March 1, 2014



KATIKA soka la Afrika Mashariki, kuna mambo mengi sana yanafanana ndiyo maana timu nyingi za Kenya, Tanzania, Uganda na hata Burundi na Rwanda zina mchezo unaofanana kwa asilimia kubwa.

Lakini kila timu hizo zinapokutana na timu za Waarabu zimekuwa katika wakati mgumu sana na kutolewa mapema kwenye mashindano, hali ambayo sasa imekuwa inaonekana ni kama kawaida tu.
Safari hii Yanga inakutana na Al Ahly ya Misri, kwa sasa ndiyo timu bora Afrika kwa maana ya takwimu, hali hiyo inaweza kuwapa hofu kubwa Yanga na wakaamini kuwa hawawezi kuwatoa Waarabu hao, si kweli, wanawezekana kufungwa na wanaweza kutolewa.
Mpira una mbinu nyingi sana na ukiangalia katika kipindi cha sasa, Yanga ina uwezo wa kuitoa Al Ahl, nitatoa sababu. Kama ni kwa maandalizi, kwa timu za Afrika Mashariki, Yanga ndiyo iliyofanya maandalizi makubwa kuliko timu nyingine.
Imekwenda kuweka kambi nchini Uturuki kwa ajili ya maandalizi, kama kweli maandalizi ya Uturuki yamekwenda vizuri na Yanga imekuwa ikiibuka na matokeo mazuri. Kwa nini isifanye vizuri dhidi ya Al Ahly.

Siku zote maandalizi ni kitu cha kwanza, hilo Yanga wameishalivuka na sasa linafuatia suala la mechi yenyewe kuwa wataicheza vipi. Fanya umejiandaa vizuri, lakini ukashindwa kucheza vizuri basi mara moja tu unatolewa.
Kuna mambo matatu muhimu ambayo Yanga wanatakiwa kuyafanya ili kushinda mchezo wa Jumamosi dhidi ya Waarabu hao wa Misri. Moja ni maandalizi mazuri, hilo wamefanya, pili ni good concentration (umakini) na determination (kujituma).
Kuwa makini maana yake ni kutimiza kila ulichokipanga kwenye mazoezi, mfano plani mlioyonayo kwa ajili ya mchezo husika. Mnaweza mkawa mmejiandaa vizuri lakini kama mtashindwa kuwa na good concentration, maana yake hakuna mtakachofanya kufikia mafanikio.
Lakini mkiwa na good preparation (maandalizi mazuri), pia good concentration, bado utaona vitu hivi vinategemeana.  Lazima pia muwe na determination ambayo sasa mwisho itabeba vipengele vyote viwili vya mwanzo.
Kama haujitumi hata ukiwa na akili unaweza kufeli darasani, ndivyo ilivyo mpirani. Kama haujitumi, hata kama uko fiti, mwisho utafeli, hilo halina ujanja.
Nakumbuka wakati nikiwa Kocha wa Tusker (ya Kenya), tukiwa mabingwa tulipangiwa kucheza na Al Ahly, kama sijakosea ilikuwa kati ya mwaka 2001 au 2002. Mechi ya kwanza ilikuwa ni mjini Cairo na tulipoteza kwa kufungwa kwa mabao 3-1.
Mechi iliyofuatia nilijua lazima nitawatoa tukiwa Kenya, kwa kuwa nilitakiwa kushinda mabao 2-0 tu. Kwa uchezaji wao wanapokuwa ugenini, wanabaki nyuma na kukusubiri uje, lakini ukienda kijinga wanapiga counter attack (shambulizi la kushitukiza), wanakufunga halafu wanarudi nyuma kulinda.
Nilijua mchezo wao huo na nikaandaa mtego, tuliwazidia sana karibu dakika zote 90 na tulifanikiwa kuwafunga bao 1-0 ambalo lilidumu hadi mwisho wa dakika 90. Kweli tukawa tumeshinda nyumbani lakini tukatoka.
Hii inaonyesha hata Yanga wakiwa wamejipanga vizuri, wana uwezo wa kuwafunga na kizuri zaidi kwao kwa kuwa mchezo wa kwanza wanaanzia nyumbani basi ndiyo kipindi cha kutengeneza akiba ya baadaye. Washinde zaidi ya mabao mawili, itakuwa ahueni kwao.
Sasa dunia nzima mpira uko hivi, anayecheza ugenini mara nyingi anabaki kwake na kusubiri mwenyeji akashambulie sana kwa kuwa yuko nyumbani anakuwa na papara. Hivyo kubaki kwenye zone yako, maana yake mnapunguza uwanja.
Hivyo Al Ahly wanaweza kuanza kwa kushambulia kujaribu kama watapata bao, lakini wakiona Yanga ni wakali, watabaki nyuma muda mwingi, wataupoza mpira ili mradi tu watoke sare au wakipoteza iwe idadi ndogo lakini wakipata nafasi, hawaichezei watafunga na iwe shida zaidi kwa Yanga katika mechi ijayo.
Nawatakia kila la kheri kwa maana ya Tanzania iko Afrika Mashariki, Al Ahly wanafungika lakini lazima kazi iwe ya uhakika.
Mulee ni kocha wa zamani wa Tusker na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars. Sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic