January 24, 2014





Na Saleh Ally
HISTORIA inaonyesha Ureno na Hispania ni nchi zilizopita kwenye mambo mengi yanayohusisha uhusiano mzuri na mbaya.

Mwaka 1777, kulikuwa na vita ya mipaka kati yao, ilidumu kwa zaidi ya miaka mia. Katika karne ya 18, Ureno ikaegemea kwa Uingereza na Hispania kwa Ufaransa. Zikawa na uadui mkubwa.

Nchi hizo mbili ni jirani na ndiyo zilizo katika Peninsula ya Iberia, Kusini mwa Ulaya, zinapakana kwa karibu kabisa na Algeria iliyo Kaskazini mwa Afrika. Urafiki wao umepewa jina la Uhusiano wa Iberia.


Urafiki wao umekuwa ukitafsiriwa kuwa ni wa kinafiki kutokana na historia inavyoonyesha na mara nyingi Wareno wanawatuhumu Wahispania kwa kuonyesha wao ni watu wa daraja la juu kuliko wao.
Ingawa wengi wamekuwa wakiutafsiri urafiki wa nchi hizo kuwa ni wa kinafiki, lakini hivi karibuni zilionyesha zinaweza kufanya kazi pamoja zilipoomba kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 kwa kushirikiana.

Mara nyingi suala hilo linaonekana kufichwa, lakini wakati Kocha Jose Mourinho akiwa Madrid ilionekana wazi tofauti zao zilikuwa ni za Kihispania na Kireno, ndiyo maana zaidi alizozana na Iker Casillas na Sergio Ramos.

Lakini waliowatetea wachezaji wa Real Madrid walikuwa wale wa Barcelona, Xavi na Iniesta, na utetezi ulilenga utaifa zaidi. Ndiyo maana hakuna ubishi kwamba hata vita kati ya Mourinho na kiungo mshambuliaji, Juan Mata, inaonekana hivyo.

Hakuna sababu ya kushangaa kwamba Mata alikuwa upande wa akina Ramos, Casillas, Xavi na Iniesta. Haijulikani alichowahi kusema lakini kuna gazeti la Hispania liliandika kuwa lazima Mata atahama Chelsea kwa kuwa Mourinho ni Mreno.

Sababu za Mourinho kumkataa Mata hazitoshi, kitaalamu au hata katika hali ya kawaida, lakini mwisho amekubali aondoke kirahisi.

William:
Dalili za kwamba Mourinho alipania Mata kuondoka ni pale alipolazimisha usajili wa William kutoka Anzhi Makhachkala. Lakini kama haitoshi akaongeza mshambuliaji wa kati kutoka Ujerumani, André Schürrle.

Mourinho aliuita mpango wake huo kama utanuzi wa kikosi, lakini wakati anafanya yote hayo, alionyesha wazi hakutaka Mata acheze.

Rooney:
Kama hiyo haitoshi, ingawa zoezi lake lilikwama, Mourinho alitaka kumsajili Wayne Rooney kutoka Manchester United, maana yake ilikuwa ni kuziba kabisa nafasi ya Mata.

Hata kama sasa Mata atacheza Manchester United, kupatikana kwa nafasi hakutakuwa shida kwa kuwa hawana mtu imara wa kushoto kama ilivyokuwa kwa Chelsea ambayo pamoja na kuwa na mawinga wawili bora, bado ilikuwa imemuongeza William.

Oscar:
Kweli ni kati ya wachezaji bora wa Chelsea na Ligi Kuu England, lakini hajawa na kiwango bora kama cha Mata ambaye amekuwa mchezaji bora wa Chelsea kwa misimu miwili iliyopita.

Kama ni kufuatilia misimu iliyopita, Mourinho alikuwa hawezi kumchagua Oscar akamuacha Mata.


Msimu huu:
Msimu huu Mourinho, amefanikiwa kumvuruga Mata. Kwani amekuwa akimtoa au kumuingiza dakika chache tu, hivyo katika mechi 13, ametoa pasi mbili tu za mabao, hana bao.

Lakini msimu uliopita, pamoja na kuwa mmoja wa wafungaji alitoa pasi 12 za mabao na kuwa bora zaidi ya wote katika Premiership.

Mata ambaye ni mchumi kitaaluma ameonyesha kiwango cha juu kwa kipindi chote ambacho amekuwa Chelsea, tena amekuwa juu kuliko mchezaji yeyote.

Vipi Mourinho anaweza kumtoa mchezaji ambaye ni bora kuliko wote katika kikosi? Hiyo ndiyo dalili ya vita ya makabila mawili au nchi mbili tofauti.

Kama ilivyoelezwa awali kwamba Wahispania wamekuwa wakiamini Wareno ni watu wa chini, huenda Mourinho naye ameamua kuwaonyeshea kwamba yeye ni zaidi yao.

Hata kuondoka kwake Madrid kulihusishwa na kuzidiwa na nguvu ya Uhispania, akawa hana ujanja. Je, naye anaendeleza hasira zake?

Kama kweli atakuwa amefanya hivyo, maana yake amekubali kuharibu kwa kushindwa kusimamia weledi na badala yake ameangukia kwenye kupigania haki za kabila au taifa moja akiutumia mpira.

Si rahisi kuamini kocha makini kama Mourinho anafanya hivyo, lakini hizi ni dalili kwamba kweli hakuna binadamu aliyekamilika!

WAKALI WA PASI ZA MWISHO 2012-13
1.    Juan Mata (Chelsea) 12
4.    Wayne Rooney (Manchester United) 10
5.    Theo Walcott (Arsenal) 10
6.    Steven Gerrard (Liverpool) 9
7.   Lukas Podolski (Arsenal) 9
8.   5. Shaun Maloney (Wigan Athletic) 8
9.   Robin Van Persie (Manchester United) 8
   David Silva (Manchester City) 8
10.                     Carlos Tevez (Manchester City) 8

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic