April 25, 2014



Na Saleh Ally
KUMEKUWA na mvutano mkubwa kuhusiana na ligi kuu ipi ni ngumu zaidi barani Ulaya, huku kila upande ukivutia ngoma upande wake.


Kwa kawaida, ugumu ndiyo mvuto wenyewe kwa kuwa ‘nature’ ya watu wa soka wanafurahia kuona upinzani mkali zaidi na takwimu kwa wastani, zinaonyesha Premiership inafanya vizuri zaidi kwa maana ya burudani inayovutia zaidi.

Si rahisi kujua mapema timu gani itakuwa bingwa na hali hiyo ni karibu kila msimu sasa, angalau Manchester United ya Alex Ferguson ilikuwa ikitangulia mapema. Lakini sasa mambo ni tofauti kabisa. Hali hiyo inavutia watazamaji wengi zaidi.

Utaona Italia na Hispania ndiyo kuna viwanja vingi vikubwa ukilinganisha na England, lakini zimeingiza watazamaji wachache zaidi. Ujerumani, wameendelea kuwa na watazamaji wengi zaidi kutoka na ukubwa wa viwanja pia.

Klabu nyingi za England zimeanza kufanya ukarabati wa viwanja vyao, wanaviboresha na kuongeza uwezo wa kuchukua watazamaji na hiyo inatokana na idadi kubwa zaidi ya watu wanaotaka kuingia viwanjani. Hili ni sehemu ya jibu kuwa Premiership ina mvuto zaidi hadi sasa.

Kudorora kwa Man United msimu huu bado hakujaiathiri sana Premiership, huenda kurejea kwa Liverpool kumefanya mambo yawe sawa tu. Lakini kudorora kwa AC Milan, Inter Milan kunazidi kuiporomosha Serie A.

Kwa takribani misimu minne, England imekuwa ikionekana kuwa ni ngumu zaidi ya ligi nyingine ingawa bado Ujerumani na ligi yao ya Bundesliga pia wamekuwa wakisema ligi yao ni ngumu zaidi na ina mvuto kuliko nyingine.

Kimpangilio wa mambo, mfano uandaaji wa mechi, ushabiki na idadi ya watu. Bundesliga kweli iko juu, lakini ukitoka nje ya nchi yao, wanaoifuatilia si wengi kama ilivyo Premiership. Huenda lugha pia ni tatizo.

Hispania, bado pia wanasisitiza La Liga ni kiboko lakini wachambuzi wengi wanaiita ni ligi ya timu mbili ingawa msimu huu, kuimarika kwa Atletico Madrid kunaonekana kubadili mambo kwa kiasi kikubwa.

Italia na ligi yao maarufu kama Serie A, wamekuwa wakiendeleza upinzani kwamba ligi yao ni ngumu na bora. Ingawa takwimu zinaonyesha hali hiyo ilikuwepo misimu zaidi ya saba iliyopita.

Huku ligi zote hizo nne maarufu zikiwa zinaendea ukingoni, ujazo wa takwimu zilizopatikana zimetoa jibu kuwa Premiership ya England ndiyo ligi ngumu zaidi.

PREMIERSHIP:
Mechi: 347, kati ya 380
Ushindi nyumbani:  46.7%
Sare:  21.0% 
Ushindi ugenini:  32.3%    
Mabao: 958 
Bao kwa mechi: 2.76 
Wastani wa watazamaji kwa mechi: 35,405
% ya mabao ya penalti:      7.0%
% ya mabao baada ya dakika ya 80: 16.9%
*Wastani wa mabao ya kufunga baada ya mechi 347 unaonyesha ugumu wa ligi hiyo, lakini asilimia 32.3 za ushindi wa ugenini zinathibitisha kiasi gani Premiership ni nondo ingawa takwimu zinathibitisha kuwa ligi hiyo ina utamu zaidi kwa kuwa mabao yanafungwa zaidi ya ligi nyingine.
Mabao 958 yaliyofungwa, ndiyo mengi zaidi kuliko ligi nyingine zote (La Liga 942, Serie A 913 na Bundesliga ni 883).

BUNDESLIGA:
Mechi 279, kati ya 306
Ushindi nyumbani:  46.6%
Sare:  21.5% 
Ushindi ugenini:  31.9%    
Mabao:  883
Wastani wa mabao kwa mechi:  3.16    
Wastani wa watazamaji kwa mechi:  43,382
% ya mabao ya penalti:  6.7%
% ya mabao baada ya dakika ya 80: 15.7%
*Inaonyesha ni ligi ngumu pia kwa kuwa wastani wa ushindi nyumbani unapishana kwa kiasi kidogo sana na ule wa Premiership, hali kadhalika sare. Lakini Bundesliga inaendelea kutawala kwa kuwa ligi inayoingiza idadi kubwa zaidi ya mashabiki.

LA LIGA:
Mechi: 339, kati ya 380
Ushindi nyumbani:  47.8%
Sare:  21.8% 
Ushindi ugenini:  30.4%    
Mabao:  942
Wastani wa mabao kwa mechi:  2.78    
Wastani wa watazamaji kwa mechi:  26,172
% ya mabao ya penalti:  7.3%
% ya mabao baada ya dakika ya 80: 15.3%
*Wastani wa watazamaji uko chini hii inaonyesha ni mechi chache ambazo huingiza watu wengi zaidi, maana yake mvuto hauko juu. Mvuto wa mechi nyingi, maana yake timu nyingi zinakuwa na uwezo wa juu na kusababisha upinzani zaidi.

SERIE A:
Mechi 340, kati ya 380
Ushindi nyumbani:  46.8%
Sare:       24.1%    
Ushindi ugenini:  29.1%    
Mabao:  913
Bao kwa mechi:  2.69
Wastani wa watazamaji kwa mechi:  19,575
% ya mabao ya penalti : 9.5%
% ya mabao baada ya dakika ya 80: 16.3%
*Idadi ya watazamaji pia iko chini, wastani  uko chini, hiyo ni sehemu ya kuonyesha si mechi nyingi zinazokuwa na mvuto badala yake ni zile zinazohusisha timu chache maarufu kama Juventus, AS Roma. Lakini kudorora kwa AC Milan na Inter kumekuwa tatizo.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic