January 24, 2014





SAKATA la mshambuliaji Emmanuel Okwi limechukua sura mpya na sasa limeegemea upande wa Yanga ambao awali walionekana kushinda vita ya kumpata Mganda huyo kwenye kikosi chao.


Lakini uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba imesitisha usajili wake siku chache kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara unashtua kidogo.

Wengi wameshangazwa na hilo, ukweli haikuwa sahihi na huo ni mfano wa kuonyesha namna mambo mengi ambavyo yamekuwa yakichelewa kwa kuchukuliwa uamuzi katika wakati ambao si mwafaka. Lazima kuwe na marekebisho katika hilo.

Hakika uamuzi walioufanya ulikuwa ni mzuri kwa maana unaweza kuisaidia baadaye Yanga, ingeweza kumchezesha Okwi halafu ikajikuta inapokwa pointi, kitu ambacho kingekuwa hatari zaidi. Sasa isubiri uamuzi wa Fifa.

Pamoja na uamuzi mzuri ambao huenda utakuwa msaada mkubwa kwa Yanga, lakini TFF lazima ijifunze kuwa uamuzi wa haraka kutokana na hali halisi ni jambo bora. Ndiyo maana Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa), wao walichukua hatua haraka.

Leo TFF wamejichanganya, mwanzo walionyesha usajili wa Okwi hauna tatizo, leo wanasema tofauti!

Achana na hilo, kabla ya kufafanua kwa nini nasisitiza na TFF nao wanapaswa kuwajibika, nataka kuwakumbusha Yanga kwamba kuna mambo ya kujifunza kabla ya kuyafanya.

Mimi na wadau wengine wa soka tutaendelea kusikiliza hadi mwisho jibu litakapotolewa, lakini wao Yanga pia wanapaswa kujifunza kwa kuwa suala hili hata kama wakifanikiwa kushinda, lakini waliamua kuingia katika sehemu ya mgogoro na waliujua.

Namna Okwi alivyokwenda Uganda kujiunga na SC Villa kulikuwa na mkanganyiko kweli kama ilikuwa sahihi kuuzwa. Lakini wao walisema ni sahihi, kama ni kweli basi sawa lakini itakapogundulika si sahihi itaonyesha hawakuwa tayari kujifunza. Mimi bado nahisi kuna walakini.

Sasa narudi kwenye hoja ya msingi kwamba kwa nini nasisitiza kuwa TFF nao wanapaswa kuwajibika, tokea sakata la uhamisho lilivyoanza wakati Okwi anakwenda Tunisia, Simba haikulipwa fedha zake dola 300,000 (zaidi ya milioni 480) ambao inaendelea kuhadi hadi leo na imekuwa hadithi.

Baadaye iligundulika, ofisa mmoja wa TFF alishirikiana na kiongozi wa juu kutoa uhamisho wa Okwi kwa madai kwamba ilikuwa ni lazima ifanyike hivyo na muda ulikuwa umeisha. Sawa, lakini hadi leo Simba inadai fedha zake, ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amekuwa tatizo, awajibike.

Lakini hata huyo ofisa wa TFF pia ni tatizo, safari hii taarifa zinaeleza kwamba alishughulika pamoja na viongozi wa Yanga kuhakikisha Okwi anajiunga na Yanga na inawezekana alijua kabisa kufanya hivyo si sawa.

Sielewi ili atekeleze kazi yake huwa anapewa kitu gani hadi anaamua kufanya mambo ilimradi tu! Leo tatizo jingine limeibuka ambalo kwa kiasi fulani linafanana na lile la mwanzo la Okwi kuondoka.

Tunajua utaalamu wa utoaji vibali vya kimataifa unavyufanya na TFF ina kitengo maalum na kinahusika, ofisa huyo ndiye alikuwa akifanya kazi hiyo. Bila ya kujali yupo au hayupo, TFF inapaswa kuwajibika kwa kuziingiza Simba na Yanga kwenye matatizo.

Rage awajibike, ofisa huyo wa TFF pia awajibike kama si yeye, basi shirikisho lenyewe na mwisho viongozi wa Yanga nao wanapaswa kujifunza kwa kuwa wakiendelea hivi, itafikia siku wataangukia kwenye hasara kubwa itakayowaumiza.

Unaweza ukahoji kwamba TFF haihusiki kwa kuwa upatikanaji wa ITC unaweza ukafanywa na maofisa wa klabu, lakini mwisho ofisa huyo alishirikiana na Simba, halafu Yanga na kote kuna matatizo tena makubwa.

Kiasi gani inaonekana Watanzania wasivyokuwa makini, lakini bado nasisitiza kama ambavyo imekuwa siku zote, suala la Okwi limejaa ubinafsi, linalohusisha watu wengi waliotaka kushibisha matumbo yao ndiyo maana mwisho unaweza kuona hivi;

Simba inaidai Etoile (hakuna malipo), Yanga inalia na fedha ilizopoteza (hakuna wa kuzilipa), halafu Okwi anaenda zake!

1 COMMENTS:

  1. Ni kweli nah Hana na wewe kuwa TFF inastahili lawama lakini kwa undani zaidi hili lilichangiwa na afisa wa secretariat ya TFF ambaye ama kwa ushabiki au kwa hongo aliamua kuficha nyaraka za FIFA zilizopo TFF juu ya suala hili. Na hili pia linachangiwa na Yanga wenyewe ambao inaonesha walitaka iwe hivyo kusudi wamtumie mchezaji huyo lakini mbeleni lingewaletea wenyewe. Hata Mbuyu Twite ni hivyo hivyo maana transfer yake ilikuwa ifanywe kutokea Rwanda lakini ili wawazunguke Simba wao wakapitia Congo na hao hao waliofanya magumashi ya sasa ndio waliofanya ya Twite. Itakuwa bora TFF iwachukulie hatua za dhati kabla hawajatutia aibu zaidi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic