March 1, 2014


YANGA imevunja mwisho wa kuonewa kila wanapokutana na Al Ahly kwa kuikaanga kwa bao 1-0.

Bao holo limefungwa na beki, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye ameingia kwenye rekodi ya wachezaji Watanzania waliowahi kutikisa nyavu za Warabu hao noma


Kabla yake, hakukuwa na Mtanzania aliyekuwa amewahi kufunga bao ambalo lilimaliza Ahly hapa Tanzania, isipokuwa mshambuliaji wa Simba, Mtemi Ramadhani.
Mwaka 1985 ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa timu ya Al Ahly ya Misri kupoteza mchezo wake katika ardhi ya Tanzania, ilichapwa mabao 2-1 na Simba.
Baada ya hapo imewahi kucheza mechi kadhaa na Yanga, lakini ilikuwa ni sare au wao kushinda na walipokwenda Cairo, basi walitoa adhabu kwa timu za Tanzania wakati mwingine kali.

Mechi hiyo ya mwisho Al Ahly kufungwa na Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, imebaki kuwa ndiyo rekodi pekee ya Warabu hao kunyanyasika.
Baadaye mwaka 2003, wapinzani wao Zamalek nao wakakiona kwa Simba baada ya kuchapwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam, wakashinda bao 1-0 jijini Cairo lakini Simba wakawatoa kwa mikwaju ya penalti.
Zamoyoni Mogella na Mtemi Ramadhani ndiyo wenye rekodi ya kufunga mabao mawili ya mwisho yaliyoimaliza Al Ahly.
Mtemi wakati huo alikuwa ndiye nahodha wa Simba, alifunga bao hilo la pili baada ya kupokea pasi ya Mogella ambaye alikuwa tayari amefunga la kwanza.
“Nilipokea mpira kwa mguu wa kulia, nikaushuka na kufunga kwa shuti la mguu wa kushoto, lilikuwa bao zuri tu,” anasema Mtemi.
Kabla ya mechi ya leo Yanga v Ahly, alisema haya:
 “Kufungwa inawezekana, tatizo vijana wetu hawapendi mazoezi. Wanaona kama adhabu na kitu kibaya zaidi makocha wazungu wanawachukulia hawa kama professional sana, kumbe ni matatizo.
“Wanafanya mazoezi mara moja kwa siku, tena mazoezi mepesi kabisa. Si sahihi na hilo ni tatizo kubwa sana, kwenye mpira lazima uwe na mazoezi ya kutosha.
“Angalia Mbeya City, wala hauwezi kusema wanajua kupita wote. Lakini mazoezi yao kuwa makali na ya kutosha, basi mambo yao yanakwenda vizuri tu.
“Mazoezi ya siku moja kwa siku hayatoshi, pia wachezaji lazima wajubali kwamba mazoezi ni muhimu na lazima wafanye ya kutosha ili waweze kufanya vizuri,” anasema Mtemi.
“Ukiipigia mahesabu Yanga ya sasa, kwenye karatasi, kweli ni timu nzuri sana. Lakini mazoezi wanayopata yakiwa hayatoshi, basi hawawezi kufanya lolote la maana.
“Pia ni lazima wajitume ili kupambana na Waarabu ambao wanafanya mazoezi makali, wanakula vizuri na ni professional kweli kwa kuwa wanajua namna ya kujiweka na kujitunza,” anasema Mtemi ambaye sasa ni kati ya wachezaji wakongwe waliokuwa ‘noma’ wakati wa enzi zao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic