January 29, 2014



Na Saleh Ally
Jezi namba 10, iwapo katika timu ya taifa hilo mchezaji atapewa jezi hiyo, basi anajua ana mzigo mkubwa na anatakiwa kuibeba timu.

Hii imekuwa hivyo hata katika timu nyingi zinazoshiriki ligi za juu za Brazil, mfano Corinthians, Vasco Da Gama na nyingine za Brazil. Kwa kifupi jezi namba 10 ina heshima kubwa.
Hali hiyo inatokana na jezi hiyo kupata mafanikio makubwa akiwa nayo mchawi mweusi, Pele. Utaona hata Argentina wamefuata hilo, kwa kuwa tu Diego Maradona alifanya makubwa akiwa na jezi namba 10.
Hali hiyo ilisambaa duniani kote na heshima ya jezi namba 10, ikawa haishikiki kwa kila klabu. Angalau kufanya vizuri kwa Romario akiwa na namba 11 na Bebeto akiwa na namba 7 (au unaweza kusema #7 kwa kuwa alama # inawakilisha neno namba), katika Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani, ikapunguza makali ya namba 10.

Burudani zaidi ni jezi namba 7 katika kikosi cha Manchester United, ndiyo inayoheshimiwa zaidi na inahofiwa na wachezaji wengi wakiwemo nyota wenye uwezo mkubwa uwanjani.
Wako ambao wamewahi kukabidhiwa wakakataa, lakini wengine waliwahi kuivaa na baadaye wakaamua kuivua na kuna wale waliosajiliwa Man United, halafu wakakataa kuichukua pamoja na uongozi na kocha kuona wana uwezo wa kuifanyia kazi.

Hali hiyo inatokana na presha kubwa kwa yeyote anayeivaa jezi hiyo, hata kama ana uwezo mkubwa, lakini lazima awe jasiri kwa kuwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10, imekuwa gumzo na tatizo pia, kwamba ukiivaa ukafeli, basi umeondoka.

Wiki iliyopita, Juan Mata ambaye amejiunga Man United akitokea Chelsea, pia ameingia katika kundi la wachezaji ambao wameikataa jezi namba 7. Pamoja na mambo kufanywa kwa uficho, inaelezwa Mata alimuomba Kocha David Moyes amruhusu kuvaa jezi namba 8 iliyokuwa inatumiwa na Anderson ambaye amepelekwa kwa mkopo hadi mwisho wa msimu kwenye kikosi cha Fiorentina ya Italia.

Ingawa awali ilielezwa kwamba Manchester United wameihifadhi jezi hiyo kwa kuwa wanaamini Cristiano Ronaldo  atarejea, lakini ukweli Mata alihofia presha kuu mbili, kwanza ametoka Chelsea akionekana hana uelewano na Kocha Jose Mourinho, pili haikuwa sahihi kujiongezea presha na watu waanza kumpiga kwa namba ya jezi.
Miezi kadhaa, Antonio Valencia naye aliamua kuivua jezi hiyo na kuirudisha, akachukua namba 25 na alieleza kweli kwamba presha yake ni kubwa kwenye kikosi cha Manchester United.

Rekodi zinaonyesha, Valencia hakuwa mchezaji wa kwanza kuikataa jezi hiyo. Pamoja na ubora wake, Wayne Rooney ‘Wazza’ naye alinyoosha mikono, akaikataa jezi hiyo, akaamua kutoka kwenye jezi namba 8 na kuchukua 10 ambayo anaitumia sasa.

Jezi namba 8 hapo kabla ilitumiwa na viungo wawili wakorofi wa Man United, Nicky Butt na Paul Ince. Utaona hakuna aliyehofia kuichukua, Rooney alifanya hivyo na baadaye Valencia. Lakini Michael Owen alionyesha ujasiri, mara baada ya kutua Man United akakubali kuichukua jezi hiyo ‘kimeo’, mwisho wake akafeli.
Unaweza kujiuliza, nini kinawaogopesha wengi kuhusiana na jezi hiyo, mafanikio makubwa waliyopata wachezaji watano ambao waliivaa awali au ni nini?
Mkongwe zaidi, George Best aliyekuwa mchezaji kipenzi cha mashabiki wa Man United katika miaka ya 1960 na 70 mwanzoni, alifanya vizuri akiwa na jezi hiyo na baadaye ilikuwa ni zamu ya Bryan Robson ambaye alikuwa nahodha wa Man United pia kipenzi cha mashabiki.

Jezi hiyo ikahamia kwa mtukutu Eric Cantona na mchezaji wa kwanza kutoka nje ya Uingereza kuivaa na kupata mafanikio makubwa. Pamoja na ujeuri kupindukia lakini nyota yake katika miaka ya 1990, iliifanya Man United kuwa tishio.

Alipoondoka jezi hiyo ikabaki kwa muda bila kupata mtu lakini baadaye Kocha Alex Ferguson, aliamua kumwika kinda David Beckham baada ya kupata mafanikio makubwa. Aliendelea kuing’arisha hadi timu ya taifa ambako alipewa unahodha kama ilivyokuwa kwa Man United na kuifanya jezi hiyo ipate umaarufu mkubwa pia kwa taifa hilo.
Shujaa pekee aliyekubali kuuvaa mzigo wa Beckham, safari hii mgeni tena kutoka nje ya Uingereza alikuwa Cristiano Ronaldo. Ameonekana ni zaidi ya wengine, kwani 2008 alichukua uchezaji bora wa dunia akiwa nayo, kaendeleza utamaduni hadi alipokwenda Madrid ambako ameshinda uchezaji wa dunia tena, safari hii akiwa nje ya United.

Baada ya hapo, kila mmoja anaihofia na swali la wengi limekuwa hivi, nani atakubali siku moja kuivaa jezi hiyo kimeo na kupambana hadi kufikia mafanikio kama ya waliowahi kuivaa?



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic