MIMI nianze na kusema kuwa lazima
tukubali kuwa wenzetu Waarabu wamekamilika katika suala la mpira, ukianzia
maandalizi na hata mipango, wako makini kweli kama ukiwalinganisha na sisi.
Mwaka 1985, ilibaki kidogo sana tuweke
rekodi ya kuwatoa Al Ahly katika michuano ya kimataifa, lakini tukafeli kidogo
sana kwa uzembe wa viongozi wetu.
Mjini Mwanza tuliwafunga mabao 2-1, mimi
nikianza kufunga la kwanza, halafu nikatoa pasi na nahodha wangu, Mtemi Ramadhani
akafunga bao la pili lililowamaliza. Baada ya mechi hiyo wachezaji tukaomba
kuweka kambi jijini Mwanza, lakini haikuwa hivyo.
Viongozi wakasisitiza turudi Dar es
Salaam, lakini wiki nzima, kambi haikuwekwa na ilikuwa vigumu kuwaona. Hata
siku tulipofika Cairo, Misri tukalazimika kufanya mazoezi usiku na kesho yake
tukafungwa mabao 2-0, tena kwa taabu sana. Wao wakasonga mbele.
Kwa wachezaji wa kipindi kile, kweli
tulikuwa tunajituma sana na tuliona sifa kupata mafanikio, lakini hatukupenda
hata kidogo kuwaangusha mashabiki wetu, kitu ambacho wachezaji wa Yanga
wanapaswa kufanya Jumamosi (leo).
Nimesikia kuna ahadi wamepewa, hilo ni
jambo zuri lakini wasipokuwa makini itakuwa ni kazi bure ndiyo maana
ninasisitiza kuwa lazima wawafikirie mashabiki watakaojitokeza kwa wingi
uwanjani siku hiyo kwamba hataki kushinda na wakijituma wana uwezo wa kushinda.
Sisi tulitolewa kwa uzembe wa viongozi
wetu, wao viongozi wao wanajitahidi ikiwa ni pamoja na kuwapa kambi nzuri,
maandalizi mazuri pamoja na ahadi. Hivyo wana kila sababu ya kufanya vizuri.
Lakini kitu cha muhimu lazima wasisahau
kwamba jamaa wamekamilika kama nilivyosema awali, watuelie na waonyeshe wako
nyumbani. Maana wachezaji wa siku hivi wakiona uwanja umejaa,
wanachanganyikiwa, wanakuwa waoga.
Waachane na uoga, wawajali mashabiki na
huu ndiyo wakati mzuri kwa wachezaji wa Yanga kusema sasa inatosha, wawafunge
Al Ahly na inawezekana kabisa.
Kama wakisema hivyo, huu ndiyo utakuwa
wakati sahihi wa dunia kuijua Yanga, maana kuitoa Al Ahly ambao ni mabingwa wa
Afrika, timu bora bara hili. Dunia nzima itapata habari hizo, ninasisitiza,
hilo linawezekana.
Inawezekana sisi wadau, au waandishi wa
habari na vyombo vyao kwa ujumla wakaamua kuisifia na kuipamba vilivyo Yanga
kwa lengo la kuipa moyo, lakini wenye uamuzi wa mwisho ni wachezaji wenyewe.
Nidhamu ya mchezo ni jambo la muhimu
sana na wachezaji wetu wengi hawana, limekuwa ni tatizo lao kubwa sana. Wale Al
Ahly wana nidhamu ya juu sana ya mchezo, wanajua nini cha kufanya kwa ajili
kila wanayekwenda kupambana naye.
Mimi wakati nacheza, nilikuwa naucheza
mchezo kabla ya kuingia uwanjani. Nikifumba macho hivi naona nitafanya hivi na
vile, mipango ni mapema na nikiingia uwanjani nihamu ni ya juu. Kingine Yanga
waangalie wasifungwe bao la mapema, maana watateseka sana maana Ahly wakiipata
nafasi hiyo, basi wanajua wafanye nini.
Mogela ni mshambuliaji wa zamani hatari
wa Simba na baadaye Yanga. Ndiye alikuwa mmoja wa wachezaji wawili wa Tanzania
kutikisa nyavu za Al Ahly mwaka 1985 wakati Simba ikiifunga timu hiyo mabao 2-1
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment