
uongozi na hofu iliingia.
Baada ya kushinda uchaguzi alisema kitu cha kwanza kilikuwa ni
kurudisha imani kwa mashabiki wa Yanga na alifanikiwa.
Alitaka wajiamini tena na kuamini kwamba Yanga iliteleza tu na
kufungwa mabao yale matano na inaweza kurejea katika hadhi yake.







0 COMMENTS:
Post a Comment