February 24, 2014


Na Saleh Ally
WAYNE Rooney amekuwa mchezaji wa sita wa Manchester United kufikisha mechi 300 za Ligi Kuu England, akiwa na timu hiyo.

Lakini rekodi hiyo si gumzo sana kama ile ya mkataba wake mpya ambayo unakwenda hadi 2019, kwani amesaini mkataba wa miaka mitano na nusu na atakuwa akilipwa pauni 300,000 (zaidi ya Sh milioni 750) kwa wiki.


Kwa Ulaya, mjadala mkubwa umekuwa ni sababu zipi Manchester United imekubali kulipa fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya Rooney, maarufu kama Wazza wakati hakuwa na kiwango kizuri msimu uliopita hadi ikaelezwa alikuwa na mpango wa kwenda Chelsea.

Kiwango hicho cha juu kabisa duniani ni gumzo, lakini inaonekana Manchester walikuwa na kila sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa hawapo katika hali nzuri na usingekuwa wakati mzuri kumpoteza Rooney.

Dalili zinaonyesha wako katika wakati mgumu na huenda miezi minne ijayo watakuwa katika foleni wakisubiri ratiba ya michuano ya Europa League badala ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kumpoteza Rooney ni sawa na kupotea njia mara mbili.

Lakini ndani ya mkataba huo, inaonyesha Manchester United itaendelea kubaki na haki za mauzo ya picha ya Rooney, kitu ambacho kitaisaidia kuingiza mamilioni ya pauni na kuisaidia kuweza kumlipa Rooney kiwango hicho bila ya kutetereka.

Kwa kifupi, pamoja na kiwango, lakini Manchester katika wakati mgumu kama huu, ilikuwa inahitaji jina la mtu kama Rooney kuendelea kuonyesha iko imara, ina uwezo kifedha na ina wachezaji nyota na wenye majina makubwa.

Yote hayo yatabaki kuwa kati ya Rooney na Manchester United, lakini malipo ya juu kama hayo ya Rooney au yale ya Cristiano Ronaldo na Real Madrid au manunuzi ya Gareth Bale ya pauni milioni 86 kutoka Tottenham kwenda Real Madrid, yanaonyesha soka ni biashara kubwa sana hapa duniani.

Mshahara wa pauni 300,000 kwa wiki, nani atalipwa? Hata awe profesa wa chuo kikuu maarufu kuliko vyote duniani, haitawezekana, lakini Rooney anapata kwa wiki.

Fedha anazolipwa kwa wiki, huenda zina nafasi ya kutatua matatizo makubwa zaidi ya Yanga na Simba kwa muda mrefu na wakayasahau milele.

Mfano sasa zimekuwa katika mchanganuo wa mambo mengi sana, kwamba klabu zina mipango ya kisasa na zinataka kubadilika. Yanga na Simba ndizo timu kongwe zinazotia aibu kuliko zote kwa kipindi kirefu.

Hazina hata uwanja wa mazoezi, zinafanya mazoezi kwa kukodi. Hazina tofauti na wakazi wengi wa Dar es Salaam ambao maisha yao ni kupanga. Angalau wao wanaweza kusema ugumu wa maisha, lakini Yanga, Simba zina uwezo wa kuingiza fedha na kucheza viwanja angalau vya mazoezi.

Gharama zinaonyesha hivi, uwanja hasa wa nyasi bandia unaweza usizidi Sh milioni 150. Maana yake Yanga na Simba zinahitaji angalau Sh milioni 300 tu kwa zote mbili, kumaliza milele matatizo ya kutokuwa na viwanja hata vya mazoezi tu.

Mshahara wa wiki wa Rooney unaweza kuwajengea uwanja wa mazoezi Yanga na ndugu zao Simba. Lakini jiulize, kwa nini fedha za kwenye soka ifikie upande mmoja fedha ya wiki inaweza kutatua matatizo ya milele kwa upande mwingine?

Ukweli ni kwamba wapo wanaouchukulia mchezo wa soka ni biashara kubwa ambayo si ya kuifanyia mzaha, ndiyo maana kuna wachezaji wanaoweza kulipwa fedha za kufuru kama Rooney na Ronaldo au wanaweza kununuliwa kwa vitita vikubwa kama Bale.

Hapa nyumbani, hakuna wanaoona hivyo na kama wapo ni wachache na wamekuwa wakikatishwa tamaa na wengi ambao ni wagumu kuelewa na bado wanaamini Yanga na Simba ni kwa ajili ya kuburudisha mioyo tu pale zinaposhinda.

Hakuna atakayekataa kama Yanga na Simba zinafanya biashara ya soka, lakini haziko makini. Ndiyo maana mambo yamekuwa ya kubahatisha zaidi.

Kutokuwa na uwanja hata wa mazoezi ni sehemu ya kuonyesha kiasi gani timu hizo haziko makini au si zilizopania kupata mafanikio kiutendaji na badala yake kushinda pekee ndiyo kunabaki kuwa mafanikio A na Z.

Hakuna kiongozi wa Man United anayeweza kutoa hata senti yake mfukoni kumlipa Rooney. Fedha zote zinatokea kwenye mfereji wa mipango ambao unatokana na umakini wa klabu hizo. Kweli huko ni England, sawa. Lakini hapa basi Yanga na Simba zifikie hata robo ya hapo!

Angalau kupitia njia ileile ya kuuza jezi, kuyashawishi makampuni makubwa kuidhamini, kusajili timu bora inayofanya vizuri ili kuvuta watu wengi uwanjani. Pia kusaini mikataba ya uhakika ya haki za runinga. Basi, fedha za kuwalipa wachezaji, kujenga viwanja na maendeleo mengine, haziwezi kuwa vikwazo.

Viongozi wa Yanga, Simba zenye utajiri wa watu wanaosubiri kununua au kulipia chochote kutoka katika klabu hizo lakini hawakipati, wasishangilie fedha za Rooney kama gumzo la vijiwe vya kahawa. Badala yake ziwaumize na waanze kutafakari angalau kwa tundu dogo tu, walitumie kama njia ya kutokea walipokwama miaka nenda rudi.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic