Na Boniface Wambura, Lusaka
Twiga Stars imepoteza mechi ya kwanza
ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake
(AWC) baada ya leo kufungwa mabao 2-1 na Zambia (Shepolopolo) kwenye Uwanja wa
Nkoloma jijini hapa.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika
katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Salma Mukansanga timu hizo zilikuwa
suluhu.
Wenyeji ndiyo walianza kupata bao
lililofungwa na Hellen Mubanga dakika ya 75. Mfungaji huyo aliyeingia kipindi
cha pili nchini alimalizia wavuni mpira uliotemwa na kipa Fatuma Omari.
Dakika nne baadaye Zambia ambao
walikuwa wakishangiliwa kwa nguvu na washabiki wao baada ya kufunga la kwanza,
walipata bao la pili ambalo nahodha wa Twiga Stars, Sophia Mwasikili alijifunga
mwenyewe.
Mwasikili alikuwa akijaribu kutoa nje
mpira uliopigwa na nahodha wa Shepolopolo, Mupopo Kabange ambapo ulipishana na
kipa Fatuma Omari kabla ya kujaa wavuni.
Bao la Twiga Stars lilifungwa na
Donisia Daniel dakika ya 90. Beki huyo wa kushoto ambaye pia ni mchezaji wa
Tanzanite alipanda mbele kuongeza mashambulizi ambapo akiwa nje ya eneo la
hatari alipiga shuti lililomshinda kipa Hazel Nali.
Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa
Twiga Stars, Rogasian Kaijage alisema amebaini upungufu katika kikosi chake ambao
ataufanyia kazi kabla ya mechi ya marudiano ili timu yake iweze kusonga mbele.
“Kwa matokeo haya bado tuna nafasi ya
kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano nyumbani na kusonga mbele,” alisema
Kaijage.
Twiga Stars iliwakilishwa na Fatuma
Omari, Fatuma Bashiru, Donisia Daniel, Fatuma Issa, Evelyn Sekikubo, Sophia
Mwasikili, Vumilia Maarifa, Mwapewa Mtumwa/Amina Ali, Asha Rashid, Etoe
Mlenzi/Zena Khamis na Shelida Boniface.
Timu hiyo inarejea nyumbani kesho kwa
ndege ya Fastjet ambapo itatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana.








0 COMMENTS:
Post a Comment