Uongozi wa Tawi la Simba la Mpira Pesa, lililopo Magomeni Mikumi
jijini Dar, umempa siku moja, yaani hadi kufikia kesho Jumamosi, Mwenyekiti wa
Simba SC, Ismail Aden Rage, awe amejiuzulu wadhifa wake kwa kile walichosema
hawana imani naye tena.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa tawi hilo, Masoud
Hassan ‘Ustaadh’, mwenye kadi namba 536, aliainisha makosa matatu muhimu
yanayomkabili Rage ya kukiuka katiba ya klabu yao pamoja na ile ya Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), hali inayoiweka Simba katika hali ya sintofahamu mpaka
sasa.
Alisema kuwa, kama Rage asipojiuzulu hadi kufikia kesho, wanachama
wote wa tawi hilo wataandamana hadi bungeni mjini Dodoma kumshtaki kwa Spika wa
Bunge.
Aliyataja makosa hayo kuwa ni kudharau tamko la TFF lililomtaka
kuitisha mkutano mkuu wa dharura ndani ya siku 14 ambazo zinakwisha leo Ijumaa,
kumuingiza Michael Wambura kwenye Kamati ya Utendaji ya Simba kinyume na katiba
na kugomea kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa klabu uliokuwa ufanyike Desemba,
mwaka huu.
“Mpira Pesa tumechoshwa na Rage na hali inavyoondelea anataka
kuihatarisha klabu yetu, tunamuomba kiungwana kufikia Jumamosi (kesho) awe
amejiuzulu, vinginevyo Jumatatu tumepanga kuandamana kwenda bungeni kumshitaki
kwa kiongozi wake wa bunge, Anna Makinda,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment