Mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi, kwa sasa yupo nchini Uganda,
aliondoka juzi Jumatano na kuzungumza na SALEHJEMBE na Gazeti la Championi Ijumaa pekee huku
akiitaja Simba.
Okwi ambaye aligoma kucheza mechi za mwishoni mwa Ligi Kuu Bara, msimu
uliomalizika hivi karibuni kutokana na kile kilichoelezwa kuwa alikuwa
hajamaliziwa malipo ya usajili wake, amefunguka kuwa Simba ndiyo ambayo
imemfanya kuwa vizuri kiuchumi.
Raia huyo wa Uganda ambaye alisajiliwa ‘bure’ Étoile du Sahel ya
Tunisia akitokea Simba, kabla ya baadaye kutua AS Villa ya Uganda na kisha
Yanga, ameishukuru Simba kuwa ndiyo iliyochangia neema nyingi na kumfanya
ajiweke vizuri kiuchumi kwa kuwekeza zaidi nchini kwao Uganda.
Okwi amesema kuwa alipokuwa Simba ni wakati ambapo aliweza kufanya
mambo mengi ya kukuza pato lake ikiwemo kununua magari sita aina ya Fuso kwa
ajili ya biashara, magari mengine binafsi pamoja na nyumba ya kifahari.
“Naipenda sana Tanzania na nina mambo yangu mengi tu huku,” alisema
Okwi muda mfupi kabla ya kuondoka nchini, juzi, aliendelea kufunguka:
“Siyo mshahara pekee wa Simba lakini nilipokuwa pale nilikuwa nikipata
vitu vingi, mfano kuna mwanachama mmoja mwanamke alinipa gari, mashabiki nao
walikuwa wakinipa vitu vingi, nawashukuru sana kwa yote.”
Okwi aliongeza kuwa anarejea Uganda kwa kuwa Ligi Kuu Bara imemalizika
lakini akatoa kauli kuwa atarejea baada ya wiki tatu kwa ajili ya kukamilisha
mambo yake binafsi.
“Kuna vitu fulani nitakuja kuvifanya, siwezi kuvizungumza kwa kuwa ni
vyangu binafsi, lakini nafikiri muda ukifika nitazungumza mengine mengi,
Watanzania watajua, huu siyo wakati sahihi,” alisema Okwi.
Wakati akiondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) jijini Dar, Okwi alisindikizwa na watu wawili waliokuwa wamebeba mabegi
yake, alipofuatwa na mwandishi wa habari (siyo wa Championi) akaweka simu
sikioni na kutotaka kuzungumza chochote.
Lakini baada ya kuachwa iligundulika baadaye kuwa simu ilikuwa
imezimwa na alikuwa haongei na mtu yeyote.
0 COMMENTS:
Post a Comment