MWOMBEKI KAZINI |
Licha ya wachezaji Said Bahanuzi wa
Yanga na Betram Mwombeki wa Simba kuonekana si lolote si chochote katika klabu
zao, benchi la ufundi la Mtibwa Sugar linaloongozwa na Mecky Maxime, limeonyesha
nia ya kuwahitaji wachezaji hao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Bahanuzi alikuwa akiichezea Mtibwa kabla
hajasajiliwa Yanga na sasa timu hiyo ya Morogoro inataka kumrudisha. Mwombeki mwenyewe
alianza kwa mbwembwe Simba lakini ameshindwa kupata nafasi chini ya kocha
Zdravko Logarusic.
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime,
ameliambia gazeti hili kuwa, endapo atafanikiwa kuwapata wachezaji hao, itakuwa
ni jambo zuri kwake kwani ana uhakika kuwa watamfanyia kazi kubwa ambayo itarudisha
heshima ya klabu hiyo.
Alisema Simba ya Yanga kwa sasa
zinawaona wachezaji hao kuwa hawana lolote lakini yeye anaamini kuwa ni miongoni
mwa washambuliaji hatari ambao timu hizo zimeshindwa kujua ni jinsi gani ya
kuwatumia.
“Ligi kuu ya msimu huu ndiyo kwanza
inafikia ukingoni hivi karibuni na baada ya hapo taratibu za usajili zitaanza,
hivyo tutaangalia kama tunaweza kuwasajili.
“Wachezaji hao kwa hakika ni miongoni
mwa washambuliaji bora hapa nchini lakini wamenyimwa nafasi, endapo nikiwapata
nitawatengeza na kuwarudisha katika viwango vyao ambavyo watu wote walikuwa
wakivijua,” alisema Maxime.
Maxime pia amewaonya wachezaji kuwa
makini kufanya maamuzi hasa ya kujiunga Simba au Yanga, kwani mara nyingi
vipaji vyao hupotea kutokana na kushindwa kutumika vizuri kutokana na uhaba wa
nafasi.
0 COMMENTS:
Post a Comment