Na Maulid Kitenge
KOCHA wa Simba Mcroatia, Logarusic wiki iliyopita alifanya kitu
ambacho kilimshangaza kila mmoja wakati Simba ilipokuwa inacheza na Rhino
Rangers ya Tabora kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kitendo hicho ni kile cha kumuingiza
dakika kama ya 86 hivi kwa mshambuliaji Betram Mwombeki na kisha na kumtoa
dakika chache tu baada ya kumuingiza.
Imewashangaza watu kiasi mpaka
kitendo hicho kulaaniwa na Chama cha Wanasona Tanzania (Sputanza).
Kimewashangaza watu kwa vile
haijueleweka kosa la Mwombeki ni nini mpaka alimuingiaza na kumtoa dakika
chache. Kitendo hicho kilionekana kumuuzunisha Mwombeki kiasi cha wachezaji
wenzake kumpoza baada ya mechi.
Logarusic kwa mtazamo naona ni mwalimu
ambaye anacheza sana na jukwaa na kutafuta sifa zaidi na hii ni hatari sana
kwake. Aombe Mungu mambo yaende vizuri lakini siku yakibadilika ni hao hao
mashabiki watakaombadilikia.
Ukiangalia amekuwa na mbwembwe nyingi
zisizo za maana kabisa kwa Kocha makini hapaswi kuwa hivyo hata kidogo. Kitendo
cha kubadili tu mchezaji anavyojisikia, kucheza na jukwaa na maneno mengi
yasiyokwisha ipo siku yatamtokea puani. Lakini kwa vile mambo sasa yanakwenda
vizuri hakuna anayeona hili.
Kitu kingine ambacho
kilinistaajabisha kwa kocha huyu Mcroatia ni kitendo wakati mchezaji wake
Ramadhani Singano akipiga penalti katika mechi hiyo yeye kugeukia kwa mashabiki
akiwa hataki kuangalia.
Hivi najiuliza ataonaje makosa ya
mchezaji wake kama Kocha na wewe unaogopa kuangalia penalti ya mchezaji wako?
Hii ilinishangaza kweli.
Logarusic anachofanya yeye ni zaidi
ya shabiki sasa. Hivi juzi tumesikia ameingia katika bifu na beki wake Joseph
Owino kiasi cha kumpeleka kikosi cha pili. Anaonekana anafanya ukali
pasipokuhitajika ukali.
Nakubaliana naye katika suala la
nidhamu lakini sio katika ukali anoufanya na kucheza na jukwaa hasa katika
mechi. Ndiyo maana nasema wakati huu mambo yanaenda vizuri mashabiki utakuwa
nao mgongoni lakini mambo yakibadilika, utabaki mwenyewe Logarusic.
Punguza mbwembwe zisizo na maana na
jaribu kufanya mambo kama kocha unayejiamini na upunguze maneno, maana watu
wangependa kuona Simba inacheza soka ya kueleweka kwa kuwa na Kocha wa kigeni
sio mbwembwe zisizo na maana. Ni hilo tu.
Kuna mengi yanaweza kujitokeza, kuna
sehemu Logarusic anaweza akawa sahihi, lakini suala la kukosea pia linamgusa
kutokana na matendo anayofanya.
Mpira ni mchezo wa makosa, haiwezekani
kila akikosea mchezaji, basi anakwenda benchi, lazima kuwe na utaratibu ambao
unatambulika.
Kweli Logarusic ni mtaalamu, lakini
anatakiwa kujua uongozi unahusisha mambo mengi ikiwemo molari pamoja upendo.
Lazima ajue, muhimu kuonyesha upendo na kukosoa kwa lengo la kufundisha si
kukatisha tamaa au kuharibu.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment