Uongozi wa Azam FC umempa kibarua kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog,
kwenda kusaka wachezaji pindi atakapokuwa mapumziko nchini kwao Cameroon.
Omog alitua Azam wakati wa dirisha dogo la msimu uliomalizika hivi
karibuni baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Stewart Hall
aliyemwachia madaraka baada ya uongozi kuona timu hiyo inayumba.
Hata hivyo, baada ya kukabidhiwa majukumu hayo, Omog ameonekana
kuitumikia vema timu hiyo na hatimaye kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
Bara msimu wa 2013/2014 ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo tangu ipande
daraja.
Katibu Mkuu wa Azam FC, Idrissa Nassoro, amefunguka kuwa, kocha huyo anatarajia
kuondoka nchini leo Ijumaa kuelekea Cameroon kwa ajili ya kwenda mapumziko na
familia yake, lakini akadai kuwa atakapokuwa huko atakuwa na kazi ya kuangalia
wachezaji na iwapo atamuona anayefaa, basi atautaarifu uongozi ili kuweza
kufanyia kazi.
“Kwa sasa kila mtu yupo mapumziko kuanzia kocha, wachezaji hadi
uongozi baada ya kumaliza ligi, tutajiandaa kuhakikisha tunafanya usajili wa
kiwango cha juu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na si ligi kuu pekee.
“Kila mmoja amepewa jukumu lake kuelekea usajili wa msimu ujao lakini
kwa sasa ni mapema mno kuweza kuweka wazi juu ya kinachoendelea, tusubiri
kwanza,” alisema Nassoro.
0 COMMENTS:
Post a Comment