Na Saleh
Ally
MWENDO wa kocha
Jose Mourinho ulianza taratibu sana huku ikionekana kama vile ’amebugi’ kwa
vile Ligi Kuu England ni ngumu zaidi, tofauti na wakati alipokuwepo.
Kadiri siku
zinavyosonga mbele, kikosi chake kimekuwa kikiimarika na hakuna ubishi ndani ya
mwezi mmoja tu, kimeishachukua nafasi inayoonyesha kuwa wana nafasi ya kubeba
ubingwa wa England msimu huu.
Mourinho
anaonekana ana nafasi ya kutwaa ubingwa kutokana na namna kikosi chake kinavyozidi
kuonekana tishio lakini sifa nyingine ni ukubwa wa kikosi.
Chelsea na
Manchester City ndizo timu zisizoweza kuyumbishwa na majeruhi kwa kuwa zina rundo
la wachezaji mahiri na wengi kwenye safu
zote, yaani beki, kiungo na ushambuliaji.
Mfano,
Arsenal au Liverpool, ikitokea wachezaji wawili tu wa kikosi cha kwanza
wameumia, basi tatizo litakuwa kubwa maradufu kuliko inavyoweza kuwa kwa timu
hizo mbili.
Hesabu za
Mourinho kutoka Ureno zimekuwa tofauti na makocha wengi, amekuwa akijitahidi
kujenga uwezo mkubwa wa kipumzi hata kabla ya kuanza mashindano.
Mfano,
alikuwa akisajili kikosi kikubwa, hali iliyowashangaza wengi kwa kuwa waliona
ni kama matumizi mabaya ya fedha.
Lakini faida yake inaanza kuonekana katika
hatua za mwisho.
Mourinho
kama ameingia katika mbio za kuwania ubingwa, hakuna ubishi atakuwa msumbufu
kwa kuwa pamoja na uwezo mkubwa kimbinu, ana kikosi kipana na anaweza
kubadilisha nusu yake kikafanya vizuri.
Upande wa
kikosi, mfano kwa mabeki na viungo wakabaji kuna nyota kama John Terry, Garry
Cahill, Branislav Ivanovic, Ashley Cole, Cesar Azpilicueta, David Luiz,
Ramirez, Mikel Obi, Nemanja Matic na wengine, anakuwa na uhakika hata wa mechi
kumi mfululizo. Kiungo ndiyo amejaza watu lukuki kama akina Eden Hazard, Oscar,
Willian na Frank Lampard.
Lakini
angalia washambuliaji, Mohammed Salah, Samuel Eto’o, Demba Ba, Fernando Torres,
Andre Schurrle na baadhi ya chipukizi.
Ratiba ya mechi
za mwisho kwa Chelsea ni dhidi ya West Brom, Man City (Kombe la FA), Everton,
Galatasaray (Ligi ya Mabingwa), Fulham halafu Tottenham. Kwa kikosi chake
hakutakuwa na usumbufu mkubwa.
Kwa mfumo Mourinho
amekuwa kimya lakini ameibukia katika kipindi mbio zinaenda ukingoni, wakati
wanashtuka kuwa ni hatari, tayari amepanga jeshi lake vizuri na ameshakuwa
msumbufu.
Tayari
Mourinho na kikosi cha Chelsea wanaonekana ni washindani hatari na wenye nafasi
ya kutwaa ubingwa. Lakini mambo mengi Mourinho aliyafanya akionekana kama
anakosea au ameshindwa na ugumu wa Premiership msimu huu, lakini sasa mambo ni
tofauti kabisa.
Man City ya
Manuel Pellegrini hawana tofauti kubwa na Chelsea, angalau wana kikosi chenye
wachezaji wengi wenye uwezo na wanaweza kutoa msaada hadi mwisho wa ligi.
Arsenal si
dhaifu, lakini haina kikosi kipana chenye wachezaji wengi wazoefu, pia angalia
ratiba yao, ni hatari na vigumu kwao kupambana nayo hadi mwisho. Na kama
Arsenal watafeli, hali kadhalika Liverpool, basi ubingwa utakwenda kwa timu
kati ya Chelsea au Man City ambazo zinavaa jezi za bluu.
Angalia
ratiba inavyoiangusha Arsenal na kuitupa kwenye wakati mgumu sana; keshokutwa
Jumatano, inakutana na Manchester United, kweli itakuwa nyumbani Emirates
lakini kumbuka inatokea katika majeruhi ya kupigwa mabao 5-1 na ndiyo gumzo
sasa katika soka England na duniani kote.
Mara tu
baada ya mechi hiyo, Arsenal haitakuwa na muda wa kutosha kupumzika kwa kuwa
siku tano baadaye inakutana na Liverpool katika mechi ya Kombe la FA, hii ni
mechi kubwa.
Siku tatu
baada ya mechi hiyo, Arsenal watacheza tena Emirates dhidi ya mabingwa wa
Ulaya, Bayern Munich ambayo ndiyo inaaminika kuwa na kikosi bora zaidi barani
humo kwa kipindi hiki.
Arsenal
watamaliza Februari kwa kucheza na Sunderland tarehe 22, baada ya hapo Machi
Mosi ndiyo watakuwa wanarejea dimbani kuwavaa wabishi Stoke City. Machi 8
wanaivaa Swansea na mwezi huohuo tena wanacheza na Bayern Munich mechi ya pili,
safari hii wakiwa Ujerumani.
Achana na
ugumu wa mechi hizo ngumu na mfululizo, Arsenal katika mwezi huohuo wana mechi
nyingine ngumu Machi 16 dhidi ya Tottenham na Machi 22 dhidi ya Chelsea. Halafu
watafunga mwezi na mechi dhidi ya Man City.
Ratiba hii
si rahisi kwa Wenger, maana yake inatoa nafasi kwa Chelsea na Manchester City
kuwa na nafasi na kutwaa ubingwa.
Liverpool wenyewe nao mambo siyo rahisi sana
kwani itacheza na Fulham, Arsenal, Swansea, Man United na Cardiff katika mechi
zinazofuata.
City ya
Pellegrini, nayo haina ratiba ngumu ya kutisha mwishoni ambayo itacheza na
Sunderland, Chelsea, Barcelona (Ligi ya Mabingwa), Stoke, Sunderland, Aston
Villa, Barcelona tena, halafu Hull City.
Mpira una
mambo mengi sana yanayoshangaza, yasiyoaminika na yanayoshtukiza, ndiyo maana
hakuna anayeweza kujiamini.
Ingawa timu
zenye rangi ya bluu zinapewa nafasi kubwa kutokana na hali halisi, lakini mambo
yanaweza kugeuka ikitokea upande mmoja ukazubaa au kulala.










0 COMMENTS:
Post a Comment