Soka
inaweza kusaidia mapambano dhidi ya mauaji ya tembo
Tanzania imekuwa katika kampeni kubwa ya kupambana na mauji ya wanyama aina ya tembo
ambao kadiri siku zinavyosonga mbele imekuwa ikionekana kuwa watatoweka.
Tembo
wanauawa kwa kuwa kuna watu wanaingiza mamilioni ye fedha kutokana na kuuza
pembe zao, hii inaonyesha kiasi gani watu wanaweza kuwa wanyama kwa ajili ya
kujali maslahi yao na si ya taifa au uhai wa wanyama hao.
Ubinafsi ni
sehemu ya sifa ya binadamu wengi, nianze kwa kusisitiza hivi; kama kuna mtu
anashiriki katika hilo basi aamini anachofanya si sahihi na hana sababu ya
kuendelea, ambaye alikaribia kuingia kwenye mkumbo huo, aachane nao kwani dili
ziko kibao ambazo si lazima kuua.
Unaweza
kushangaa vipi leo Metodo imehamia huku, lakini lengo ni kuweka msisitizo
kuhusiana na wanyama hao ambao ni urithi wa taifa letu na wanamhusu kila mmoja.
Nchi
nyingine hazina tembo, usijali ziko Afrika au Ulaya. Lakini Tanzania tumepata
bahati hiyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo ni lazima tupambane kuhakikisha
tunalinda uhai wao kutoka kwa majangili ambayo ni miongoni mwetu kama jamii.
Lakini
kingine ambacho kimenivutia ni namna ambavyo wanaopiga kampeni ya kupambana
kuielezea jamii ubaya wa kinachofanyika na kuwataka wananchi kuungana na
serikali kupambana na watu hao.
Wanatumia
njia mbalimbali kama za matangazo na mambo mengi, lakini michezo imesahaulika
na imekuwa ni kawaida kwenye kampeni mbalimbali muhimu.
Michezo ina
nguvu hata kuliko wanasiasa wengi, hivyo inaweza kupewa nafasi ya kuzitangaza
kampeni za kupambana na ujangili na ikiwezekana wanamichezo mbalimbali wakiwemo
wa soka wakapewa nafasi ya kuziongoza kampeni hizo kwa jamii.
Soka
imetumika sehemu mbalimbali kurudisha amani kwenye jamii, mfano Rwanda ambako
baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994. Soka ni sehemu ya njia iliyotumika
kurudisha uelewano na upendo miongoni mwa Wanyarwanda bila ya kujali mmoja ni
Mtutsi, Mtwa au Mhutu.
Si Rwanda
pekee, nchi nyingi duniani wameutumia mchezo wa soka kama sehemu ya
kuwakutanisha na kufanya mambo muhimu kwa ajili ya jamii.
Angalia
Afrika Kusini iliyopata mafanikio katika kupambana na maambukizi ya virusi vya
ukimwi kupitia mchezo wa soka. Hali ilikuwa mbaya, lakini kupitia soka, nafuu
ikawa kubwa.
Jaribu
kuwauliza watu wengi kuhusiana na mshambuliaji wa Yanga au kiungo wa Simba
anaitwaje. Lakini fanya hivyo kama unataka kujua mbunge wa jimbo fulani,
itakuwa kazi kukutamkia.
Hiyo ni
sehemu ya kuonyesha michezo inapewa nafasi kubwa na jamii ya Watanzania na
nguvu yake iko juu. Hivyo wananchi wanaweza kupata somo la kuwarejesha na
kuwakumbusha umuhimu wa kuwalinda tembo hao.
Lakini
inawezekana kuwashawishi majangili hao, kwa kuwa ninaamini lazima watakuwa ni
sehemu ya wanamichezo au wapenda soka, kwamba hata wapenda michezo wenzao
wanapinga. Inawezekana ikawa vigumu kuamini lakini ukweli unabadilisha wengi,
labda wale viburi ambao watakataa makusudi.
Sitaki
kuingilia kampeni hizo ambazo zinaonyesha kuwa kweli Tanzania na nchi nyingine
jirani zimenuia kweli kupambana nao ujangili huo. Lakini lazima muamini, kama ni
kufikisha ujumbe kwenye jamii, soka ina nguvu.
Inawezekana
hamkuwa mmefikiria nilichowakumbusha leo, lakini bado hamjachelewa na pia
ujumbe kwa wengine; msisahau kuwa michezo hasa soka ina nguvu na sauti yake ni
ya juu zaidi kuliko ile ya wanasiasa. Hivyo itumieni.
0 COMMENTS:
Post a Comment