Na Saleh Ally
KUKAA nje kwa Lionel Messi kwa takribani miezi miwili sasa
kumekuwa gumzo kubwa katika soka duniani.
Lakini juzi amecheza mechi yake kwanza tangu kurejea
uwanjani huku karibu kila upande duniani ukiwa na hamu ya kutaka kujua kama
kweli atakuwa sawa. Mechi hiyo ilikuwa ni ya Copa del Rey na Barcelona ilikuwa
ikitoana jasho la Getafe na kufanikiwa kushinda kwa mabao 4-0.
Messi raia wa Argentina anaaminika ndiye mchezaji bora
zaidi katika kipindi hiki ingawa kumekuwa na mjadala wa kila aina.
Kurejea kwake na mabao mawili kumezua mengi, lakini
kufunga tu hakujawa sababu ya gumzo, badala yake kweli yuko fiti.
Kuonyesha kweli yuko fiti, Messi aliingia katika dakika ya
61 kuchukua nafasi ya Andres Iniesta, halafu akafanikiwa kufunga mabao hayo
mawili huku akionyesha uwezo wake kama ilivyozoeleka.
Kimahesabu, Messi amecheza dakika 29 na kufanikiwa kufunga
mabao mawili, hakuna ubishi sasa yuko fiti.
Lakini kivutio kingine ni kwamba, Messi amefunga mabao
hayo mawili ndani dakika tatu tu. Bao moja katika dakika ya 89 na dakika za
nyongeza.
Hali hiyo inaonyesha mambo mawili, kwamba yuko fiti kweli
kimwili na kisaikolojia, lakini ana uwezo wa kucheza kwa kasi zaidi kila muda
unavyosonga uwanjani, ndiyo maana akafunga hata kipindi ambacho mpira
unakwisha.
Inaonyesha kiasi gani dunia ilikuwa inamsubiri Messi kwa
hamu kubwa kwa kuwa vichwa vya habari vya kila aina vyenye ufundi wa aina yake
vilitundikwa kwenye magazeti na runinga mbalimbali.
Inakadiriwa zaidi ya vichwa vya habari 200 viliandikwa
kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari kama runinga na magazeti katika
mabara ya Ulaya, Amerika Kaskazini na Kusini. Huenda kesho vikaongezeka kupitia
magazeti ya Tanzania na kwingineko Afrika na Asia.
Hata magazeti yenye mtazamo au upinzani na Catalonia
anakotokea Messi kama lile la Marca ambalo liko jijini Madrid lilikubali kuweka
kichwa kikubwa cha habari: “Messi amerudi”, halafu likaongeza: “Alihitaji chini
ya nusu saa kuonyesha yuko fiti.”
Upande wa eneo la Catalonia ndiyo usiseme, vichwa vya
habari hadi vilivyoonekana kukiuka maadili ya uandishi vilitupiwa kwenye
magazeti kadhaa.
Lakini mengi yalieleza kurejea kwa “Masta” au “Mfalme”,
huku vyombo hivyo vikisifia namba alivyoonyesha uwezo mkubwa pia kufunga mabao
mawili ndani ya dakika tatu na moja akiwa ‘amewakokota’ mabeki wawili kabla ya
kufunga kiufundi.
Ajabu zaidi ni vichwa vya habari lukuki kutoka barani
Amerika Kusini ambako mchezo maarufu zaidi ni ule wa mpira wa kikapu.
Lakini gumzo lilikuwa ni mabao mawili ya Messi ndani ya
dakika tatu na sekunde 31, huku wachambuzi wakisisitiza ni mchezaji wa kipekee
na hakuna wa kumfananisha naye.
Runinga maarufu ya michezo ya ESPN na ile kubwa namba moja
duniani kwa habari ya CNN, zilitenga muda maarufu kuelezea kurejea kwa Messi na
alichokifanya katika mechi hiyo ya Copa del Rey.
Kwao Argentina hasa katika mji aliozaliwa wa Rosario mambo
yalikuwa tofauti, wengi waliisubiri mechi hiyo kama vile ni ya Kombe la Dunia,
lakini walitaka kuhakikisha kama kweli Messi amerudi na anaweza kufanya
makubwa.
Kila bao lake lilishangiliwa kwa nguvu na kelele
zilisikika sehemu kadhaa za mji huo, Gazeti la The Buenos Aires Herald liliandika:
“Kasi ya ajabu”, halafu likasema ni ahueni kwa Kocha Gerardo Martino katika
mechi ya kesho Jumamosi dhidi ya wakali Atlético Madrid. Gazeti la Argentine Daily
Olé likaandika kichwa: “Muuaji kazini”.
Messi aliumia Novemba 10, mwaka jana na tokea hapo
ilionekana La Liga imedorora kwa kuwa Cristiano Ronaldo hakuwa na mpinzani wa
kumtoa jasho na hata Diego Costa wa Atletico Madrid alipofanya vizuri
alionekana si saizi yake.
Messi amekuwa na sifa ya kutoumia mara kwa mara, huenda
ndiyo maana imekuwa gumzo kutokana na kuumia kwake. Hata hivyo bado ana muda wa
kuthibitisha kama kweli yuko sawa na mechi ya kesho dhidi ya Atletico Madrid
inaweza kutoa majibu.
Kwa sasa Messi na Ronaldo ndiyo wachezaji wanaotupiwa
macho na kutegewa masikio zaidi mwingine yoyote kwa sasa.
Kurejea kwake, hivi karibuni kutaanza kurudishwa kwenye
ushindani dhidi yake na Ronaldo anayepewa nafasi zaidi ya kutwaa tuzo ya Ballon d'Or.
0 COMMENTS:
Post a Comment