Bekiwa zamani wa Yanga, Stephano Mwasyika,
anayechezea Ruvu Shooting kwa sasa amesema mabao ya haraka yaliwatoa mchezoni
na kujikuta wakipokea kipigo kikubwa cha mabao 7-0 kutoka kwa Yanga.
Ruvu walikula kichapo hicho kwenye
mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam, Jumamosi iliyopita.
Ruvu ilijikuta ikifungwa bao la kwanza
sekunde 58 ya mchezo kipindi cha kwanza, bao lililofungwa na Didier Kavumbagu huku bao la pili
likifungwa dakika 2 na winga Simon Msuva.
Mwasyika
amesema kuwa licha ya kufanya maandalizi hawakutarajia kufungwa mabao ya mapema kiasi
kile kutokana na uzuri wa timu yao.
“Yale mabao tuliyofungwa mwanzoni ndiyo
yalitutoa mchezoni, hatukutegemea kabisa kuruhusu mabao yale ila wapinzani
walitumia udhaifu wetu uliojitokeza na kuweza kutufunga, malengo yalikuwa
kushinda mchezo ule (Jumamosi).
“Tulijaribu kujipanga lakini
ilishindikana, wenzetu walionekana wakitumia mipira mirefu ambayo wameweza
kuimudu vema kuliko sisi ila tunaenda kujipanga na mchezo unaofuata tusipoteze kama huu,” alisema Mwasyika.
0 COMMENTS:
Post a Comment