Kutokana na mwenendo wa kusuasua wa Simba katika Ligi Kuu Bara, beki
wa kati wa timu hiyo, Joseph Owino, raia wa Uganda, amekiri kwa kusema kwamba
hawana chao msimu huu, hivyo wanaziachia Simba, Yanga, Azam na Mbeya City
zipambane zenyewe kwenye tatu bora.
Owino ambaye amekuwa nahodha wa mechi kadhaa baada ya Said Nassor
‘Chollo’ kuwekwa benchi huku Amri Kiemba akiwa na matatizo ya kifamilia,
alisema kwamba ni kama wamepitiwa na upepo mbaya, hivyo ni bora wakamilishe
ratiba, ligi imalizike waanze upya msimu ujao.
Alisema kwamba kwa hali jinsi ilivyo ni vigumu kuwaahidi mashabiki
kwamba watafika nafasi ipi kabla ya ligi kuisha kutokana na ushindani na kasi
iliyopo baina ya Mbeya City, Yanga na Azam kwenye nafasi za juu msimu huu.
“Ukiangalia timu yetu ni nzuri tu wala si mbovu lakini ni kama upepo
mbaya umetupiga msimu huu, kwa hiyo ngoja tukamilishe ratiba ligi imalizike,
tuanze upya kwa nguvu mpya.
“Mechi nyingi huwa tunacheza sisi mpira lakini utashangaa baadaye ndiyo
tunafungwa au tunatoka sare, kwa jinsi hali ilivyo ni ngumu kusema kwamba
tutafika nafasi fulani, msimu huu tuwaache tu Yanga, Azam na Mbeya City ambao
wanaonekana wapo vizuri waendelee kupambana,” alisema Owino.
0 COMMENTS:
Post a Comment