Na Saleh Ally
AL AHLY ndiyo habari ya mjini na tayari
wako jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili leo alfajiri kwa ndege ya Shirika
la Ndege la Misri au Egypt Air wakitokea kwao Cairo.
Mabingwa hao wa Afrika wako jijini Dar es
Salaam, kuwavaa mabingwa wa Tanzania, Yanga, katika mechi ya kwanza ya Ligi ya
Mabingwa kabla ya kurudiana wiki moja baadaye jijini Cairo.
Yanga haijawahi kuifunga Al Ahly tangu
zilipoanza kukutana, ushindi dhidi ya Waarabu hao wa Afrika Kaskazini huwa ni
sare. Katika mechi itakayopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, watakachotaka Yanga ni kusonga mbele.
Kusonga mbele kwa Yanga lazima kusiwe na
miujiza, badala yake ni kuhakikisha wanavunja rekodi kwa kuifunga Ahly katika
mechi ya kwanza hiyo Jumamosi kabla ya kupanga itapambana vipi jijini Cairo.
Kuwang’oa vigogo hao si kazi ndogo,
lakini katika soka hakuna linaloshindikana na kama Yanga wakijipanga vilivyo,
basi watakuwa na uwezo wa kuwaondoa, lakini ni lazima washinde mechi ya Dar es
Salaam.
Ahly ni bahari, kuishinda kunahitajika
mipango mingi na lazima iwe kuanzia nje, yaani kabla ya mechi na wakati wa
mechi. Moja ya mbinu zao ni kugomea, kupoozesha mchezo, kupoteza muda hasa
wakianza kufunga na kushambulia kwa kushtukiza.
Wao pamoja na kwamba watakuwa ugenini,
lakini wana mifumo mingi ambayo wataifanya kuhakikisha wanashinda au kupata
sare ya ugenini ili kujiweka katika nafasi nzuri.
Wanapokuwa ugenini, mara nyingi
wakifungwa ni sare na wanapokwenda kwao, basi wanahakikisha wanashinda. Mifumo
ni mingi kuhakikisha wanapata sare hiyo na utaona wanapocheza kuwa ni watu
waliojipanga na wanajua wanachokifanya.
Vurugu:
Yanga wanapaswa kuwa makini na mambo
mengi, kuanzia nje ya uwanja ni namna ambavyo Waarabu hao wanakuwa na vituko,
wanaotaka kuonyesha kwamba wanaonewa, hawajaridhika na wanatumia muda mwingi
kusababisha hali ya mabishano.
Utaona watataka kukataa basi,
watasisitiza hawataki hoteli, hawamtaki mtu fulani waliyepewa, wanaweza kubeba
maji yao, ikiwezekana hata chakula na wakati wa kupikiwa lazima awepo mtu wao.
Wanachotaka kufanya ni kuona nguvu nyingi
ya wenyeji wao inawalenga wao, Waingereza wanasema attention. Yaani mnaelekeza akili
yote kwao, kumbe wao wameshafanya maandalizi ya kutosha.
Wanaamini kunapokuwa hakuna utulivu, ni rahisi
wao kupanga au kung’amua ni nini cha kufanya. Hivyo Yanga lazima wawe watulivu
kama walivyofanya Simba mwaka 2003, Zamalek ilitua Dar es Salaam ikakutana na
kipigo cha bao 1-0, mfungaji akiwa Emmanuel Gabriel ‘Batigol’.
Dawa:
Tabia za timu nyingi za Kiarabu ni ujanja
nje ya uwanja, kingine ambacho kinatumika ni moja ya dawa ambayo hupunguza
nguvu ya mtu kama akiivuta na lazima Yanga wawe makini hata wakiwa nyumbani.
Mwaka 2009, wakati Taifa Stars inafuzu
kwenda kucheza Chan nchini Ivory Coast, iliitoa Sudan, wakati huo kukiwa hakuna
Sudan Kusini.
Wakati wa mechi ya Dar es Salaam,
Wasudani walijaribu kufanya mchezo huo, wakashitukiwa. Wakiwa kwao Khartoum,
pia walifanya hivyo kwa kupulizia dawa kwenye lifti wakati wachezaji wa Stars
wakishuka kwenda kwenye mechi. Watu wakashituka, wachezaji wakatumia ngazi
kushuka chini.
Uwanjani:
Waarabu hao wameshinda makombe zaidi ya
10, kama utachukua ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Washindi na Kombe la
Shirikisho. Hakuna ubishi wana mbinu zote.
Lazima Yanga wawe makini kwa kila hatua,
wanaposhambulia na wanaposhambuliwa kwa kuwa Ahly wanajua wanafanya nini kila
wanapokuwa na mpira au hawana.
Kupoza:
Wana tabia ya kupoza mpira, hasa
wanapokuwa wakicheza ugenini. Halafu wanafanya mashambulizi ya kushitukiza,
wakikufunga, wanarudi nyuma.
Faulo:
Wana sehemu zao wanazotaka kufanyiwa
madhambi, wanalazimisha kuguswa hasa wanapokuwa nje ya 18. Wakipata faulo eneo
hilo, hasa kwenye kona ya msitari wa 18, wana watu maalum kwa ajili ya kazi
hiyo, hivyo lazima Yanga wawe makini.
Aboutrika:
Mohammed Aboutrika amestaafu akiwa na
miaka 34, ingawa umri wake ulikuwa umekwenda, lakini ukweli ni ahueni kwa
Yanga.
Ufundi wake ulikuwa wa juu, mechi mbili
za fainali za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Orlando Pirates, zote mbili alifunga.
Alianza kufunga bao nchini Afrika Kusini wakati walipopata sare ya 1-1.
Waliporejea Cairo, wakashinda kwa mabao 2-0, yeye akiwa ametupia la kwanza.
Ameamua kustaafu, lakini kuna wengine
kama Gedo na Emad Motaeb anayevaa jezi namba 9, bado wanatakiwa kuchungwa sana.
Zote hizo ni mbinu za ushindi, lakini
ukifuatilia zinaendana na umakini wa nini cha kufanya. Kama wawakilishi hao wa
Tanzania wakiweza kushinda Dar es Salaam, kitu ambacho kinawezekana kama wakiwa
makini kweli basi lazima wajipange nje na ndani ya uwanja, maana Waarabu hao
wako makini sana.
0 COMMENTS:
Post a Comment