Na Saleh Ally
YANGA ina kila sababu ya kusema sasa
inatakiwa kuwa katikati ya maandalizi ya kutosha dhidi ya mabingwa wa Afrika,
Al Ahly ya Misri kwa kuwa si timu ya mzaha.
Mechi yao itakuwa Jumamosi, Machi 8,
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kurudiana ni jijini Cairo siku
chache baadaye, hakuna haja ya kuficha mambo kwa madai ya kutaka kuwapa Yanga
moyo, badala yake ukweli ni huu, haitakuwa mechi lelemama.
Wakati Yanga inakwenda kumalizia
mchezo wake dhidi ya timu dhaifu ya Komorozine ya Comoro, Jangwani wataanza
rasmi Ligi ya Mabingwa Afrika watakapokutana na wababe hao wa Afrika, ambao
usipokuwa makini, utawadharau kwa mengi, lakini si kwamba hawafungiki.
Al Ahly wameonyesha hawafanyi utani
katika suala la ushindi, angalia pamoja na kwamba Yanga inaweza isiwe timu
tishio kwao kwa maana ya uzoefu au mafanikio katika michuano hiyo ya Afrika
lakini wameshaanza kutuma watu kufuatilia mwenendo wa Yanga na huenda wanafanya
zaidi ya hapo. Hadi sasa hatujui, lakini inawezekana wanafuatilia mambo mengine
kwa kuwa kweli wanataka kuvuka na kusonga mbele.
Wakati Yanga ina takribani mwezi
mzima kabla ya kuwavaa wababe hao wa Afrika, burudani katika soka
zitakapokutana timu hizo ni suala la umri na uzoefu baina ya wachezaji wa Yanga
na wale wa Al Ahly.
Moja ya sifa kuu ya Al Ahly ni kuwa
na wachezaji wenye umri mkubwa lakini wanaoendelea kuitumikia na kufanya
vizuri, kwani hakuna aliyetarajia kama wangeweza kubeba ubingwa wa Afrika wakiwa
na lundo la “watu wazima”.
Idadi kubwa ya wachezaji wake nyota
ni wale wanaozidi umri wa miaka 30, lakini bado wako fiti na wamekuwa
wakiendelea kufanya vizuri katika anga za kimataifa na tishio katika soka la
Afrika. Hesabu zinaonyesha zaidi ya wachezaji 12 wa Al Ahly wanazidi miaka 30.
Mwaka 2006, Mohamed Barakat alikuwa
kati ya wachezaji wa timu ya taifa ya Misri iliyotwaa ubingwa wa Afrika kwa
kuifunga Ivory Coast jijini Cairo, lakini bado ameendelea kuichezea timu yake
ya Al Ahly hadi leo na sasa ana umri wa miaka 37.
Jaribu kupata picha, Barakat akiwa anachuana
na David Luhende wa Yanga mwenye miaka 22 na akafanikiwa kumshinda, tofauti yao
ni miaka 15. Lakini leo wanapambana na huenda Barakat akaonekana ni bora.
Kuna nyota mwingine, Mohamed
Aboutrika, umri wake ni miaka 35, lakini ndiye atakuwa akipambana na Frank
Domayo ambaye atakuwa akitofautiana naye kiumri kwa zaidi ya miaka 13,
inaonyesha kuna jambo la kujifunza.
Kwamba wachezaji wa Al Ahly
wanajitunza na kuthamini kazi yao, ndiyo maana wanaweza kudumu kwa kipindi
kirefu wakiendelea kufanya vizuri huku wakiwashangaza wengi barani Afrika na
duniani kote.
Wakati mwingine hata wachezaji
kutoka Bara la Ulaya wameshindwa kudumu katika soka kwa muda mrefu kama ilivyo
kwa wachezaji wa Misri ambao wanasifika kwa kuwa makini kwa kazi yao, na
inaelezwa kutoendekeza starehe kupita kiasi hasa uzinzi na ulevi kupindukia,
kunawasaidia kudumu kwa kipindi kirefu.
Kweli mwenendo wa Al Ahly si mzuri
katika Ligi Kuu ya Misri, hata mechi ya mwisho imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya
Al Ittihad lakini iko katika nafasi ya pili, unaweza kusema haifanyi vibaya
maana hata Yanga iko katika nafasi ya pili kwenye msimamo hapa nyumbani.
Mara ya mwisho Yanga kucheza na Al
Ahly ilikuwa mwaka 2008 kwenye Uwanja huo wa Taifa jijini Dar na wachezaji
waliokuwepo na kucheza wakati huo na wapo hadi sasa katika kikosi cha Yanga ni
Juma Kaseja, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Idd ‘Chuji’, Mrisho Ngassa na
Jerry Tegete.
Al Ahly ilishinda kwa bao 1-0
lililofungwa na mshambuliaji Mreno, Flavio aliyepata pasi ya Aboutrika. Kwa
upande wa Yanga, Kaseja alikuwa langoni, Cannavaro, Ngassa na Chuji walimaliza
dakika 90, Tegete aliingia kuchukua nafasi ya Boniface Ambani ambaye siku hiyo
soka lilimkataa.
Kama Yanga ni watano tu waliokuwepo
kipindi hicho, Al Ahly wanarudi na takribani wachezaji 10 waliokuwa katika
kikosi kilichoing’oa Yanga. Maana yake ni watu wanaoelewana, wanaopanga
kinachoeleweka na pamoja na umri wao, bado watatoa upinzani.
Changamoto zote ni sehemu ya Yanga
kuangalia namna ya kujipanga, jamaa wana uwezo lakini Yanga ina timu nzuri na
inaweza kufanya vema hasa kama watajiamini kuwang’oa inawezekana, lakini isiwe
kwa maneno tu.
MSIMAMO MISRI
P Pts
Al Mokawloon 8 16
Al Ahly 8 16
Smouha 7 16
Al Ittihad 8 12
Misr Lel Makasa 8 11
MSIMAMO TANZANIA BARA
P Pts
Azam 16 36
Yanga 16 35
Mbeya 17 34
Simba 17 31
Coastal 17 22










0 COMMENTS:
Post a Comment