February 14, 2014


Straika wa Simba, Amissi Tambwe amewajia juu wanaosema kuwa Mbeya City ni timu ngumu inayosumbua vigogo kwenye Ligi Kuu Bara ambapo amedai kuwa hiyo ni timu ya kawaida na kuahidi kushinda kesho Jumamosi dhidi ya timu hiyo ya Mbeya.


Tambwe, raia wa Burundi, amesema timu za Tanzania zinalingana viwango, ndiyo maana hata wao walifungwa 1-0 na Mgambo JKT ambao wapo mkiani kwenye msimamo.

“Hakuna timu ambayo inamzidi mwenzake kwa kiwango kikubwa kwenye hii ligi, zote zinalingana, ndiyo maana zinapishana kwa pointi chache kwenye msimamo, wanaosema Mbeya City ni ngumu si kweli, isipokuwa wanajitahidi kupata tu matokeo bora.

“Unaposema ni timu ngumu au ni kiboko ya vigogo unakosea kwa sababu ukiangalia kiwango chao ni kama cha timu nyingine tu hapa Tanzania isipokuwa huwa wana kombinesheni,” alisema Tambwe na kuongeza:

“Nimepanga nijitahidi kufunga ili kuisaidia timu yangu ishinde lakini najua kila mmoja atakuwa ananiangalia mimi siku hiyo ili nisifunge, wakumbuke kwamba sipo peke yangu uwanjani.”

Kwenye mchezo wa timu hizo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar zilitoka sare ya mabao 2-2.

Mbeya City imefungwa mechi moja katika mechi zote 17 ikiwa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo huku Simba ikiwa na rekodi ya kupoteza michezo miwili msimu huu na ipo nafasi ya nne katika msimamo.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic